TIMU za Simba na Yanga zimetamba sasa zimeimarika baada ya wachezaji
wao kurejea nchini wakitokea Ethiopia walikokuwa katika michuano ya
Kombe la Chalenji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti makocha wa timu hizo
walisema wanaamini kuanzia leo wachezaji hao watakuwa wamejiunga na
vikosi vyao na maandalizi yatakuwa yamekamilika.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der
Pluijm, amesema wiki hii amepanga kubadilisha programu ya mazoezi kwa
vile tayari atakuwa na wachezaji wake wote.
Kwa muda wa wiki tatu Yanga imekuwa ikifanya mazoezi kwenye uwanja wa
Boko Veterani, huku ikitumia idadi kubwa ya wachezaji wa timu ya
vijana, baada ya wale wa kikosi cha kwanza wengi wao kuwa Ethiopia
katika michuano ya Chalenji.
“Nimefurahi kuona idadi kubwa ya wachezaji wangu wa kikosi cha kwanza
tayari wamerudi kundini, mikakati yangu kuanzia sasa ni kubadili
mpangilio wa mazoezi na kuongeza mkazo kuhakikisha timu inarudi kwenye
kiwango chake, ili tuweze kupata matokeo mazuri kwenye mechi zetu za
ligi,” alisema.
Alisema ana uhakika na wachezaji aliokuwa nao kwenye mazoezi na hata
wale waliokuwa kwenye timu za taifa, lakini anachotaka kufanya ni
kubaini utimamu wao ili kujua upungufu uliopo kabla ya mchezo wao wa
mzunguko wa 10 wa Ligi Kuu dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga mwishoni mwa
wiki ijayo.
Wachezaji wa Yanga waliokuwa kwenye michuano ya Chalenji Ethiopia ni
Ally Mustapha ‘Barthez’, Kelvin Yondan, Salum Telela, Deusi Kaseke,
Simon Msuva na Malimi Busungu wote wa Tanzania Bara ‘Kili Stars’.
Wengine ambao walikuwa timu ya Taifa ya Zanzibar ni ‘Zanzibar Heroes’
ni Nadir Haroub ‘Cannavar’, Haji Mwinyi, Matheo Simon na Said Juma,
ambapo pia alikuwpeo Amissi Tambwe aliyekuwa na timu ya taifa ya Burundi
na Haruna Niyonzima wa Rwanda.
Kati ya wachezaji hao ni Niyonzima tu ambaye bado yupo Rwanda, ambapo
timu yake ya Taifa leo inacheza mechi ya nusu fainali, wakati wachezaji
wengine timu zao zimeshaondolewa na wamerejea nchini.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr alisema anaamini
kikosi chake sasa kitakuwa imara kujipanga kwa ajili ya mechi ya Ligi
Kuu dhidi ya Azam Jumamosi wiki ijayo. Kerr, ambaye timu yake ipo
kambini Zanzibar, alisema anaamini kutimia kwa kikosi chake kutampa
fursa ya kuwapa mafunzo ya uhakika kwa ajili ya ligi hiyo.
Wachezaji wa Simba waliokuwa Kilimanjaro Stars ni Hassan Kessy, Jonas
Mkude, Said Ndemla, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, wakati kwa Zanzibar
Heroes ni Awadh Juma na Samir Haji Nuhu Pia yupo Juuko Murshid
anayechezea timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ambayo leo inacheza
nusu fainali.
“Kambi yetu hapa Zanzibar imeanza kupendeza baada ya wachezaji baadhi
waliokuwa Ethiopia kuripoti kambini, tunaamini kuanzia kesho (leo) wote
watakuwa wameshafika kambini,” alisema kocha huyo. Kwa upande wake
Mratibu wa Simba mjini Zanzibar, Abbas Suleiman alisema jana kuwa timu
yake leo itacheza na Kimbunga katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Amaan.
0 comments:
Post a Comment