MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetangaza kuanza kutoa mashine za
kielektroniki za kodi (EFDs) bure kwa wafanyabiashara stahiki 200,000.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango hatua hiyo
itakuwa endelevu, huku ukilenga kutanua zaidi wigo wa kukusanya kodi.
Kabla ya uamuzi huo wa TRA, kwa takribani miaka miwili kuliibuka
mvutano baina ya wafanyabiashara na TRA, ambapo wafanyabiashara waligoma
kutumia mashine hizo wakitaka Serikali ishughulikie kwanza kero zao
zikiwamo za bei ya mashine, utitiri wa kodi, ukwepaji kodi na urasimu.
Hawakuishia hapo, waliitisha pia mgomo nchi nzima, kabla ya kuanza
mazungumzo ya mara kwa mara na Serikali, ambayo wakati mwingine
hayakufikia ukingoni, hatua iliyofanya baadhi ya viongozi wa
wafanyabiashara kukamatwa.
Hata hivyo, hayo yamebaki kuwa historia baada ya viongozi hao kufutiwa mashitaka.
Akizungumza juzi, Dk Mpango alisema uchambuzi wa wafanyabiashara
wanaostahili kupewa mashine hizo, unaendelea nchi nzima kwa kuangalia
ukubwa wa biashara ili wapewe mashine hizo.
Kutokana na kusudio jipya la TRA na serikali kwa ujumla la kugawa
bure mashine za EFD, sisi wa HabariLeo tunatoa pongezi za dhati kwa
uamuzi huu wa busara unaolenga kujenga mazingira rafiki zaidi ya
ukusanyaji wa kodi, lakini pia kutanua wigo wa ulipaji kodi ambayo
mapato yake serikali inayahitaji kwa udi na uvumba katika kuhakikisha
ustawi wa nchi katika sekta mbalimbali unakua kwa kasi.
Aidha, tunaipongeza mamlaka kwa usikivu, kwani hivi karibuni Rais
John Magufuli aliwapa `darasa’ TRA huku akielezea mshangao wake kwa
mamlaka hiyo kushindwa kugawa bure mashine husika kwa wafanyabiashara.
Alisema TRA walipaswa kubaki na kazi ya kukusanya mapato, huku akisema
muda uliopotea na kodi ambayo haikukusanywa wakati wa mvutano na
wafanyabiashara, ungetosha kununua mashine mpya na kuwagawia.
“Kama mnajua mashine hizi ni halali na ni zenu, wapeni bure kazi yenu
iwe ni kukusanya kodi, ni hesabu rahisi sana isiyohitaji kwenda chuo
kikuu, kwamba muda uliopotea na fedha hazifiki Sh bilioni 12 zingetosha
kununua mashine na kazi iwe ni kukusanya kodi,” alisema Rais Magufuli.
Tunaamini kwa kuwa TRA wamekuwa wasikivu na kuamua kugawa bure
mashine husika, bila shaka roho za wafanyabiashara sasa zitakuwa kwatu
na kuisaidia serikali kukusanya mapato.
Hata hivyo, tunaisihi TRA kuharakisha mchakato wa uchambuzi wa
wafanyabiashara zaidi wanaostahili kulipa kodi, ili wigo wa kukusanya
kodi uwe mpaka, badala ya kubaki na wafanyabiashara wachache,
wafanyakazi walioko katika sekta rasmi ambao hawana ujanja wa kukwepa
kodi kwa kuwa hufyeka kupitia mishahara yao, na kadhalika.
Hili likiwezekana, tuna uhakika kasi ya ukusanyaji mapato itazidi
kupaa, huku Watanzania wakiendelea kuona mabadiliko ya kasi katika
huduma za kijamii na unafuu wa maisha hasa kwa kipindi hiki ambacho Rais
Magufuli ameshikilia msimamo wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,
ili fedha za mlipa kodi zirudi kumnufaisha mlipa kodi kwa njia
mbalimbali.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment