UJENZI wa Barabara ya Bagamoyo kipande cha kutoka Mwenge hadi Morocco
jijini Dar es Salaam,chenye urefu wa kilometa 4.3, kinatarajia
kukamilika ujenzi wake ndani ya miezi sita.
Ujenzi wa barabara hiyo ulianza juzi, ikiwa ni siku moja baada ya
Rais John Magufuli kuamuru fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za
Uhuru, zikajenge barabara ya Bagamoyo kipande cha Mwenge-Morocco.
Taarifa iliyotolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia
Mtendaji Mkuu wake, Patrick Mfugale, ilisema mkandarasi ameshaanza kazi
na anatarajia kuikamilisha ndani ya miezi sita.
“Ujenzi umeanza na utakamilika katika kipindi cha miezi sita,”
ilisema sehemu ya taarifa hiyo huku akiomba wananchi wanaofanya shughuli
zao kando ya barabara hiyo kupisha ili mradi usikwame.
“Ili utekelezaji usikwame, tunaomba wananchi wanaofanya biashara
kandokando ya barabara hiyo, waondoke mara moja, aidha wanaoegesha
magari katika eneo la mradi kipindi hiki cha upanuzi waache mara moja,”
ilieleza taarifa hiyo ya Mfugale.
Aidha, Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA) imewataka watembea kwa miguu na wananchi, kutoa ushirikiano
katika kipindi hiki cha upanuzi wa barabara hiyo ili kufanikisha ujenzi
ndani ya muda uliopangwa.
Juzi gazeti hili lilishuhudia tingatinga mbili, mali ya kampuni ya
ukandarasi ya Estim katika eneo la Mwenge zikisafisha eneo la barabara
hiyo, ikiwa ni maandalizi ya upanuzi kama maagizo ya Rais yalivyosema.
Dk Magufuli aliamuru Sh bilioni 4 zilizopaswa kutumika kugharamia
sherehe za sikukuu ya Uhuru, ambazo zingefanyika Desemba 9, mwaka huu,
kutumika kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco yenye
kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Tayari fedha hizo zimepelekwa Tanroads kwa ajili ya kutekeleza agizo
hilo. Dk Magufuli alimwagiza Mfugale, walipokutana Ikulu Dar es Salaam
mapema wiki hii, kuwa ujenzi wa barabara hiyo uanze haraka ili
kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika barabara hiyo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment