SHIRIKISHO la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeunga
mkono kazi inayofanywa na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu wake, Kassim
Majaliwa kwa kuwa kinachofanywa na viongozi hao, ndicho ambacho
wafanyakazi wamekuwa miaka yote wakitaka Serikali zilizotangulia,
zifanye ili maslahi yao yawe mazuri.
Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya alisema hayo jana
alipozungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Tucta, Dar es
Salaam. Tangu ashike madaraka siku 28 zilizopita, Rais Magufuli
amevutia wengi katika utendaji wake baada ya kuamua kushughulikia kwa
haraka matatizo yanayogusa maisha ya Watanzania wengi.
Alianzia kwa ziara ya kushitukiza katika Hazina ya Taifa (Wizara ya
Fedha), kabla ya kushitukiza kwa ziara ya Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) na kisha kwa kupitia Waziri Mkuu Majaliwa akaibukia katika Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), ambako uliibuliwa ufisadi wa makontena
ulioleta hasara ya Sh bilioni 80.
Aidha, Dk Magufuli alipiga marufuku sherehe za Sikukuu ya Uhuru na
maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, na kupiga marufuku uchapishaji wa
kadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa gharama za fedha za umma.
Amezuia pia safari holela za watumishi wa umma nje ya nchi, akitaka
zifanyike kwa kibali maalumu.
Awali pia aliagiza fedha zaidi ya Sh milioni 200 zilizokuwa zitumike
kwa ajili ya mchapalo wa sherehe za uzinduzi wa Bunge la 11 mwishoni mwa
mwezi uliopita, zitumike kwa ajili ya kununua vitanda vya wagonjwa
katika Hospitali ya Muhimbili na fedha za Uhuru zitumike kupanua
barabara ya Bagamoyo jijini Dar es Salaam katika kipande cha kutoka
Morocco kwenda Mwenge.
Ni kutokana na utendaji huo, Tucta kupitia kwa Kaaya imesema mara
zote wamekuwa wakiiambia Serikali kuwa ina uwezo wa kulipa wafanyakazi
wake mishahara mizuri kama itakusanya mapato yake inavyotakiwa. “Bila
shaka hatukueleweka.
Tulisema suala la ukusanyaji hafifu wa kodi, tulisema suala la
wakwepaji wa kodi, wizi wa fedha za umma, misamaha ya kodi na ubadhirifu
mkubwa wa fedha za umma kwenye halmashauri zetu,” alisema Kaaya
akizungumzia hatua kali alizoanza kuchukua Dk Magufuli katika kukusanya
na kudhibiti mapato.
Kaaya alisema Tucta inaunga mkono kasi ya ‘kutumbua majipu’ na
kuwataka Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuunga mkono kazi
hiyo kubwa ya Rais Magufuli ya kurejesha nchi mahali pake.
Hata hivyo, alikemea na kukataa mtindo ulioibuka hivi karibuni kwa
watawala kutumia nafasi zao kuwakandamiza wafanyakazi kwa kisingizio cha
kaulimbiu ya Rais Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu.’
Alisema kauli hiyo ya rais wote wanaikubali na wameona inavyofanya
kazi, lakini wapo viongozi wachache wenye madaraka wanaotumia kaulimbiu
hiyo, kujionesha kuwa wanakwenda sambamba na kasi ya Magufuli.
Alisema hivi karibuni kuna mkuu wa wilaya ambaye aliamuru maofisa wa
ardhi watupwe rumande, amri anayoieleza haikuwa sahihi na ilikwenda
kinyume cha sheria za kazi na haki nyingine za msingi za binadamu.
“Wale wafanyakazi hawakutenda kosa lolote la jinai. Sheria na
taratibu za kazi ziko wazi kuhusu hatua za kinidhamu kwa wafanyakazi
wanaokiuka maadili ya kazi. Tucta tunalaani kitendo hicho na wafanyakazi
hao wana haki ya kumshitaki mkuu huyo wa wilaya na sisi tunawaunga
mkono,” alisema Kaaya.
Pia katika kipindi hiki, kiongozi huyo wa Tucta alisema kumekuwa na
kauli ya mkuu wa mkoa mmoja, akiwakataza maofisa wake kwenda likizo, eti
kwa vile rais yuko kazini na hajakwenda likizo.
Alisema ieleweke kuwa likizo ni haki ya mfanyakazi na kama kuna
mwajiri anataka kuzuia likizo hiyo, anapaswa kufanya majadiliano na
mwajiriwa ili wakubaliane kulingana na taratibu za sheria zilizopo.
Alisema kauli nyingine imeelekeza mashirika ya umma yasiyojiendesha kwa
faida, yapunguze wafanyakazi.
“Tunapenda ieleweke kuwa kinachofanya mashirika ya umma yashindwe
kujiendesha sio wingi wa wafanyakazi, bali ni uongozi mbovu wa mashirika
hayo,” alisema na kuongeza kuwa uongozi mbovu unatokana na uteuzi wa
wakuu wa mashirika hayo usiozingatia weledi, bali kujuana na urafiki.
‘Hapa Kazi Tu’ ni kaulimbiu ambayo Dk Magufuli aliitumia wakati wa
kampeni za Uchaguzi Mkuu na baada ya kuapishwa kuwa rais, amekuwa
akionesha utekelezaji wa kauli hiyo kwa vitendo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment