HALMASHAURI ya wilaya ya Morogoro na
Manispaa ya Morogoro wamefanikiwa kuandikisha jumla ya wanafunzi 9,943
watakaojiunga na darasa la kwanza na shule ya awali katika kipindi cha mwaka
2016.
Wakizungumza kwenye kikao
kilichohusisha maafisa elimu wa halmashauri hizo za wilaya na wadau wengine wa
elimu,Kaimu Afisa elimu ya msingi katika Manispaa ya Morogoro Christopher
Wangwe amesema wamefanikiwa kuandikisha wanafunzi 4,406 wakiwemo 2,978 wa elimu
ya awali na 1,428 wa darasa la kwanza.
Wangwe amesema uandikishwaji huo
umefanya idadi ya walioandikishwa kufikia 4,109 ni sawà na asilimia 56 ya
malengo yaliyokusudiwa na kwamba asilimia 44 zilizosalia zinatarajiwa
kumaliziwa katika uandikishaji unaoendelea katika kipindi cha Januari mwakani.
Naye Afisa elimu ya msingi katika
wilaya ya Morogoro Donald Pambe amesema halmashauri hiyo imeandikisha wanafunzi
3,560 wa shule ya awali na 3,556 wa darasa la kwanza na kufanya jumla ya
walioandikishwa kufikia 7,116.
Akizungumza katika kikao hicho,Mkuu wa
wilaya ya Morogoro Muhingo Rweyemamu amewaagiza maafisa elimu na wale wote
wanaohusika na elimu kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule
wakiwemo wale wenye umri wa hadi miaka 15 ambao wengi ni watoto wa jamii ya
wafugaji wanaandikishwa shule katika elimu ya awali na elimu ya msingi.
Rweyemamu amesema wilaya hiyo ya
Morogoro imezungukwa na jamii ya wafugaji na kwamba wengi wa wazazi hawana
tamaduni za kupeleka watoto shule badala yake huwaelekeza kuchunga mifugo na
wengine kuwakatiza masomo kwa kuhama hama,jambo ambalo Serikali haikubaliani
nalo.
Amesema Serikali imetenga fedha kwa
ajili ya kusomesha wanafunzi bure hivyo mzazi hana haja ya kuwa na visingizo
vitakavyofanya mtoto wake kukosa elimu na kuonya watakaokaidi sheria itachukua
mkondo wake kwa kuwachukulia hatua kali wazazi watakaobainika kupinga agizo
hilo.
0 comments:
Post a Comment