Wawakilishi wa makundi ya upinzani nchini Syria yameanza mazungumzo
yanayodhaminiwa na Saudi Arabia, yenye lengo la kusaka msimamo mmoja
katika mazungumzo yanayotarajiwa baina yao na utawala wa rais Bashar
al-Assad.
Ingawa makundi yote ya upinzani hayakualikwa katika mkutano huo
unaofanyika mjini Riyadh, ni mara ya kwanza kwa makundi mengi ya kisiasa
na kijeshi kukaa pamoja tangu kuanza kwa mzozo wa Syria mwaka 2011.
Lengo kuu la mkutano huo unaohudhuriwa na wajumbe 100 ni kuweka kundi
moja litakalowakilisha wapinzani wote katika mkutano na serikali ya
Assad, ambao nchi zenye nguvu duniani zinaamini utafanyika kabla ya
mwaka huu kumalizika.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Saudi Arabia Adel al Jubeir ambaye
ameonya mara kadhaa kwamba ikiwa rais Assad hataki kuachia madaraka kwa
amani anaweza kulazimishwa kijeshi kufanya hivyo, amehudhuria mkutano
huo kwa muda mfupi kuwakaribisha wajumbe na kuwatakia mafanikio.
Msimamo mmoja miongoni mwa wapinzani
Mwenyekiti wa muungano wa wapinzani wa Syria Khaled Khoja amesema makundi mengi yaliyowakilishwa yana maoni sawa.
''Makundi mengi ya upinzani yaliyoundwa nchini Misri, Dubai na nchi
nyingine , yamewasilishwa na kamati zao'' amesema Khoja, na kuongeza
kuwa kumekuwepo mawasiliano, na mengi ya makundi hayo yanakubaliana
kuhusu mtazamo wa kisiasa juu ya mchakato wa kipindi cha mpito, na hivyo
maoni yetu ni kwamba njia mwafaka ni kupata maafikiano.''
Mkutano huo ambao unafanyika katika hoteli ya kifahari yenye ulinzi
mkali, na unaongoza na Abdulaziz Sager, msaudia ambaye pia ni mwenyekiti
wa kituo cha utafiti cha Ghuba ambacho kiko mjini Geneva. Shirika la
habari la Saudi Arabia limesema kuwa mkutano huo pia umeitikiwa na
makundi mengi ya upinzani kutoka ndani ya Syria.
Kulingana na ratiba ya mazungumzo, siku ya kwanza imejikita juu ya
sura ambayo muafaka wa kisiasa inaweza kupewa, na siku ya pili, kesho
Alhamis, wajumbe watajadili tatizo la ugaidi, usitishaji mapigano na
mchakato wa kuijenga upya Syria.
Khoja ambaye muungano anaouongoza wa National Coalition una makao yake
mjini Istanbul, amesema anayo matumaini kwamba mkutano huo utafanikiwa
kuunda kundi moja la uwakilishi katika mazungumzo, na pia juu ya nguzo
kuu za mazungumzo baina yao na serikali ya Rais Bashar al Assad.
Makundi yenye silaha yanayoaminika kuwa ya kigaini, kama vile Dola la
Kiislamu, na al-Nusra Front hayakualikwa katika mazungumzo hayo ya mjini
Riyadh, lakini washirika wa al-Nusra, Ahrar al-Sham wamethibitisha
kushiriki kwao, hali ambayo imeyafanya baadhi ya makundi mengine
kujiondoa katika mazungumzo hayo.
Kundi jingine ambalo limetengwa katika mazungumzo hayo ni lile la Syrian
Democratic Forces linaloungwa mkono na Marekani, ambalo linawajumuisha
wakurdi, wasuni na wakristo wanaolipinga kundi la IS.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment