WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa
siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Eng. John Ndunguru kukamilisha
uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi juu ya tuhuma ubadhirifu wa
fedha za umma unaohusisha uuzwaji wa jengo la KIGODECO na viwanja 12 vya
Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka taratibu.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati
akizungumza na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa akifanya
majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkonai humo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema anazo
taarifa kuwa jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na jengo jingine
la MIBOS kwa sh. milioni 50/- licha ya kupewa barua na Mkuu wa Mkoa huo
kusitisha uuzwaji wa jengo pamoja viwanja hivyo, bado liliuzwa.
“Katibu Tawala wa Mkoa kaa na
Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu na unipatie taarifa kwa
maandishi ifikapo Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu huku akishangili
“Nataka kujua nani alifanya tathmini
ya jengo, ni kwa nini jengo liliuzwa kwa thamani hiyo, je ndiyo thamani halisi
ya jengo? Ni kwa nini RC alipozuia, utaratibu uliendelea? Je, utaratibu wa
uuzaji ulifuatwa? Ni kwa nini viwanja viliuzwa chini ya thamani,? Katibu Tawala
kaa na watu wako na uniletee hiyo taarifa kwa maandishi. Tukigundua kuna
mianyamianya tutachukua hatua za kinidhamu,” alisema.
Viongozi walioagizwa kukutana na
Katibu Tawala wa Mkoa ni Mkurugenzi wa Manispaa, Eng. Boniface Nyambele;
Mhandisi wa Manispaa, Eng. Boniface William na Mhasibu wa Mapato wa Manispaa,
Ndg. Bawili Mkoko.
Kuhusu uuzwaji wa jengo na viwanja,
imebainika kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Luteni Kanali (Mst), Issa Machibya alizuia
uuzaji huo kwa barua ya tarehe 16 Juni 2015 akitaka viwanja hivyo vitumike kwa
matumizi ya manispaa na mchakato huo usitishwe hadi mwakani lakini agizo lake
lilipuuzwa na jengo likauzwa kwa sh. milioni 370 ambayo ni bei ya kiwanja
pekee.
Tuhuma nyingine zinazopaswa
kuchunguzwa ni pamoja na matumizi ya sh. milioni 809 kwa ajili ya ujenzi wa
maabara. Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya maendeleo
(Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya
Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji (Tanzania Strategic Cities
Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (SEDP).
Inadaiwa kwamba Mkurugenzi huyo kwa
kushirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya mipango na fedha walitumia
ujenzi wa maabara kama kigezo cha kuchota fedha hizo bila kutoa taarifa kwa
wakuu wa idara husika ambao walikasimiwa fedha hizo.
Tuhuma nyingine ni manunuzi hewa ya
vipuri (spare parts) vyenye thamani ya sh. milioni 8 na manunuzi hewa ya
stationeries yenye thamani ya sh. milioni 4.6/-. Haya yanadaiwa kufanywa Julai
25, mwaka huu na Mkurugenzi huyo akishirikiana na Mhasibu Mkoko.
0 comments:
Post a Comment