WACHEZAJI mbalimbali wa soka waliopata kuwa
manahodha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ wamezungumzia hatua ya nahodha wa timu
hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kujiuzulu kuchezea timu hiyo, huku baadhi
wakimshauri afute uamuzi wake.
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime amemtaka
Cannavaro kufuta uamuzi wake wa kujiuzulu Taifa Stars kwani mchango wake
unahitajika.
Maxime ambaye aliwahi pia kuwa nahodha wa Stars
wakati ikiwa chini ya Mbrazil, Marcio Maximo, alisema alichofanya beki huyo si
sahihi.
Hivi karibuni kocha wa Stars, Charles Mkwasa alimpa
unahodha mchezaji wa TP Mazembe ya Congo DR Mbwana Samatta na kusema Haroub
atabaki kuwa nahodha kwenye timu inayoshiriki michuano ya ndani ya Afrika
(Chan).
Akizungumza na gazeti hili jana, Maxime alisema
suala la unahodha mwenye uamuzi ni kocha, hivyo Cannavaro hana budi kukubaliana
na maamuzi hayo na kwa nafasi anayocheza kwa sasa timu ya taifa bado
anahitajika.
“Kwa nafasi ya mabeki wetu, Cannavaro bado
anahitajika sana kwenye timu, arudi tu mchango wake bado unahitajika sana
ingawa kujiuzulu ni utashi wake mwenyewe, lakini anahitajika bado ana uwezo na
ana nidhamu nzuri,” alisema.
Akifafanua zaidi suala la nafasi ya nahodha, Maxime
alisema: “Suala la kocha kumnyang’anya unahodha Cannavaro inaweza kuwa si
sahihi au sahihi, yote kwa yote. “Sahihi kwasababu kocha ndio anaamua nani awe
nahodha, kwani wachezaji wake anawafahamu vizuri, lakini pia unahodha hauna
barua unajua maana hayo ni maamuzi ya kocha, mimi nadhani Cannavaro aelewe tu
na si kweli kwamba amedharaulika,” alisema.
Naye nahodha mwingine wa zamani wa Taifa Stars,
Peter Manyika ameungana na Maxime kwamba mchezaji huyo wa Yanga anapaswa
kufanya kazi yake kwani uamuzi wa kuteua nahodha ni wa kocha.
“Kocha ndio anateua nahodha kwa sababu ndio bosi kwa
hiyo kama ameamua basi atakuwa na sababu za msingi na hatuwezi kumuingilia
sababu zake,” alisema.
Kuhusu kujiuzulu kwa Cannavaro, Manyika alisema hilo
ni jambo la utashi wa mtu ingawa upande wake anaamini bado alistahili kuwepo
kwenye timu.
“Kujiuzulu kila mtu ana upeo wake, unahodha unajua
ni kitu kizito labda sababu za kuvuliwa kwake hazijamridhisha hatuwezi kujua
kinachotakiwa hapo ni suluhisho ambalo naamini litafanywa na kocha na mchezaji
mwenyewe,” alisema Manyika.
Tangu kufanyika kwa maamuzi hayo Cannavaro amekuwa
akilalamika kwenye vyombo vya habari kwamba hakutendewa haki kwa namna
alivyovuliwa unahodha. Lakini Mkwasa akizungumza na gazeti hili, alisema
hajamvua unahodha Cannavaro bali alichokifanya ni mabadiliko ya kawaida kwenye
timu.
“Sikuwa na sababu ya kumuondoa kwenye unahodha,
namheshimu sana Cannavaro (Haroub) na ametoa mchango mkubwa kwa taifa hili na
bado namhitaji, kwa nini nimuondoe,” alisema.
“Nilichokifanya ni mabadiliko kidogo tu kwenye kazi
ni kama nyinyi huko kuna Mhariri wa Habari na Mhariri wa Michezo, ndivyo
nilivyofanya mimi na hili lipo duniani kote, hata ukiangalia wenzetu Ivory
Coast, Cameroon Zambia, Uganda na hata Rwanda… “Sasa hivi kuna mashindano ya
Chan yanaendelea lazima utakuta nahodha wa Afcon sio yule wa Chan,” alisema.
Beki huyo ametangaza kujiondoa Taifa Stars kutokana
sababu mbalimbali lakini mojawapo ikiwa ni kuvuliwa unahodha bila kupewa
taarifa, ingawa kocha alisema alimjulisha.
0 comments:
Post a Comment