Donald Trump, anayetafuta tiketi ya kuwania urais
Marekani kupitia chama cha Republican ameungwa mkono na gavana wa zamani wa
Alaska Sarah Palin, aliyewania kiti cha makamu wa rais uchaguzi wa 2008.
"Mko tayari kumuunga mkono Trump?” Bi Palin
aliwauliza wafuasi waliokuwa wakimshangilia katika mkutano wa kampeni Iowa.
Alikuwa mgombea mwenza wa John McCain mwaka 2008
waliposhindwa na Barack Obama.
Licha ya kustaafu kutoka kwenye siasa na kujitosa
katika bahari ya vyombo vya habari, yeye bado ana wafuasi wengi hasa miongoni
mwa wahafidhina.
Akitangaza rasmi kumuunga mkono Bw Trump, Bi Palin
amesema mgombea huyo ni mtu ambaye yuko tayari kuwawezesha wanajeshi wa
Marekani kuangamiza kundi linalojiita Islamic State.
"Tuko tayari kwa mabadiliko,” amesema katika
mkutano huo mjini Ames, Iowa.
"Yeye anatumikia “sisi raia”, hatumikii mtu
mwingine. Yuko kwenye nafasi nzuri sana ya kuirejeshea Marekani hadhi yake
tena.”
Bw Trump baadaye kupitia taarifa amesema anajivunia
kuungwa mkono na Bi Palin.
Bi Palin alikuwa amehudumu kama gavana wa Alaska
miaka miwili alipoteuliwa na John McCain kuwa mgombea mwenza wake.
Alikuwa akivutia umati mkubwa wa watu mikutanoni na
kuangaziwa sana na vyombo vya habari.
Baada ya uchaguzi mwaka 2009, alijiuzulu wadhifa wa
ugavana na akaanza kufanya kazi kama mwandishi wa habari na mdadisi wa masuala
ya kisiasa.
Kabla ya kutangaza kumuunga mkono Bw Trump, Bi Palin
alikuwa amesambaza makala ya mtandaoni iliyoandikwa na bintiye Bristol ambayo
inamshambulia mpinzani mkubwa wa Trump katika jimbo muhimu la Iowa, Ted Cruz.
Jimbo hilo ndilo litakalokuwa la kwanza kupiga kura
za kuamua mgombea.
Bw Cruz hata hivyo amemsifu Bi Palin akisema
"bila uungwaji mkono wake, singekuwa katika bunge la seneti”, akirejelea
uungwaji mkono aliopata wakati wa duru ya pili ya uchaguzi wa useneta mwaka
2012.
"Bila kujali atakayofanya 2016, nitabaki kuwa
mfuasi wake mkuu,” ameandika kwenye Twitter.
0 comments:
Post a Comment