Wakati fukuto la bomoabomoa likiendelea katika
maeneo mbalimbali nchini, imedaiwa kuwa mamia ya watu wanaooneka kwenye maeneo
ambayo nyumba zimebomolewa, si waaathirika bali hukaa humo mchana tu.
Uchunguzi uliofanywa na Tambarare Halisi katika eneo
la Mkwajuni, jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa matapeli hao wamefikia
hatua ya kujenga vibanda kwenye vifusi ambavyo serikali ilibomoa nyumba za
wahusika.
Licha ya kuwapo kwa matapeli hao, gazeti hili
lilibaini pia kwamba watu wachache waliobomolewa nyumba zao katika eneo hilo,
bado wanaishi hapo kutokana na kile walidai ni kukosa sehemu ya kwenda.
Wizara ya Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc),
lilibomoa zaidi ya nyumba 600 za wakazi wa eneo la Mkwajuni waliokuwa
wamezijenga pembezoni mwa Mto Msimbazi. Juzi pia serikali ilivunja
vibanda 186 vilivyokuwa vimejengwa juu ya vifusi hivyo.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo,waliiambia Tambarare Halisi kwamba baadhi ya watu waliondoka eneo hilo hata baada ya
bomoabomoa, lakini baada ya kusikia kuna uwezekano wa kupewa fidia, wakaamua
kurudi.
“Si kwamba hawa si wakazi. Walikuwa hapa na
nyumba zao tunazifahamu, sema wenzetu kidogo wamefanikiwa kuhama lakini baada
ya kusikia kuna kuorodheshwa majina,wamerudi ili wapate chochote kitu endapo
serikali itatoa msaada,” alisema Fatma Abasi.
Alisema walio na mahitaji ya kweli hawakuondoka eneo
hilo tangu Desemba 17 walipoanza kubomolewa.
Fatma ambaye awali alijenga kibanda
kilichoezekwa na mabati na mbao lakini kikabomolewa wiki iliyopita, kwa
sasa amejiegesha kado ya bonde hilo akisubiri kupata msaada wa aina yoyote
kutoka serikalini.
“Nina watoto wawili na mume, maisha tunayoishi ni ya
kulala hapa unapopaona (mwonekano wa nzi na majitaka yaliyotuama) hakuna
masaada wowote na sina pa kwenda na familia yangu ndiyo maana hadi leo nimekaa
hapa,” alisema Fatma.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Mgasa Wambura, alikiri
kuwapo kwa watu wasio waathirika akisema miongoni mwao ni waliofunga barabara
ya Kawawa juzi kwa kuchoma matairi.
TATHIMINI YAFANYIKA
Jana alfajiri, NEMC na wizara husika, walifanya
tathimini kwenye eneo hilo na kubaini kwamba ni watu saba pekee wanaolala
katika eneo hilo tofauti na hali inayoonekana nyakati za mchana.
Watu hao saba waliokutwa eneo hilo, walikuwa
wamepanga matofali na mabati na kujiifadhi ndani yake.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventure Baya, aliieleza
kwamba walifanya tathimini hiyo alfajiri ili kutambua waathirika halali wa eneo
hilo.
Naye Mwanasheria Mkuu wa NEMC, Heche Suguta,
alisisitiza kuwa wakazi hao wanapaswa kuondoka eneo hilo kwa sababu
wameshaelezwa kuwa ni eneo hatari.
“Tunachotaka ni kuwasaidia lakini badala ya kuondoka
wanaendeleza matukio katika eneo hilo ili waonekane wanaonewa,” alisema Suguta.
POLISI WAKESHA KULINDA USALAMA
Wakati juzi kukiwa kumetokea tukio la wananchi wa
eneo hilo kuchoma matairi barabarani na kusababisha adha kwa watumiaji wa
barabara ya Kawawa, Jeshi la Polisi lililazimika kukesha eneo hilo hadi asubuhi
ili kulinda usalama.
Wakazi wa eneo hilo, walilieleza gazeti hili kuwa
Polisi waliokuwa kwenye magari mawili aina ya Land Rover Defender walikesha
eneo hilo.
“Tulishangaa hadi asubuhi hapa kulikuwa na askari
pamoja na magari yao wakilinda usalama wa hapa,” alisema Tabu Nasoro ambaye kwa
sasa amejiegesha kwenye kibanda kilichoezekwa kwa vitofali na mabati chakavu.
Alibainisha kuwa askari pia walikuwa wakizunguka
eneo hilo mara kwa mara ili kudhibiti uhalifu wa aina yoyote kutokea.
0 comments:
Post a Comment