Serikali wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imeyafunga
masoko mawili ya Longoi na Rundugai, kambi zote za vibarua wa mashamba ya
vitunguu na migahawa isiyo na vyoo kwa muda usiyojulikana katika vijiji vya
kata ya Rundugai ili kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa wa kipindupindu
katika wilaya hiyo.
Mkuu wa wilaya hiyo Bw Antony Mtaka amechukua hatua
hiyo baada ya kulipuka kwa ugonjwa huo ambao ulikuwa haujaingia mkoani
Kilimanjaro kwa muda mrefu ambao hadi jana wagonjwa 35 walikuwa wametibiwa
katika zahanati ya kata ya Rundugai.
Bw Mtaka amesema, masoko na mighahawa hiyo imefungwa
ili kuzuia maambukizi hayo kutokana na msongamano mkubwa katika maeneo hayo na
matajiri wenye mashamba ya vitunguu wameagizwa kujenga vyoo kwa siku saba
na nyumba za kudumu katika mashamba yao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Chemka ambacho kimeathiriwa
zaidi kutokana na shughuli za kilimo Bw Iddi Jacob amesema, ugonjwa huo
umeletwa na watu kutoka vijiji vya wilaya ya Simanjiro ambao huwa wanakuja
katika vijiji vya wilaya ya Hai kufanya kazi za vibarua mashambani.
Mganga mkuu wa wilaya hiyo Dr Paul Chaote amesema,
kati ya wagonjwa 35 walioripotiwa wagonjwa 26 wametoka wilaya ya Simanjiro na
kwamba hadi jana ni wagonjwa watatu tu walikuwa wamebaki katika zahanati ya
kata ya Rundugai akiwemo mtoto mmoja na mwananchi kutoka Singida.
0 comments:
Post a Comment