KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima ameomba radhi
wanachama, viongozi na mashabiki wa klabu hiyo, kufuatia mambo yaliyotokea
dhidi yake na kusababisha kuvunjiwa mkataba kwa utovu wa nidhamu.
Mwishoni mwa mwaka jana, Yanga ilitangaza kuvunja
mkataba na mchezaji huyo kwa utovu wa nidhamu baada ya kuchelewa kuripoti
kwenye kambi ya maandalizi ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania baada ya kumalizika
kwa michezo ya Chalenji nchini Ethiopia alikokuwa akitumikia timu yake ya
taifa.
Akizungumza jana na waandishi wa habari kwenye ofisi
za klabu ya Yanga, Niyonzima alikiri kufanya makosa na kuomba msamaha kwa wale
aliowakosea, lakini pia kuwasamehe waliomkera na kuahidi mashabiki na wanachama
kuwa mambo yamekwisha kwani kilichobaki ni kuangalia mbele.
“Nilipata matatizo na klabu yangu lakini hayakuwa
makubwa kama ambavyo watu hufikiria, nashukuru tumeweza kukaa na uongozi na
kuweza kuyatatua na mpaka sasa tuko hapa, yamefikia pazuri na najua tutaendelea
kufanya kazi,” alisema.
Alisema Yanga ina haki ya kulalamika juu ya kile
alichokifanya kwani alivyokwenda nyumbani kwao kuitumikia timu yake ya taifa
alikuwa na maumivu yaliyomfanya kujitibia mwenyewe huku akikiri wazi hakukuwa
na mawasiliano ambayo yalisababisha yote yatokee.
Alisema: “Kikubwa ni kwamba nilikaa na viongozi
wangu na kuyazungumzia, kuangalia ni wapi nimekosea mimi kama binadamu, na
kufikia pazuri,” alisema.
Niyonzima alisema alishtushwa na uamuzi ambao
ulichukuliwa na klabu hiyo, kwani hakutarajia kitu kama hicho kingetokea.
Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alisema Niyonzima ni mtoto kwao hivyo ana imani
msamaha wake utachukuliwa na wanachama na viongozi wa Yanga na kuufanyia kazi.
Alisema uongozi wa klabu yake unajipanga kutoa
taarifa rasmi kuhusu suala la Niyonzima ambayo itahitimisha mjadala mzima.
“Kwetu sisi Niyonzima ni mtoto, na siku zote mtoto
anapokuja kwako akaunyea mkono haukatwi, unaupangusa na natumaini mashabiki,
wapenzi wa Niyonzima watamsikia alichokisema na viongozi wetu wamesikia aliyosema,
kwa hiyo sisi kama Yanga tumeyapokea kwa mikono miwili, tutayafanyia kazi,”
alisema.
Aliongeza kuwa, “Sisi kama uongozi wa Yanga,
tunamshukuru Niyonzima kwa kuwa muungwana juu ya hili suala na kuamua kuja kwa
uongozi wa Yanga na kuomba radhi kwa yote yaliyotokea, tutatafakari kwa manufaa
ya klabu na kutoa majibu, ” alisema.
Uongozi wa Yanga ulifikia hatua ya kuvunja mkataba
wa mchezaji huyo kufuatia kurudia makosa mara nyingi, kiasi cha kuikera klabu
yake na kuamua kumchukulia hatua hiyo sambamba na kutakiwa kuilipa klabu hiyo
zaidi ya dola za Marekani 71,175 kama fidia inayotokana na mkataba mpya
unaomalizika 2017.
Ingawa suala hilo halijawekwa wazi bado, lakini
habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa mchezaji huyo amerudishwa
kundini na huenda akajiunga na wenzake wiki hii.
0 comments:
Post a Comment