KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamke mmoja
amepanda katika paa la jengo la Wizara ya Fedha na Mipango huku tukio hilo
likizua sintofahamu kwa wafanyakazi wa wizara hiyo na wapita njia.
Tukio hilo lilitokea jana Dar es Salaam majira ya
asubuhi ambapo mwanamke huyo anayedaiwa kuwa raia wa Kenya alipanda juu ya paa
hilo na kuanza kupiga kelele.
Katika tukio hilo inadaiwa mwanamke huyo aliwasili
katika eneo hilo la wizara akionekana kama mmoja wa wananchi ambao walikwenda
kwa ajili ya kupatiwa huduma, lakini baada ya muda alionekana akiwa juu ya paa
huku akipiga kelele.
Mwanamke huyo aliyekuwa amebeba mkoba, ambaye
haikufahamika mara moja nia yake ya kupanda juu ya paa hilo, ilimchukua saa
kadhaa akiwa juu na pale walinzi wanaolinda ofisi za wizara hiyo walipokwenda katika
eneo hilo na kumwomba ateremke aligoma.
Hata hivyo hali hiyo ilionekana kutowakatisha tamaa
walinzi hao wanaolinda majengo ya Wizara ya Fedha na Mipango yaliyopo mita
chache kutoka Ikulu ya Dar e Salaam, ambao walikwenda tena wakiwa na ngazi na
kuanza kumbembeleza ambapo jaribio hilo lilifanikiwa na mwanamke huyo
kuteremka.
Wakati mwanamke huyo akiwa juu ya paa, wananchi
waliokuwa chini walianza kumuuliza maswali, lakini hakusikika majibu yake
kutokana na kelele za watu ambao kila mmoja aliimuuliza swali lake.
Hata hivyo mmoja wa askari wa kikosi cha Usalama
Barabarani ambaye alisogea kwa karibu kumuuliza mwanamke huyo, alisema kuwa
alimwambia amechukua uamuzi huo kutokana na kuteswa na askari nchini Kenya.
“Tukio hili ni la ajabu na linaibua maswali… hivi
inakuwaje kwa jengo kama hili la wizara ambalo lipo jirani na Ikulu mtu
anapanda juu na walinzi wapo?
“Hii inasikitisha sana na ni ajabu kwa kweli, ipo
siku tutakuta watu wanaingia Ikulu na kufanya mambo ya ajabu kwa viongozi
wetu,” alisema mmoja wa wananchi waliokuwa katika eneo hilo ambaye hakupenda
kutajwa jina lake gazetini.
Tambarare Halisi ilipomtafuta Msemaji wa wizara
hiyo,Ingiahedi Mduma ili kuzungumzia suala hilo, alisema kwa sasa yupo mjini
Dodoma katika maandalizi ya vikao vya Bunge na hana taarifa ya tukio hilo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi
Ilala, Lucas Mkondia, alisema hajapata taarifa hizo na kwamba atafuatilia tukio
hilo.
“Hatujapata taarifa hizo, ndiyo kwanza nasikia
kutoka kwako, labda tufuatilie,” alisema Kamanda Mkondia.
0 comments:
Post a Comment