TIMU za Simba na Azam leo zinashuka katika viwanja
tofauti katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Simba itakuwa mgeni wa JKT
mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, wakati Azam FC itakuwa
mgeni wa Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 30,
Azam ya pili ikiwa na pointi 36 sawa na vinara Yanga wakitofautiana uwiano wa
mabao ya kufunga na kufungwa.
Mchezo wa Dar es Salaam unazikutanisha timu mbili
zenye mazingira tofauti, ambapo imetoka kushinda mchezo wake dhidi ya Mtibwa
Sugar bao 1-0 mwishoni mwa wiki iliyopita ikiwa chini ya Kocha Msaidizi Jakson
Mayanja.
Hata hivyo inakutana na JKT Ruvu, ambayo imetoka
kupata kichapo cha mabao 5-1 dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga, ambacho kiliwastua
kwa kuwa walikuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani. Kutokana na hali hiyo ni wazi
Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Abdallah Kibadeni atataka kushinda ili kuiweka sawa
timu yake.
Kwa upande wa Azam inayokutana na Mgambo itakuwa na
kibarua kizito kutokana na timu hiyo kuwatesa vigogo kwenye uwanja wao wa
Mkwakwani. Timu hizo ziliwahi kukutana wakati Azam ikijiandaa na maandalizi ya
michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa
kirafiki uliochezwa mkoani huko.
Pia, Azam imetoka kupata sare dhidi ya African
Sports ya Tanga katika mchezo wa ligi uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kama Azam itateleza leo kisha Yanga ikashinda kesho dhidi ya Majimaji itakuwa
imeweka pengo kubwa kati yake na Yanga.
Mechi nyingine leo itakuwa kati ya Ndanda FC ikiwakaribisha
Mbeya City kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Ndanda sio timu rahisi licha ya kuwa hawako katika
nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, wamekuwa wakitingisha timu kubwa. Pia,
Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Sokoine
jijini Mbeya.
Timu hiyo ya Tanga iko kwenye hatari ya kushuka
daraja, hivyo ushindi ni muhimu kuhakikisha inajinasua kwenye hatari. Kwa
upande wa Stand United itakuwa mwenyeji wa Toto Africans kwenye Uwanja wa
Kambarage Shinyanga. Timu hizi zinajuana na zimekuwa zikionesha kandanda safi.
0 comments:
Post a Comment