DILI la wachezaji wa Azam FC, Kelvin Friday na Farid
Mussa kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania limekuwa gumu.
Friday alifuzu kucheza katika klabu ya St. George ya
Ethiopia baada ya kwenda kufanya majaribio ya wiki mbili hivi karibuni, wakati
Mussa alikuwa anatakiwa na timu moja ya Slovenia iliyokuwa imeweka kambi
Hispania.
Akizungumza na gazeti hili, Mtendaji Mkuu wa Azam
FC, Saad Kawemba alisema kuwa Friday baada ya kufuzu, timu hiyo ya Ethiopia ilisema
ingekuja kufanya mazungumzo lakini haifanya hivyo.
“St. George ilionesha nia kwa sababu mchezaji
alishafuzu, lakini baadaye hawakuonekana tena, kwa hiyo mchezaji mwenyewe kwa
sababu tulimpeleka Mtibwa kwa mkopo tukamwambia aendelee na timu hiyo,” alisema.
Aidha, kwa upande wa Mussa, Kawemba alisema wakati
timu iko Zanzibar walikuwa wakimhangaikia mchezaji na alikuwa tayari amepata
hati ya kusafiri, lakini kilichotokea kuna baadhi ya vitu walitakiwa kuwa
navyo.
“Mambo yalikuwa yanaenda vizuri, tulipata hati ya
safari kule ubalozini lakini kuna vitu walihitaji tuwape na kwa wakati huo
hatukuwa navyo, kwa hiyo nikamwambia mchezaji aende Zanzibar kujiunga na
wenzake na baadaye tutaendelea,” alisema.
Kawemba alisema kwa vile Mussa bado umri wake ni
mdogo wataendelea kumuimarisha kiwango chake kwa kuwa bado kuna timu za Ulaya
zimeonesha nia ya kumhitaji na mambo yakiwa sawa wataweka wazi.
0 comments:
Post a Comment