Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri
wa Majini na Nchikavu (Sumatra-CCC), limepinga vikali nauli zilizopendekezwa na
kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT) kwa ajili ya mabasi yaendayo kasi. Baraza
hilo lilipinga nauli hizo juzi wakati wa kikao kilichohusisha wadau wa usafiri
na wananchi jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kiliitishwa kwa ajili ya kujadili
nauli zilizopendezwa na UDA-RT kwa ajili ya huduma za mabasi yaendayo kasi
jijini Dar es Salaam. Nauli zilizopendekezwa ni kiasi cha Sh.
700 kwa njia za mlisho, Sh. 1,200 kwa njia kuu na
Sh. 1,400 kwa mlisho wa njia kuu. Sumatra-CCC imepinga nauli hizo kwa maelezo
kuwa ni za juu kutokana na ukweli kuwa watumiaji wengi wa usafiri huo ni
walalahoi.
Hata hivyo, UDA-RT wanapinga malalamiko hayo wakidai
kuwa nauli waliyopendekeza itawasaidia kumudu gharama za uendeshaji wake.
Sababu mojawapo wanayoeleza kuwa ni mabasi hayo hayatakuwa yanasubiri abiria
vituoni na kulazimika nyakati fulani kubeba abiria wachache kutokana na muda.
Pia wanadai kuwa mabasi ni ya kisasa, ambapo ni
gharama kubwa kuyaendesha. Hata hivyo, pamoja na yoye, tunadhani kuwa serikali
inapaswa kulisimamia suala hili kwa kuangalia hali ya mwananchi mwenye kipato
kidogo.
Bahati nzuri serikali imeliona hili na kutoa taarifa
kupitia Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, kuwa haijaridhia mapendekezo hayo ya nauli
kwa kuwa mradi huo ulianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi hasa waishio
nje ya jiji.
Moja ya madhumuni makubwa ya serikali kuanzisha
huduma za usafiri wa umma ni kusaidia watu wenye kipato kidogo wasiomudu
kununua magari. Pia ni mfumo mzuri wa kupunguza msongamano wa magari ikiwa
huduma zitatolewa vizuri kwani zitafanya hata wenye magari kuyaacha majumbani.
Serikali ilipaswa kuangalia suala la usafiri wa umma
kama huduma kwa wananchi wake na sio suala la watu kuachiwa kutengeneza faida
kubwa. Suala la utoaji wa huduma za usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam
halijaanza leo, kwani wakati wa kipindi cha utawala wa kikoloni wa Mwingereza
ilikuwapo Kampuni ya Stage Coach kabla ya kuundwa kwa Shirika la Usafiri Dar es
Salaam (UDA) baada ya uhuru ili kutoa huduma ya usafiri. Kwa kuwa wananchi
wanafanya shughuli mbalimbali zinazoliingizia taifa kodi, basi iangalie kuwa
suala la usafiri kama huduma ya kuwasaidia wananchi kufika maeneo ya uzalishaji
na si biashara. Madhumuni ya kuanzishwa kwa mradi huu wa mabasi yaendayo kasi
ilikuwa kupunguza foleni katika jiji la Dar es Salaam. Sio siri suala la foleni
katika jiji la Dar es Salaam limekuwa kero kubwa katika maisha ya kila siku
katika jiji hili. Hali hiyo inachangiwa zaidi kutokana na uchache wa barabara
uliochangiwa zaidi na mipango miji mibovu.
Bahati mbaya idadi ya wakazi za jiji la Dar es
Salaam imekuwa ikiongeza, huku kukiwa na mipango miji mibovu.
Matokeo yake namba ya wakazi imekuwa kubwa na maana
yake idadi ya watu wanaomiliki magari imeongezeka zaidi.
Moja ya madhumuni makubwa ya utoaji wa usafiri kwa
umma ni kurahisisha watu kutoka upande mmoja kwenda mwingine, hivyo tunashauri
serikali isimamie jambo hili kuhakikisha kuwa huduma ya mabasi yaendayo kasi
inalenga kusaidia wananchi wa kuanzia wa kipato cha chini hadi juu.
Itakuwa jambo la kusikitisha ikiwa nauli kubwa
zitatozwa kwenye mabasi hayo na kufanya wananchi kushindwa kumudu.
Tunakubaliana na hoja kuwa gharama za uendeshaji wa mabasi hayo ni kubwa,
lakini tukumbuke kuwa hii ni huduma kwa wananchi. Serikali inakusanya kodi
kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na wananchi hao, ndio maana
tunaomba serikali, Sumatra -CCC na UDA-RT wakae na kupanga bei zitakazosaidia
wananchi kumudu gharama zake ili lengo la kuboresha usafiri wa wakazi wa jiji
la Dar es Salaam litimie
0 comments:
Post a Comment