Tume ya Taifa ya uchaguzi imeamua kuwa viti vitatu(3) vya wabunge wanawake wa Viti Maalum vilivyobaki uteuzi wake utafanyika mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi katika jimbo la Kijitoupele Zanzibar.
Kikao cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kilichokutana Januari 14 na 15, 2016 kimefikia uamuzi huo kwa sababu ya kuahirishwa uchaguzi katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa mgawanyo wa viti Maalum uliofanywa na Tume, kuna jumla ya viti maalum 113 ambavyo ni asilimia 40 ya wabunge wote 281 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo CCM ilipata viti 64, Chadema viti 36 na CUF viti 10.
Katika Mgawanyo huo, vimebaki viti vitatu kukamilisha idadi ya viti 113 ambavyo havikugawanywa kutokana na kutokukamilika kwa Uchaguzi katika majimbo nane ya Ulanga Mashariki, Arusha Mjini, Handeni Mjini, Ludewa, masasi Mjini, Lushoto, Lulindi na Kijitoupele.
Tayari chaguzi zimeshafanyika katika majimbo hayo saba na jimbo la Kijitoupele kubaki hali iliyosababisha kikao cha Tume kuamua kuwa uteuzi wa viti hivyo vitatu ufanyike mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi katika jimbo la Kijitoupele.
Kwa mujibu wa Ibara ya 78 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, ili chama cha siasa kilichoshiriki katika Uchaguzi Mkuu kiweze kupata Viti Maalum ni lazima kiwe kimepata angalau asilimia tano (5) ya kura zote halali za Wabunge.
Aidha, ili kuweza kukamilisha zoezi hili ni wazi kuwa, Uchaguzi ni lazima ukamilike katika majimbo yote. Kwa kuwa uchaguzi haujafanyika katika jimbo la Kijitoupele, Tume haitoweza kugawa viti vilivyobaki. Hii ni kutokana na ukweli kwamba endapo uteuzi utafanyika, kura za Kijitoupele hazitatumikja katika kupata viti Maalum vilivyobaki jambo ambalo litakuwa ni kinyume na matakwa ya Katiba.
Kwa mantiki hiyo viti hivyo vitatu (3) vitagawanywa mara baada ya uchaguzi kufanyika katika jimbo la Kijitoupele.
Wakati huo huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakusudia kutoa mashine za kuandikishia wapiga kura (BVR) 5000 kwa Taasisi ya NIDA na 1000 kwa Taasisi ya RITA ili ziweze kufanya kazi za uandikishaji wa Vitambulisho vya Taifa na usajili wa vizazi na vifo.
Katika kipindi cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo wa ‘Biometric Voters Registration’ (BVR) Tume ilitumia mashine 8000 kukamilisha zoezi hilo kwa kipindi cha miezi miwili.
0 comments:
Post a Comment