RAIS wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amefuta
rasmi hati ya umiliki wa mashamba makubwa matano yaliyokuwa na hati za miaka 99
yaliyopo Mkoani Tanga yaliyokuwa yamemilikishwa kwa watu waliokuwa wakilima
kilimo cha zao la mkonge.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa ardhi nyumba na
maendeleo ya makazi William Lukuvi katika ziara yake aliyofanya Mkoani Tanga
ambapo aMEsema Rais Magufuli alitoa tamko la kufutwa kwa umiliki wa mashamba
hayo mnamo tarehe 19 mwezi 12 2015.
Waziri Lukuvi ameyataja mashamba hayo kuwa ni
Kikugwi, Sagulasi Estate, Lewa Estate, Bwembwera, pamoja na Azimio yote
yaliyopo katika wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.
Waziri Lukuvi alisema sababu zilizopelekea Rais
Magufuli kutengua hati za umiliki wa mashamba ni pamoja na wawekezaji wa
mashamba hayo kuyatelekeza na kupelekea wananchi wa maeneo hayo na maeneo
jirani kukosa maeneo ya kufanyia shughuli za kilimo.
Waziri huyo amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mwantumu
Mahiza afanye ukaguzi wa mashamba hayo ili ajue mipaka rasmi na kutambua mali
zilizopo ndani ya mashamba hayo pamoja na kupeleka mapendekezo ya kuandaa
mpango kazi wa matumizi bora ya mashamba hayo.
Waziri Lukuvi amesema wizara yake itadhibiti wimbi
la watu wasiotaka kufanya kazi kihalali na badala yake kuwalangua wanunuzi wa
viwanja na kuahidi kuwa ifikapo mwezi wa 7 atapunguza kodi ya ardhi ili kila
mwananchi aweze kuhimili ujenzi wa nyumba na umiliki wa ardhi kihalali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mwantumu
Mahiza ameahidi kuyafanyia kazi maagizo aliyopewa na Waziri Lukuvi ili
kuhakikisha wananchi wanafaidika na ardhi yao pamoja na kupunguza wimbi la
migogoro ya ardhi inayojitokeza siku hadi siku.
0 comments:
Post a Comment