Katika kutekeleza agizo la serikali la kutoa elimu bure
nchini Mkoa wa Dodoma umepokea zaidi ya Sh. 584 milioni kwa ajili ya Elimu bure
kwa shule za Sekondari na Msingi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Chiku
Gallawa kwenye kikao cha kazi cha watendaji wa sekta ya elimu ngazi ya
halmashauri na Mkoa.
Gallawa amesema Mkoa huo umepokea sh. 244,089,000
kwa ajili ya shule za Msingi huku ruzuku ya uendeshaji ikiwa ni sh. 214,264,000
na sh.29,825,000 kwa ajili ya chakula.
Amesema pia Mkoa huo umepokea sh. 340,235,000 kwa
ajili ya shule za Sekondari ikiwa ni kwa ajili ya chakula huku sh. 143,116,000
zikiwa ni kwa ajili ya fidia ya ada ya bweni.
Amesema pia wamepokea sh. 85,755,000 kwa ajili ya
fidia za shule ya kutwa na sh. 88,888,000 kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji,
hivyo kupokea jumla ya sh.584,324,000 kwa ajili ya shule za Msingi na
Sekondari.
Mkuu huyo amesema Mkoa huo unakabiliwa na changamoto
ya kufanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba pamoja na kidato cha nne
hivyo kuwataka wanaohusika kuiondoa aibu hiyo.
Amesema kuwa katika matokeo ya darasa la saba mkoa
huo ulishika nafasi ya 24 kati ya mikoa 25 na katika matokeo ya kidato cha nne
ulishika nafasi ya 19 kati ya Mikoa 25,hizi ni nafasi mbaya hazikubaliki huu ni
mkoa ambapo makao makuu ya Serikali na bunge tuoneane aibu.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Juma
Kaponda akitoa mada iliyohusu wajibu wa Watendaji kwa mwaka 2016 katika mkutano
huo amesema,watendaji wa elimu wanatakiwa kufikiri, kupanga na kutekeleza ili
kuinua taaluma katika mkoa wa Dodoma.
Kaponda amewataka watendaji hao kusimamia
utekelezaji wa elimu, bure na kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayekiuka
maagizo hayo.
0 comments:
Post a Comment