Serikali imekiri kuwa ilifanya makosa kutoa
leseni namba tatu ya uchimbaji wa madini kwa Shanta Mining Tanzania Limited
inayochimba dhahabu katika kijiji cha Saza, Chunya mkoani Mbeya.
Kukiri huko kumetokana na baada ya kuwepo kwa
mgogoro kati ya wakazi wa kijiji cha Saza na mwekezaji huyo ambaye alipewa
leseni ya tatu kwa ajili ya kuendelea na uchimbaji.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo,alisema mwekezaji huyo hakuwa na kosa la kuvamia eneo hilo kwa kuwa
alipewa kisheria ila uzembe ulitokea kwa serikali kupitia kwa maofisa wake
wanaohusika na utoaji wa leseni.
Prof. Muhongo alisema kutokana na uzembe huo,
amemwagiza Kamishna Msaidizi wa Madini nchini, John Nayopa, kwa
kushirikiana na maafisa wa madini wa kanda, wilaya na mwekezaji kupitia upya
mipaka na kurejesha eneo namba 518 kwa wananchi ili kumaliza mgogoro huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shanta
Mining Limited, Toby Bradbury, alisema baada ya kukabidhiwa leseni ya
tatu, aliomba kufanya mkutano na wananchi lakini walidai kuwa kijijini
hapajatulia na kuwa wanaingia kwenye kipindi cha uchaguzi.
Alisema baada ya hapo aliamua kwenda kuwaeleza
wananchi wa kijiji cha Mbangala ambao walielimwishwa juu ya upatikanaji wa
leseni hiyo na walielewa bila kuwapo mgogoro kama wa kijiji cha Saza na
kwamba tangu waanze shughuli hiyo, hawajawahi kugombana na wanakijiji wa
Mbangala.
Alisema kampuni yake inachotaka ni uhusiano mzuri na
wananchi, hivyo hata baada ya kurudisha kibali cha utafiti na kupewa cha
uchimbaji, walimweleza Ofisa Madini wa Wilaya ya Chunya na walimwomba
afanye mkutano na wanakijiji wa Saza lakini wananchi wakakaidi.
0 comments:
Post a Comment