Tahadhari ya kunyesha kwa mvua kubwa katika mikoa
kadhaa nchini kuanzia mwezi huu imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini
(TMA).
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa zitanyesha mvua
katika maeneo mbali mbali nchini huku mikoa ya
Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro na Zanzibar ikitarajiwa kuwa na vipindi
vifupi vya mvua kubwa kati ya Januari na Februari.
Taarifa ya TMA iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mkuu
wake, Dk. Agnes Kijazi, ilisema kuwa maeneo yanayopata misimu
miwili ya mvua, Ukanda wa Ziwa Victoria
hususani maeneo yaliyopo mashariki mwa Ziwa Victoria mikoa ya Mara,
Simiyu na Mwanza) na Nyanda za juu Kaskazini Mashariki
yenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro
yanatarajiwa kupata vipindi vya mvua katika miezi
hiyo.
Mamlaka hiyo inaeleza kuwa maeneo yaliyopo
maghariki mwa ziwa Victoria yenye mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga na
yale ya kaskazini mwa mkoa wa Kigoma yanatarajiwa kupata mvua
ya kawaida.
Taarifa hiyo ilisema yapo maeneo ambayo yatapata
mvua kubwa na kuwataka wananchi wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari na
kuendelea kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na Mamlaka hiyo.
Aidha, TMA imesema kuwa hali ya joto inaonyesha kuwa
joto limeendelea kuongezeka katika Bahari ya Pasifiki kama kiashiria cha
kuimarika kwa El-Niño sambamba na kuongezeka kwa joto katika Bahari ya Hindi
kama iliyotarajiwa na kuelezwa katika taarifa ya utabiri wa mvua.
Kuwapo taarifa kuwa baadhi ya maeneo yatapata mvua
kubwa hazinabudi kuwa changamoto kwa mamlaka mbalimbali za serikali na watu
binafsi kwa kuwa kuna uwezekano wa kutokea athari mbalimbali. Mvua kubwa
zimekuwa zikisababisha mafuriko na nyingine kuambatana na upepo ambao huezua
nyumba na kuharibu mazao.
Athari za mafuriko mara nyingi zimekuwa zikiwakumba
na kuwaathiri wakazi wanaoishi katika maeneo hatarishi, yakiwamo ya mabondemi
na kulazimika kuhitaji misaada ikiwamo ya malazi, chakula, dawa na nyingine za
kibinadamu.
Kutokana na athari hizo hususani za mafuriko
kuyakumba maeneo ya mabondeni kila mwaka, serikali ya Awamu ya Tano
imeshaanzisha operesheni ya kuzibomoa nyumba zote za wananchi waliojenga katika
maeneo yasiyoruhusiwa yakiwamo ya mabondeni nchi nzima.
Ingawa kuna baadhi ya watu wanaokaidi agizo la
serikali la kuwataka waondoke maeneo hayo, lakini taarifa ya TMA inayotabiri
kuwa maeneo kadhaa yatakumbwa na mvua kubwa zinapaswa kupewa umuhimu na
kuchukuliwa hatua za tahadhari haraka kuanzia sasa dhidi ya madhara yanayoweza
kutokea.
Moja ya hatua hizo ni wananchi waliojenga maeneo
hatarishi kukubali kuondoka kwa hiyari yao na kuhamia maeneo mengine, lakini
pia na mamlaka za serikali hususan halmashauri kuboresha miundombimu ya
barabara, madaraja, mifereji ya maji ili mvua hizo zikinyesha zisilete athari.
Hatua hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa kuwa kuwapo kwa
taarifa kuwa hali ya joto inaonyesha kuwa joto limeendelea kuongezeka katika
Bahari ya Pasifiki kama kiashiria cha kuimarika kwa El-Niño sambamba na
kuongezeka kwa joto katika Bahari ya Hindi, ni dalili kuwa mvua za El-Nino
zinaweza kuyakumba baadhi ya maeneo nchini na kuleta maafa.
Dalili za kutokea kwa athari katika maeneo ya nchi
kuanzia sasa hadi kuanza kwa mvua za masika zimeshaanza kuonekana kwa kuwa
tayari kuna maeneo kama ya Mkoa wa Manyara ambayo imenyesha mvua kubwa na
kuharibu miundombinu husani barabara na madaraja.
0 comments:
Post a Comment