Waziri wa nchi, ofisi ya rais -tawala za mikoa na
serikali za mitaa, Tamisem Mh. George Simbachawene amewasimamisha kazi
wakurugenzi watendaji wa manispaa za Kigoma, mkoa wa Kigoma na manispaa ya
Mpanda, mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kuridhia na kutekeleza maamuzi ambayo
yamesababishia serikali hasara na upotevu wa fedha.
Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Mhandisi Boniface
Nyambele anakabiliwa na tuhuma ya uuzaji wa nyumba za halmashauri bila kufuata
sheria, kanuni na taratibu zilizopo na bila kibali cha waziri mwenye dhamana
kama sheria inavyo elekeza.
Mkurugenzi wa manispaa ya Mpanda ndugu Suleiman
Lukanga ana kabiliwa na tuhuma za ununuzi hewa wa gari la kusomba taka kwa
kiasi cha shilingi milioni tisini na mbili na laki saba na elfu hamsini
(92,750,000/=) na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya
Kakese kiasi cha shilingi milioni mia mbili, tisini na nne (294,000,000/=).
Aidha, Mheshimiwa waziri wa nchi ameagiza nafasi ya
mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma ikaimiwe na Mhandisi Sultan Imari Ndilowa
ambaye ni mkuu wa idara ya maji, manispaa ya Kigoma, nafasi ya mkurugenzi wa
manispaa ya Mpanda ikaimiwe na ndugu Lauteri John Kanoni ambaye ni katibu
tawala msaidizi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa waziri wa nchi, amewataka
wakurugenzi watendaji wa mamlaka za serikali za mitaa kote nchini kuwa
makini katika kutekeleza majukumu yao wafuate sheria, kanuni na taratibu
zilizopo.
Serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa
watumishi wote ambao watakiuka matakwa ya sheria, kanuni na taratibu na
kutoweka mbele maslahi ya umma.
0 comments:
Post a Comment