YANGA jana ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
Ndanda katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es
Salaam na kukalia kilele cha msimamo wa ligi hiyo.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 36
sawa na Azam na kuishusha kileleni timu hiyo kwa uwiano mzuri wa mabao.
Haikuwa kazi rahisi kwa Yanga kupata bao hilo katika
mechi ya jana baada ya wachezaji wa Ndanda kuonekana kujitutumua hasa katika
kipindi cha kwanza ambapo walionekana kucheza soka ya kuzuia zaidi.
Mfungaji wa Yanga jana alikuwa beki Kelvin Yondani
aliyefunga kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 62.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya Deus
Kaseke kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari na mchezaji wa Ndanda.
Ilikuwa penalti ya pili baada ya Amis Tambwe kukosa
penalti katika dakika ya 49 iliyotolewa na mwamuzi baada ya Simon Msuva
kuangushwa eneo la hatari na Paul Ngalema.
Penalti hiyo ya Tambwe iligonga mwamba kabla ya
kuokolewa na kipa wa Ndanda, Jeremia Kisubi. Katika mechi ya jana, Yanga
ingeweza kupata bao la mapema zaidi kama washambuliaji wake wangekuwa makini
kwani katika dakika ya tatu ya mchezo nusura Donald Ngoma aandike bao lakini
mpira uliwahiwa na mabeki wa Ndanda na kuuondosha eneo la hatari.
Juma Abdul nusura apate bao katika dakika ya 29,
lakini mpira wa adhabu aliopiga uliokolewa na kipa wa Ndanda.
Kwa upande wa Ndanda, mchezaji Atupele Green alikuwa
kwenye nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 38 lakini shuti lake lilikuwa dhaifu.
Dakika mbili baadae Paul Ngalema alikosa bao lingine
la wazi.
Yanga: Deogratius Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua,
Vicent Bossou, Kelvin Yondani, Salum Telela, Simon Msuva, Thamani Kamusoko,
Donald Ngoma, Amisi Tambwe/Malimi Busungu, Deus Kaseke/ Issoufour Abubacar.
Ndanda: Jeremia Kisubi, Azizi Sibo, Paul Ngalema,
Kassian Ponera, Salvatory Ntebe, Jackson Nkwera/ Omega Seme, William Lucian,
Hemed Khoja, Atupele Green, Kigi Makasi/ Masoud Ally, Braison Raphael.
0 comments:
Post a Comment