TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kwamba
haianzishi na haijaanzisha Jimbo jipya la Uchaguzi baada ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25, mwaka huu, huku ikisisitiza kuwa Jimbo la Kijitoupele mjini Unguja
litafanya uchaguzi wake ambao uliahirishwa mwaka jana.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema
hayo jana katika taarifa yake kwa umma kuhusu habari iliyoandikwa na gazeti la
kila wiki la MwanaHALISI juzi yenye kichwa cha habari “NEC yaibua mapya.”
Kailima alisema hata kabla Tume ya Uchaguzi
Zanzibar, haijafuta matokeo wa Zanzibar, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
ilikuwa imeshatangaza kuahirisha uchaguzi katika majimbo manane, likiwemo la
Kijitoupele kwa sababu za vifo vya wagombea na hitilafu mbalimbali.
“Jimbo la Kijitoupele la Zanzibar ni miongoni mwa
majimbo nane (8) ambayo yaliahirishwa kufanya uchaguzi wa Wabunge tarehe 25
Oktoba, 2015, ambapo majimbo sita (6) ambayo ni Lushoto, Ulanga Mashariki,
Masasi Mjini, Ludewa, Handeni Mjini na Arusha Mjini yaliahirishwa kutokana na
vifo vya wagombea na majimbo mawili (2) ya Kijitoupele - Zanzibar na Jimbo la
Lulindi – Masasi yaliahirishwa kutokana na hitilafu mbalimbali,” alieleza
Kailima.
Kuhusu hoja nyingine iliyotolewa na gazeti hilo
kuhusu uteuzi wa wabunge wa Viti Maalumu, Kailima alisema ifahamike kwamba
katika maamuzi yake kuhusu Viti Maalumu, Tume imezingatia matakwa ya Ibara ya
78 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Alisema Katiba hiyo inaeleza kuwa ili chama
kilichoshiriki Uchaguzi Mkuu, kipate Viti Maalumu ni lazima kiwe kimepata
angalau asilimia tano ya kura zote halali za ubunge. “Hivyo, Viti Maalumu
vilivyobaki haviwezi kugawanywa hadi hapo Jimbo la Kijitoupele litakapofanya
uchaguzi katika tarehe ambayo itatangazwa na Tume hapo baadaye,” alifafanua
Kailima.
“Kwa kuwa Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI
alikusudia kuupotosha umma kwa sababu anazozifahamu yeye mwenyewe kwa kutoa
taarifa zisizo sahihi, za uongo na uchochezi Tume ya Taifa ya Uchaguzi inamtaka
Mhariri wa MwanaHALISI kuiomba radhi Tume ya Taifa ya Uchaguzi ukurasa wa mbele
wa toleo lijao kama alivyofanya katika toleo hilo. Kama wasipofanya hivyo Tume
ya Taifa ya Uchaguzi italichukulia Gazeti la MwanaHALISI hatua za kisheria,”
alibainisha Kailima.
0 comments:
Post a Comment