Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu
vikali kushambuliwa kwa ubalozi wa Saudi Arabia nchini Iran na waandamanaji
waliokasirishwa na kuuawa kwa mhubiri wa Kishia.
Taarifa ya baraza hilo haijazungumzia kutekelezwa
kwa hukumu ya kifo dhidi ya mhubiri huyo maarufu, Sheikh Nimr al-Nimr.
Saudi Arabia ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na
Iran Jumapili baada ya ubalozi wake kuvamiwa na kuchomwa moto.
Jumatatu, naibu waziri mkuu wa Uturuki Numan
Kurtulmus alihimiza nchi hizo mbili kutuliza mgogoro huo, ikisema eneo la
Mashariki ya Kati tayari limo hatarini ya kulipuka.
Baraza la Usalama la UN, likijibu barua kutoka kwa
Saudi Arabia, limeshutumu shambulio hilo la katika ubalozi Tehran pamoja na
shambulio katika afisi ya ubalozi wa Saudia Arabia katika jiji jingine la Iran
la Mashhad.
Baraza hilo limeitaka Iran kulinda mabalozi na mali
ya ubalozi pamoja na wafanyakazi wake “kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa”.
Limetoa wito kwa pande zote mbili “kushauriana na
kuchukua hatua za kupunguza wasiwasi katika kanda hiyo”.
Hata hivyo, baraza hilo halijazungumzia hatua ya
Saudi Arabia kumuua Sheikh Nimr al-Nimr, mhubiri wa madhehebu ya Shia,
aliyeuawa Jumamosi pamoja na watu wengine 46 baada ya kutuhumiwa kutekeleza
makosa yanayohusiana na ugaidi.
Akizungumza New York, balozi wa Saudi Arabia katika
UN Abdallah al-Mouallimi amesema mzozo wa sasa ungeepukika iwapo Iran
ingejiacha “kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, ikiwemo Saudi Arabia”.
Awali, Saudi Arabia imewahi kuituhumu Iran kwa
kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu.
Saudi Arabia na Iran ndizo nchi kuu za Kisuni na
Kishia mtawalia eneo la Mashariki ya Kati na zimekuwa wapinzani wakuu.
Nchi hizo huunga mkono pande pinzani katika mizozo
Syria na Yemen.
Bw Mouallimi amesema juhudi za kutafuta Amani katika
mataifa hayo hazifai kuathiriwa na mzozo wa sasa.
Kufuatia mashambulio hayo, nchi kadha washirika wa
Saudi Arabia zimekatiza uhusiano na Iran zikiwemo Bahrain na Sudan na Jumuiya
ya Milki za Kiarabu (UAE) ambayo imepunguza hadhi ya ujumbe wa kibalozi wa
Iran.
Somalia pia imesema inaunga mkono hatua ya Saudi
Arabia kuvunja uhusiano na Iran.
0 comments:
Post a Comment