Mkurugenzi wa kampuni ya Victoria Media Services Ltd
ambaye pia ndiye Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mawio,Simon Martha Mkina,
amelaani vikali kitendo cha serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John
Magufuli kuanza kuminya uhuru wa vyombo vya habari na kujaribu kuzima sauti za
wanyonge hapa nchini.
“Serikali lazima iwe na uvumilivu wa kusikia na hata
kuona isiyoyapenda, ilimradi ni kilio cha wananchi wake,MAWIO limekuwa gazeti
pekee linalobeba kilio hicho, ni njia ya wasiokuwa na sauti kusikika. Sasa
wamezibwa midomo-wakasemee wapi? Ni ubabe.” Inaeleza sehemu ya taarifa ya Mkina
aliyoitoa kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Taarifa iliyochapishwa kupitia Mwanahalisi Online
Inasemaa.
BAADA ya kulisakama kwa muda mrefu hatimaye Serikali
kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nauye,
imelifungia kwa muda wote gazeti la kila wiki la MAWIO linalochapishwa na
kampuni ya Victoria Media Services Ltd. Anaandika Charles William …
(endelea).
Katika tangazo lake lililotolewa kupitia gazeti la
Serikali notisi namba 55 ya Januari 15, 2016 Serikali imebainisha kuwa
imechukua uamuzi huo wa kulifungia gazeti la Mawio kwa muda wote kwa mujibu wa
mamlaka iliyonayo kupitia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 kifungu
cha 25(1).
“Mawio linatakiwa kusimamisha uchapishaji wake kwa
kipindi chote ikiwemo pia katika vyombo vya mawasiliano vya kielektroniki
kuanzia Januari 15, 2016”, ilisema sehemu ya tangazo hilo ambalo limetolewa
katika gazeti la serikali, likisainiwa na waziri Nape Nauye.
Tangazo hilo halikuweza kufafanua zaidi ni makosa
gani hasa yaliyosababisha gazeti kufungwa na kwanini adhabu iliyotolewa ni
kubwa sana ukizingatia kuwa Mawio halikuwahi kufungiwa wala kuonywa kwa kosa
lolote katika siku za wa awali zaidi ya kupokea vitisho kutoka kwa serikali
mwanzoni mwa mwezi Januari 2016.
Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa
kwa uongozi wa gazeti hilo kupitia Mkurugenzi na Mhariri Mtendaji wa gazeti
hilo, Simon Mkina juu ya kufungiwa kwake zaidi ya barua ya msajili wa magazeti
iliyoandikwa Januari 6, mwaka huu ikieleza kutoridhishwa na utetezi wa gazeti
hilo juu ya uchapishaji wa makala za uchochezi na kuahidi kuchukua hatua.
Serikali ilianza kulikabili rasmi gazeti la Mawio 31
Desemba, 2015 kwa barua iliyoandikwa na msajili wa magazeti ikimtaka mhariri wa
gazeti hilo kutoa maelezo ya kwanini gazeti hilo lisifungiwe kufuatia makala
zake mbili zenye vichwa vya habari “Hosea kortini” na “Seif Rais Zanzibar”
ambazo zilidaiwa kuzua taharuki.
“Nakujulisha kwamba ofisi ya msajili wa magazeti
haijaridhika na utetezi wako kwa kuwa hujatoa uthibitisho usio na shaka juu ya
madai ya makala ulizochapisha,” ilitamka sehemu ya barua iliyosainiwa na Raphael
Hokororo, kwa niaba ya msajili.
Gazeti la Mawio ambalo huandika habari za kiuchunguzi
limekuwa likifichua kashfa mbalimbali za ufisadi, uvunjifu wa haki za binadamu
na rushwa limefuata mkondo uleule ambao gazeti la MwanaHALISI liliufuata 30
Julai 2012 pale lilipofungiwa kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuchapisha
taarifa za uchochezi.
MwanaHALISI lilikaa kifungoni kwa zaidi ya miaka
mitatu kabla ya kurejeshwa kwa amri ya Mahakama Kuu mwezi Agosti, 2015 kufuatia
Mkurugenzi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea kufungua kesi,
akipinga kufungiwa kwa gazeti hilo.
Mpango wa kulifungia gazeti hilo ulitajwa kubainika
mapema kufuatia kurejeshwa kwa gazeti la MwanaHALISI mnamo mwezi Agosti, 2015
na hivyo serikali kupitia msajili wa magazeti kutokuwa tayari kuvumilia
machapisho ya habari na makala za kiuchunguzi kila wiki kutoka katika magazeti
hayo na hivyo kutafuta namna ya kulifungia mojawapo.>>>http://mwanahalisionline.com/
0 comments:
Post a Comment