Hatimaye aliyekuwa waziri wa fedha, Basil Mramba na
aliyekuwa waziri wa nishati na madini Daniel Yona, wamepewa adhabu ya kifungo
cha nje, ambapo watakuwa wanafanya shughuli za kijamii katika hospitali ya
Palestina Sinza, Dar es Salaam ikiwemo usafi wa mazingira.
Vigogo hao wa serikali walikuwa wanatuhumiwa
kuisababishia serikali hasara ya sh. Bilioni 11.7, baada Mramba kutoa msamaha
wa kodi kwa kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza ya ukaguzi wa madini ya
dhahabu bila kupata ushauri kutoka TRA.
Mchakato huo wa vigogo hao wa serikali kupata
kifungo cha nje, ulitokana na magereza kuandika barua katika mahakama ya hakimu
mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambayo ilikuwa na orodha ya majina likiwemo la
Mramba na Yona.
Barua hiyo ambayo iliandikwa Desemba 5, mwaka jana
na magereza ilikuwa inaeleza kuwa imeona wafungwa hao wanastahili kufanya kazi
za kijamii nje na gereza.
Magereza waliandika barua hiyo kwa kufuata sheria ya
huduma kwa jamii namba 6 ya mwaka 2002 kifungu cha tatu kinaeleza kuwa mtu
yeyote anapokuwa ametiwa hatiani kifungo kisichozidi miaka mitatu na faini kina
ruhusu mfungwa kupewa adhabu ya kifungo cha nje.
Baada ya hakimu mkuu mfawidhi wa mahakama hiyo,
Cyprian Mkeha kupata barua hiyo alitoa amri kwa maofisa wa ustawi wa jamii
kwenda gerezani kuchunguza kama kweli walichokidai magereza ni cha kweli.
Vigogo hao watatakiwa kufika katika hospitali hiyo
saa moja asubuhi kuanzia jumatatu hadi ijumaa, ambapo watatakiwa kufanya
shughuli hizo kwa saa nne kila siku.
Kama magereza wasingewaona Mramba na Yona kuwa
wanaweza kutumikia adhabu ya kifungo cha nje walitakiwa kumaliza kifungo chao
cha miaka miwili jela Novemba 5, mwaka huu.
Julai 6, mwaka jana, mahakama ya Kisutu iliwahukumu
kwenda jela miaka mitatu Mramba na Yona baada ya kuwatia hatiani
kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali
hasara ya sh bilioni 11.7.
0 comments:
Post a Comment