Balozi wa Tanzania nchini India John Kijazi amesema
ameridhika kwamba serikali ya nchi hiyo imeweka mikakati ya kutosha kuwalinda
wanafunzi, kufuatia kisa ambapo wanafunzi wanne walishambuliwa mjini Bangalore
Jumapili.
Akizungumza baada ya kutembelea pahala ambapo
wanafunzi hao walishambuliwa, na mmoja wao kuvuliwa nguo, Bw Kijazi amesema
huenda kisa hicho kilitokana na suitafahamu.
“Kilicho muhimu ni tuangalie siku za usoni kwa
sababu tusipofanya hivyo tutapotea. Tunahitaji kutatua tatizo la sasa lakini
pia tuangalie mikakati ya muda mrefu,” ameambia wanahabari.
“Nimeridhishwa na hatua za kiusalama ambazo
zimechukuliwa na serikali hapa. Kuna maafisa ambao wamesimamishwa kazi.”
Balozi huyo alikata kutaja kisa hicho kama cha
ubaguzi wa rangi.
“Hatukutaka kuangazia masuala ya ubaguzi wa rangi na
mambo mengine kwa sababu nadhani vyombo vya habari vinapendezwa sana na hilo.
Tumejadiliana kuhusu masuala halisi na hatua madhubuti ambazo tayari
zimechukuliwa na serikali ya hapa,” amesema.
Bw Kijazi alisafiri hadi Bangalore akiandamana na
maafisa wawili wa wizara ya mambo ya nje ya India ambapo walikutana na waziri
wa mambo ya ndani wa jimbo la Karnataka Dkt G Parameshwara na wakuu wa polisi
wa jimbo hilo.
Polisi mjini Bangalore wamewakamata watu tisa
kuhusiana na kisa hicho.
Mkuu wa kituo cha polisi cha Soldevenahalli pia
amesimamishwa kazi kwa tuhuma kwamba hakuchunguza kwa undani kisa hicho baada
ya mmoja wa wanafunzi hao kupiga ripoti.
Konstebo wa polisi pia amesimamishwa kazi kwa
kutochukua hatua kuzuia wanafunzi hao wasishambuliwe na umati.
0 comments:
Post a Comment