Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
amesema kuwa Mameneja wa Shirika la umeme nchini TANESCO wanaosimamia Kanda
mbalimbali nchini wataondolewa katika vyeo hivyo iwapo hawatatimiza maagizo
mbalimbali waliyopangiwa na Wizara ya Nishati na Madini ifikapo machi moja
mwaka huu.
Profesa Muhongo amesema hayo wakati wa kikao chake
na watendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na Taasisi nyingine zilizo
chini ya Wizara ya Nishati na Madini kilichofanyika katika Kituo cha kuzalishia
umeme cha Mtera.
Katika kikao hicho Prof. Muhongo amesema atawaondoa
katika nafasi zao Mameneja wa Tanesco watakaoshindwa kuunganisha huduma kwa
wateja wengi, kuwa na makusanyo makubwa ya bili za umeme, kupunguza
manung’uniko ya wananchi katika huduma za umeme na uboreshaji wa mawasiliano
kati ya Shirika hilo na wananchi
Mbali na hilo amewataka mameneja hao kutumia vyombo
vya habari kuelemisha wananchi juu ya masuala ya umeme.
Aidha, Waziri wa Nishati na Madini amekitaka Kitengo
cha Uwekezaji cha Tanesco kama hakitakuwa na miradi mipya ya umeme ifikapo
tarehe 2 Aprili mwaka huu, watendaji katika Ofisi hiyo wataondolewa katika
nafasi hiyo kwa kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Vilevile Profesa Muhongo amewaagiza watendaji wa
TANESCO katika vitengo vya ukaguzi kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa ikiwemo
usimamizi madhubuti wa nguzo za umeme ambazo baadhi huanguka kila inapofika
msimu wa mvua na kusema kuwa suala hilo halikubaliki.
0 comments:
Post a Comment