RAIS John Magufuli amepiga marufuku uingizwaji wa
sukari kutoka nje ya nchi bila idhini ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuvilinda
viwanda vya kuzalisha bidhaa hiyo nchini.
Kutokana na hatua hiyo, viwanda vya ndani ya nchi
sasa vitatakiwa kuboresha huduma zake na kuongeza uzalishaji, kwa kuwa vitakuwa
na uhakika wa soko hapa nchini, lakini pia vitatoa ajira kwa Watanzania na
kuongeza mapato kwa Serikali.
Katika kuhakikisha viwanda hivyo vinapata uhakika
huo wa soko, pamoja na agizo la Rais, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa mkoani
Tanga, alimuagiza Mkuu wa Mkoa huo, Mwantumu Mahiza, akutane na Mamlaka ya
Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Jeshi la Polisi, watafute mbinu za
kudhibiti njia za panya zinazotumika kupitisha sukari ya magendo.
Majaliwa alieleza kuwa ana taarifa za uwepo majahazi
yanayoleta sukari kutoka Brazil na kuagiza bandari zote ndogo ndogo hadi
Pangani zidhibitiwe. Sisi pamoja na kumpongeza Majaliwa kwa uamuzi huo,
tunamuomba awe mkali kwa watendaji wa mikoa yote nchini yenye bandari ndogo zinazotumika
kupitisha magendo ya sukari.
Ingawa tunaambiwa TRA na Polisi hufanya doria
kukamata sukari hizo za magendo, sisi tunaona bado kasi yao ni ndogo na
kunahitajika kuongezwa nguvu kwa upande wa boti, magari na hata maofisa.
Pia usimamizi kwa maofisa hawa wa doria na ukamataji
unahitaji kuboreshwa, mfano kwa Dar es Salaam kwenye bandari bubu eneo la
Mbweni kuna taarifa kuwa bidhaa za magendo na hasa sukari zimekuwa zikiingizwa
kiurahisi.
Taarifa zinaeleza kuwa majahazi hushusha mizigo
usiku na kuingizwa kwenye magari ambayo huegeshwa kwenye makazi ya watu, kisha
sukari na bidhaa nyingine hupakuliwa na kuhifadhiwa kwenye nyumba
zisizomalizika halafu bodaboda maalumu hupakia magunia ya sukari na kuyapeleka
kwenye maeneo wanapoelekezwa hasa Tegeta.
Bodaboda zile zimekuwa zikipishana na mamlaka
mbalimbali barabarani, hazikamatwi wala kuhojiwa kiasi kwamba hali hiyo imekuwa
ni kama mazoea, watu asubuhi wanapokwenda kazini wanapishana nazo tena zinatia
mbwembwe zinapokuwa barabarani.
Tumeona matukio machache sana ya kukamatwa kwa
shehena hizo za sukari za magendo kutoka nje kama hivi karibuni mkoani Lindi,
ambako kulikamatwa mashua ikiwa na sukari mifuko 3,725 yenye thamani ya Sh
milioni 127 iliyoingizwa nchini kutokea Brazil.
Vilevile sukari hizo haziuzwi kwa kificho, zimejaa
kwenye maduka na wahusika wanaziona kama si kuwa miongoni mwa wateja, lakini
tunashangaa inakuwaje kuwa na ugumu kwenye kudhibiti.
Sasa Serikali imedhamiria kukomesha uingizwaji huu
wa sukari kutoka nje ili viwanda vyetu viongeze uzalishaji, hivyo ni vema pia
wauzaji wakamatwe na kutozwa faini na ikibidi wasaidie kutaja wanapozitoa
sukari hizo.
Sukari hii ya nje kwanza inaingia sokoni na kutumiwa
na watu bila kujulikana ubora wake na hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS) au
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawawezi kuzikagua sukari hizo.
Wakati yote yanafanyika katika kudhibiti sukari hizo
kutoka nje, ni vema wananchi wapewe elimu ya kuwa wazalendo na kupenda sukari
ya Tanzania, ili washhiriki kugomea kununua sukari ya nje na kushiriki kutoa
taarifa pindi wanapoona sukari ya nje inauzwa au kuna sehemu inapitishwa
kuingizwa nchini.
0 comments:
Post a Comment