MOJA ya habari kubwa katika kurasa za mbele za
magazeti ya jana, ilihusiana na tukio la kundi la watu zaidi ya 30 wenye silaha
za jadi kudaiwa kuvamia kituo cha Polisi cha Duthumi, tarafa ya Bwakila
wilayani Morogoro.
Watu hao, wakiwa na mapanga, mashoka na marungu,
walivamia kituo hicho Ijumaa, majira ya saa 12:40 jioni kwa lengo la kuwaokoa
wenzao watatu waliokuwa wanashikiliwa kutokana na tuhuma za wizi wa mifugo,
wakiwemo ng’ombe 11, mbuzi wanne na kondoo mmoja.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa
Morogoro, Graifton Mushi, licha ya kufanikiwa kuvunja mlango, hawakutimiza
lengo lao, kwani watuhumiwa walikuwa wameshahamishiwa sehemu nyingine.
Hata hivyo, tukio hilo halikumalizika kimyakimya,
kwani askari Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi, risasi baridi na za
moto kwa kurusha hewani ili kuwatawanya wahalifu waliokwenda kuwatorosha
wenzao.
Kwa hakika, tukio hili na mengine ya uvamizi wa
vituo vya Polisi, mauaji ya askari wakiwa katika vituo vyao vya kazi na wizi wa
silaha yanaacha maswali mengi. Tunajiuliza, matukio haya yataachwa yaendelee
hadi lini?
Ni kwamba wahuni wana nguvu kubwa za mbinu zaidi
kuwashinda askari wetu waliofundwa kitaalamu katika vyuo vya taaluma ya Polisi
na vingine nchini? Au wana silaha bora kuliko askari wetu?
Matukio ni mengi, lakini tulitarajia tukio kama la
uvamizi, mauaji ya watu saba wakiwemo polisi wanne na uporaji wa silaha katika
kituo cha Polisi Stakishari kilichopo Ukonga, Dar es Salaam katikati ya mwaka
jana lingekuja na majibu ya ulinzi wa uhakika wa vituo vya usalama: Badala yake
watu wanaendelea kujichukulia sheria mkononi na kuthubutu kuvamia vituo hata
Polisi, mathalani hili la juzi huko Morogoro au lile la kuchoma kituo cha
Polisi Bunju pia katikati ya mwaka jana.
Lakini kabla ya hapo, majambazi, wahuni na wahalifu
hawa walishavamia, kukiteka kituo cha Polisi Ikwiriri kilichopo tarafa ya
Ikwiriri, wilayani Rufiji, mkoani Pwani na kuwaua askari wawili, kupora silaha
saba na kisha kulipua bomu kituoni hapo. Walivamia kituo kidogo cha Polisi
Mngeta, Morogoro na kupora SMG moja na magazini moja yenye risasi 30.
Aidha, Juni 11, mwaka jana baada ya watu
wasiojulikana walikivamia kituo kidogo cha Polisi Mkamba mkoani Pwani na
kusababisha kifo cha askari mmoja na mgambo. Pia walipora silaha aina ya Shot
Gun tatu, Sub Mashine Gun (SMG) mbili na magazine 30 kila moja ambazo zilikuwa
kwenye ghala la muda zikisubiri kupelekwa kwenye kituo kikubwa kwenye ghala kuu
la silaha.
Tukio jingine la kuvamiwa kituo cha Polisi lilitokea
Septemba mwaka jana katika kituo kikuu cha Polisi wilayani Bukombe mkoani Geita
ambako askari wawili waliuawa na kujeruhi wengine watatu.
Mlolongo wa matukio ni mrefu, lakini ifike mahali
jamii isiaminishwe kwamba Polisi wameshindwa kudhibiti matukio ya aina hii na
badala yake ije na mikakati itakayokomesha kabisa matukio ya aina hii.
Tunaamini chini ya uongozi imara wa Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu kwa kushirikiana na Waziri mwenye
dhamana katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, majambazi na
wahuni hawa hawataachwa waendelee kutamba.
0 comments:
Post a Comment