WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amesema kuwa wakurugenzi wa
halmashauri nchini, wakaoshindwa kutekeleza agizo la kujitosheleza kwa madawati
katika shule ya msingi na sekondari hadi Juni mwaka huu, wajitambue wameshindwa
kazi.
Pia wakurugenzi wa halmashauri watakaozalisha madeni
ya watumishi pamoja na ya wazabuni wa vyakula katika shule za serikali,
watakuwemo kwenye kundi la kuwajibishwa.
Waziri huyo wa Tamisemi alitoa kauli hiyo juzi
wakati akizungumza na Viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Morogoro wakiwemo wakuu
wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri (Ma-DED), makatibu tawala wa
wilaya, na wakuu wa idara za halmashauri zote za mkoa huo chini ya Mkuu wa
Mkoa, Dk Rajab Rutengwe.
Hivyo alisema agizo lililotolewa na Rais John
Magufuli la kutaka kuona kila mwanafunzi anaketi kwenye madawati, halina
mjadala na kwamba ifikapo Juni mwaka huu pasiwepo na mwanafunzi anaketi
sakafuni na wakurugenzi watakaoshindwa, watakuwa wameshindwa kazi na
watawajibishwa.
Aliagiza wakuu wa mikoa na wilaya, ambao ndiyo
wasimamizi wa rasilimali zilizopo katika maeneo yao hasa ya misitu, wasisite
kutoa vibali vya uvunaji wa miti ya kutengeneza madawati kwenye wilaya zao ili
watoto wote waliopo shuleni wawe wanakaa kwenye madawati.
“Tumieni vyema nafasi zenu za kuwa wenyeviti kamati
za kutoa vibali vya uvunaji rasilimali za misitu... ili madawati yaweze
kupatikana na utekelezaji wa matumizi ya vibali hivyo ufuatiliwe ili visitumiwe
vibaya na waliopewa kazi hizo,” alisema Waziri.
Alitoa mfano kuwa Mkoa wa Morogoro ambao una
rasilimali nyingi za misitu, umekuwa na upungufu wa madawati ni 73,972 katika
shule za msingi na 11,038 katika shule za sekondari za serikali.
Pia alisema mkoa una upungufu wa vyumba vya madarasa
4,508 kwa shule za msingi na madarasa 352 kwa shule za sekondari za serikali
wakati eneo la afya lina upungufu wa zahanati 334.
“Kuna kazi kubwa katika sekta ya elimu ambapo kwa
Mkoa wa Morogoro pekee unakabiliwa idadi ya madawati mengi sembuse wilaya kama
ya Kibaha,” alisema.
Waziri Simbachawene pia alionya tabia ya uzalishaji
wa madeni ya watumishi wa halmashauri na wazabuni, wanaotoa huduma ya vyakula
shule za serikali unaofanywa na watumishi wa Idara ya Uhasibu na maofisa
utumishi kuwa siku zao, zinahesabika na wajiandae kutumbuliwa majipu.
Ili kutekeleza agizo la kukomesha uzalishaji wa
madeni, alitoa maelekezo kwa maandishi kwa wakurugenzi wa halmashauri zote 181
kwa ajili ya utekelezaji wake.
Alisema halmashauri hizo, zina uwezo wa kulipa madai
ya wafanyakazi wake kama nauli ya likizo, gharama za matibabu na mambo mengine
kwa kutumia fedha za makusanyo yake ya ndani kwa kuwa fedha za mishahara na
mengine zinatolewa na Serikali Kuu.
“Serikali inalaumiwa kwa sababu wakurugenzi
hawatekelezi wajibu wao na matatizo mengi yapo katika Idara ya Uhasibu na Idara
ya Utumishi,” alisema na kuongeza: “Wahasibu ni chanzo cha matatizo yote haya
wanakuwa na mahusiano na wenye kutoa huduma, utakuta deni la shilingi bilioni
25 likihakikiwa linabakia shilingi bilioni tano, zimeongezwa tarakimu hapo na
haya yameshatokea.”
Aliongeza, “Hawa sasa wajiandae kutumbuliwa,
tunaelekea ngazi ya wakuu wa idara wa halmashauri, akitumbuliwa mkurugenzi naye
mkuu wa idara anayehusika na kashfa hiyo atawajibishwa si kwa mkurugenzi
pekee.”
Aliwakumbusha wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi
wa halmashauri nchini kutambua jukumu walilopewa la ukamilishaji wa vyumba vya
maabara na wasiokamilisha hicho ni mojawapo ya kigezo cha kupoteza nafasi zao.
0 comments:
Post a Comment