MANISPAA ya Ilala, Dar es Salaam imeanza ukaguzi wa
ndani ili kubaini ufisadi katika mfumo wa ulipaji mishahara ya askari mgambo.
Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa baadhi ya mgambo
hao walikuwa wakilipwa mshahara tofauti na uliokuwa unafahamika wa Sh 280,000
kwa mwezi.
Badala yake baadhi yao walikuwa wakilipwa kati ya Sh
50,000 na 80,000 kama posho badala ya Sh 280,000 zilizokuwa zimeidhinishwa na
manispaa hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana baada ya kukabidhiwa Ilani ya Ukawa pamoja na mwongozo wa kazi, Meya wa
Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, alisema baadhi ya maofisa ambao si
waaminifu walikuwa wakijichotea fedha kupitia mishahara ya mgambo kinyume cha
sheria.
Alisema Manispaa ya Ilala ilikuwa na mgambo 150
ambao walikuwa wakiajiriwa kwa mkataba wa miezi mitatu, lakini watendaji
walikuwa wakitumia mbinu chafu kuwapunja mishahara yao.
“Katika uchunguzi wetu tumebaini mgambo hao baada ya
kumaliza mkataba wa miezi mitatu walikuwa wakipunguzwa na kubaki 100, huku 50
wakiondolewa kwenye ajira, lakini vitabu vya mishahara vilionyesha ni 150.
“Walikuwa wakisimamishwa kazi huku wakiendelea
kuwatumikisha kwa ujanja bila kuwapa malipo yao stahiki, wakati vitabu vya
manispaa vilikuwa vikionyesha wanalipwa mshahara kamili.
“Cha ajabu baada ya ukaguzi wa awali tulibaini
baadhi ya mgambo walikuwa wakisitishiwa mkataba na kutumiwa kwa ujanja kisha
kulipwa Sh 50,000 hadi 80,000 wakati kwenye vitabu vya manispaa vilikuwa
vinaonyesha wamelipwa Sh 280,000 ambazo walikubaliana awali,” alisema Kuyeko.
MABANGO YA BIASHARA
Kuyeko alisema Manispaa ya Ilala imeingia mkataba na
kampuni ambayo imeanza kufuatilia mabango yote yaliyokuwa yanakwepa kulipiwa
ushuru pamoja na kodi kwa ujumla.
Aidha Kuyeko alizungumzia hali mbaya iliyopo katika
miundombinu ya elimu ambapo alisema shule nyingi za Serikali zipo hoi kiasi cha
kukatisha tamaa.
Alizitaja shule za sekondari Azania, Pugu Bangulo,
Pugu Stesheni na Bonyokwa kuwa miundombinu yao imechakaa kiasi cha kutisha na
kuhatarisha maisha ya walimu na wanafunzi.
Akitolea mfano Shule ya Bangulo, alisema darasa la
kwanza lina wanafunzi 305, huku kila moja likiwa na wanafunzi 100, hivyo walimu
wanalazimika kufundisha chini ya miti kutokana na uhaba wa madarasa.
Alisema katika Sekondari ya Azania wameshuhudia vyoo
vikiwa vimefurika maji taka na wanafunzi wanalala chini kutokana na msongamano
kuwa mkubwa.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Kuyeko alisema
wameweka mkakati wa kujenga madarasa matano kila shule.
0 comments:
Post a Comment