Watu wawili wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa baada
ya basi la kampuni ya Ndenjela linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es
Salaam kuligonga kwa nyuma basi dogo aina ya toyota Hiace ambalo ni daladala
linalofanya safari zake kati ya Igawilo na stendi kuu jijini Mbeya katika eneo
la Uyole, kwenye barabara kuu ya Tanzania - Zambia.
Ajali hiyo imetokea majira ya alfajiri wakati basi la
kampuni ya Ndejela likitokea gereji kwenda katika kituo kikuu cha mabasi jijini
Mbeya kwa ajili ya kuchukua abiria ili kuanza safari ya kwenda Dar es Salaam,
lakini lilipofika eneo la Kilimo katika bonde la Uyole, ndipo basi dogo aina ya
toyota Hiace ambalo lilikuwa limesimama kituoni,likaingia ghafla barabarani na
ndipo lilipogongwa na kwa nyuma na basi hilo la Ndenjela ambalo lilikuwa kwenye
mwendo mkali na kusababisha daladala hilo kuacha njia na kugonga jiwe kubwa
kando ya barabara.
Afisa muuguzi msaidizi wa zamu katika hospitali ya rufaa
Mbeya,Abdul Kumwambe amethibitisha kuwepo kwa vifo vya watu wawili pamoja na
majeruhi 13 ambao wanatokana na ajali hiyo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya,Kamishna msaidizi mwandamizi
wa jeshi la polisi,Ahamed Msangi amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo
wa kasi wa basi la kampuni ya Ndenjela huku akidai kuwa uchunguzi zaidi wa
ajali hiyo unaendelea.
0 comments:
Post a Comment