WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa
Maji wa Wilaya ya Chato, Bw. Peter Ngunura kwa kosa la kumdanganya mbele za
watu na kumpa taarifa za uongo juu ya pampu ya maji iliyodaiwa kupelekwa
Morogoro.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Machi
16, 2016) alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Chato waliojitokeza
kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo
wilayani Chato, mkoani Geita.
Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku
mbili akitokea mkoani Kagera, alisimamishwa na wakazi wa kijiji cha Kalebezo,
kata ya Nyamirembe, wilayani Chato na kukuta mabango yaliyokuwa yakidai maji
safi na kuelezea uharibifu wa pampu ya maji.
Katika maelezo yao, wakazi hao walimweleza Waziri Mkuu
kwamba mradi wa maji kwenye kata hiyo ulishakamilika lakini pampu yao
imechukuliwa na kupelekwa Morogoro jambo lililosababisha wakose maji kwa muda
mrefu.
Kwa sababu alikuwa hajafika Chato mjini na hakuwa na taarifa
sahihi za mradi huo wa maji, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba analibeba
jambo hilo na atafuatilia hadi aelezwe ni kwa nini pampu hiyo imepelekwa
Morogoro.
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara, ndipo suala la maji
likaibuka tena na Waziri Mkuu kuamua kuchukua hatua hiyo.
“It’s unethical (ni kinyume cha maadili) kumdanganya
kiongozi wako. Nimekuuliza mara mbili mbili kama una uhakika kuwa pampu hiyo
ipo ukasema una uhakika kuwa ipo. Nimemtuma diwani na vijana wangu wakacheki
wakasema hakuna pampu,” alisema Waziri Mkuu na kumwita Diwani huyo jukwaani ili
atoe majibu.
“Pale kulikuwa na pampu mbili; moja ni ya kuvuta maji kutoka
kwenye kina kirefu na kuyapeleka kwenye pump house na nyingine ni ya
kuvuta maji kutoka kwenye pump house na kuyapeleka kwenye tenki kubwa
la kuhifadhia maji. Ile ya kutoa maji kwenye kina kirefu ndiyo haipo, wataalamu
wanajua wameipeleka wapi,” alisema Bw. Charles Manoni ambaye ni diwani wa kata
ya Nyamirembe ambayo kijiji cha Kalebezo kimo.
Waziri Mkuu alisema ahadi ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuwatumikia
wananchi kwa uadilifu. “Lazima watumishi wa umma wabadilike na kuanza
kuwatumikia wananchi kwa dhati. Hatuwezi kuwa na watumishi waongo ambao
wanamdanganya hata Waziri Mkuu.”
“Kuanzia sasa, Engineer atakaa pembeni, polisi na TAKUKURU
wamchunguze. Asitoke Chato hadi uchunguzi ukamilike. Nataka kujua nani
alichukua hiyo pampu na kwa kibali gani. Tukijiridhisha atarudi lakini kwa sasa
hivi akae kando,” alisema.
Mapema jana mchana, akizungumza na viongozi mbalimbali
wa mkoa wa Geita na wilaya ya Chato mara baada ya kupokea taarifa zao kwenye
ukumbi wa Halmashauri, Waziri Mkuu alimpa fursa Mhandisi huyo aeleze nini
kimetokea kuhusu pampu inayodaiwa kupelekwa Morogoro lakini akakanusha na kudai
kuwa ipo palepale kijijini.
“Una uhakika na hayo unayoyasema? Hiyo pampu ipo kweli
kijijini? Nikienda nitaiona?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa mara mbili na
mhandisi huyo kwamba ana uhakika asilimia 100 kwamba pampu ipo na wala
haijaenda Morogoro.
Alipotaka kujua ni kwa wananchi wa kijiji kile hawana maji
kutokana na ubovu wa pampu hiyo, alijibiwa kwamba mradi ule ulikuwa chini ya
mamlaka ya maji ya mji wa Bukoba (MBUWASA) ambako wilaya hiyo ilikuwepo zamani
kabla ya kuhamishiwa kwenye mkoa mpya wa Geita mwaka 2012.
Mhandishi huyo alisema amekuwa akifuatilia fedha za
matengenezo kutoka kwa Mkurugenzi wa MBUWASA bila mafanikio, ndipo Waziri Mkuu
akamuagiza aende nje ya ukumbi huo akapige simu na kumletea majibu ni lini
fedha hizo zitapatikana ili wananchi wa kijiji kile waendelee kupata maji.
0 comments:
Post a Comment