Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt John
Pombe Magufuli amekabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa hosipitali ya
wilaya ya Chalinze, Ikiwa ni utekelezaji wa ilani na ahadi ya
uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wa jimbo la
Chalinze.
Gari hilo la kubebea wagonjwa limekabidhiwa kwa
niaba ya Rais, na Katibu Mkuu Ikulu Peter Ilomo kwa Mbunge wa Jimbo la
Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete Ikulu jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi gari hilo,
Katibu Mkuu Ikulu Ndugu Peter Ilomo amesema gari hilo limetolewa na Mheshimiwa
Rais kwa hosipitali hiyo ikiwa ni kuitikia wito na utekelezaji wa ilani na
ahadi ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya kuboresha huduma ya afya kwa
wananchi wake kote nchini.
Aidha, Ndugu Ilomo amewaomba viongozi wa jimbo la
Chalinze kulitumia gari hilo kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuwahudumia
wananchi wa eneo hilo.
Akipokea gari hilo kwa niaba ya wananchi wa jimbo
na Wilaya ya Chalinze, Mbunge wa jimbo la Chalinze Mheshimiwa
Ridhiwani Kikwete amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kwa msaada huo na kuahidi kulitumia gari hilo kwa malengo
yaliyokusudiwa, na kusema kuwa, utendaji kazi wa Rais Magufuli umekuwa ukiungwa
mkono na wananchi wa kada mbalimbali na kuwaomba watanzania kuzidi kumuombea
kwa Mungu.
Kwa upande wake Dakta Nasoro Ally Matuzya, amesema
gari hilo limekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa umezingatia utekelezaji wa
malengo ya Milenia hususan lengo namba nne linalosisitiza kupunguza vifo
vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano
Naye Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Chalinze
Ndugu Saidi Omar Zikatimu amesema gari hilo la kubebea wagonjwa litakuwa msaada
mkubwa kwa wananchi wa jimbo hilo la Chalinze hususan katika kusaidia kutoa
wagonjwa ambao wako katika maeneo ya vijijini wilayani humo na kuwafikisha
katika hospitali ya Chalinze na hivyo kunusuru maisha yao kwa kupata huduma za
afya kwa haraka.
Mbali na Wilaya ya Chalinze kupata msaada wa gari
hilo la kubebea wagonjwa, tayari magari mengine mawili ya kubebea wagonjwa
yameshakabidhiwa katika vituo vya afya vya Kiroka na Kisemu mkoani Morogoro.
Hospitali mpya ya Wilaya ya Chalinze imepanda hadhi
kutoka kituo cha Msoga ambayo ilikuwa haina gari la kubebea wagonjwa na hivyo
kufanya usafirishaji wa wagonjwa kutoka hospitali hiyo hadi hospitali ya rufaa
ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi au kutoka maeneo ya vijijini kuwa mgumu.
0 comments:
Post a Comment