Said Msangi,Dar es Salaam.
Rais Dkt.John Pombe Magufuli amefanya ziara ya
kushitukiza katika Benki kuu ya Tanzania na kuagiza benki hiyo kusitisha mara
moja ulipaji wa malimbikizo ya malipo ambayo tayari yalishaidhinishwa na badala yake yarejeshwe wizara ya fedha na
mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.
Mpaka rais Magufuli anatoa agizo hilo,Benki kuu ya Tanzania
ilikuwa katika mchakato wa kufanya malipo ya shilingi bilioni 925.6, ambazo
wizara ya fedha ilitoa idhini ya kufanyika malipo.
Akizungumza na watendaji wakuu wa Benki kuu ya Tanzania
waliojumuisha Gavana,naibu Magavana,wakurugenzi na mameneja, rais magufuli
ametaka wizara ya fedha ifanye upya uhakiki wa malipo hayo, ili kubaini kama
walengwa walioidhinishwa kulipwa wanastahili kulipwa ama vinginevyo.
Aidha,Dkt. Magufuli ameagiza kitengo cha madeni ya
nje ambacho awali kilikuwa chini ya benki kuu na baadaye kikahamishiwa wizara ya
fedha, kirejeshwe benki kuu mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na
ulipaji wa madeni.
Wakati huo huo, rais Dkt.John Pombe Magufuli
amemuagiza Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Prof. Beno Ndulu kupitia upya orodha
ya wafanyakazi wa benki hiyo, na kuwaondoa mara moja wale wote ambao hawana
ulazima wa kuwa wafanyakazi katika benki hiyo.
Rais magufuli
ametoa agizo hilo wakati ambapo benki kuu ya tanzania ina wafanyakazi 1391.






0 comments:
Post a Comment