Ziara ya Rais wa Vietnam, Truong Tan Sang, nchini
imebainisha kwamba Tanzania ina mambo mengi ya kuiga kutoka nchi hiyo na kwamba
ikiyafanyia kazi, inaweza kupaa kiuchumi kwa kasi.
Nchi hiyo imepaa kwa kasi kubwa kiuchumi na moja ya
sababu zilizoipaisha tunaambiwa kuwa ni kutumia malighafi ilizozichukua
Tanzania zikiwamo mbegu za mpunga, korosho na samaki katika miaka ya sabini.
Siri hiyo ilifichuliwa juzi na Rais Dk. John
Magufuli wakati wa mazungumzo na kiongozi huyo na kusema kuwa mbegu hizo ndizo
zilizoifanya Vietnam kuwa kinara katika uzalishaji wa mazao hayo pamoja na
ufugaji wa samaki.
Rais Magufuli amewataka Watanzania kuiga Vietnam
katika uzalishaji wa mpunga, korosho na ufugaji wa samaki, ili kuchangia uchumi
wa nchi na pato la taifa.
Alisema Watanzania wanatakiwa kuiga Vietnam yenye
watu wanaokadiriwa kuwa milioni 91, ambao wamepiga hatua kubwa ya uzalishaji,
hata uchumi wao umekua kwa asilimia 50 na kwamba imefanikiwa kupunguza umaskini
kwa asilimia 50 na sasa imetoka katika uchumi wa chini hadi uchumi wa kati.
Kilichomshangaza Rais Magufuli ni Vietnam kuchukua
rasilimali hizo kutoka nchini na zikaipaisha kiuchumi wakati Tanzania
ikiendelea kusuasua kiuchumi. Kauli ya Rais Magufuli inaonyesha jinsi gani
alivyoguswa na hali hiyo na bila shaka ameichukua kama changamoto ya kufanyia
kazi haraka iwezekanavyo.
Jambo la msingi ni kwa Tanzania kutuma wataaamu wake
kwenda Vietnam kujifunza jinsi walivyozitumia mbegu hizo kuendelea ili tutumie
mbinu walizozitumia kuzalisha mazao hayo na samaki.
Kingine ambacho Tanzania inapaswa kufanya ni
kuwavutia wawekezaji makini na kutoka Vietnam waje kuwekeza katika sekta
mbalimbali za uchumi kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa katika biashara.
Kwa kuona umuhimu huo, Serikali imesema imefungua
milango ya uwekezaji kwa wafanyabiashara kutoka Vietnam kuja kuwekeza katika
sekta mbalimbali zikiwamo utalii, mawasiliano, mafuta, gesi, kilimo, ufugaji,
nishati na huduma za kijamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, wakati wa Mkutano uliowakutanisha wafanyabisahara wa Vietnam na
Tanzania juzi, akisema kuwa kampuni za Vietnam zilizo tayari kuwekeza nchini
zinakaribiswa kwa kuwaTanzania ina zaidi ya hekari milioni 43 za ardhi, na kati
ya hizo, hekari milioni moja ni zenye rutuba na zinafaa kwa kilimo.
Tanzania imekuwa ikiwashawishi wawekezaji kuja
nchini kuwekeza, lakini uwekezaji katika kilimo haujafanyika licha ya nchi yetu
kuwa na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo.
Sababu kubwa ambayo inasababisha wawekezaji
wasichangamkie kuwekeza katika sekta ya kilimo ni kutokana na sekta hiyo
kuhitaji mtaji mkubwa tofauti na sekta nyingine ambazo wawekezaji wanakuja na
kutengeneza faida kubwa baada ya muda mfupi.
Kwa kuwa Vietnam imeonyesha nia ya kushirikiana na
Tanzania katika sekta mbalimbali, tunawashauri viongozi wetu waweke mkazo
katika kuwashawishi wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza zaidi katika sekta ya
kilimo kwa kuwa ndio uti wa mgongo wa Taifa hili wakati linajiandaa kwenda
katika uchumi wa kati.
Ikumbukwe kwamba kilimo licha ya kuongeza chakula,
lakini pia kinaweza kutoa ajira kwa Watanzania wengi ikiwa watapatikana
wawekezaji makini. Tunaamini kuwa serikali ikiwa makini, ziara ya Rais Truong
Tan Sang nchini itafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa nchi yetu.


0 comments:
Post a Comment