MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema hakuna amri
iliyotolewa kuzuia Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliotakiwa
kufanyika Februari 26, mwaka huu.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Waliarwande Lema, alisema hayo jana alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu amri
hiyo aliyodaiwa kuito kuzuia uchaguzi huo.
“Hakuna amri ya kuzuia uchaguzi wa meya, aliyesema mahakama
imetoa zuio ni muongo,” alisema Hakimu Lema.
HAKIMU MFAWIDHI KISUTU
Awali mapema asubuhi jana, waandishi wa habari za mahakama
waliwasili ofisini kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Cysprian Mkeha kutaka ufafanuzi
kuhusu zuio linalodaiwa kutolewa na mahakama hiyo kuzuia uchaguzi huo wa meya.
Hakimu Mkeha, alisema Februari 25, mwaka huu hadi anaondoka
kazini hakukuwa na maombi yoyote yaliyowasilishwa kupinga Uchaguzi wa Meya wa
Jiji la Dar es Salaam.
Alisema aliyekuwa na zuio hilo linalodaiwa kutolewa
mahakamani alipeleke, na kwamba nyaraka halali ya mahakama lazima inakuwa na
sahihi ya hakimu aliyetoa pamoja na sahihi yake.
Mkeha aliwataka waandishi wa habari kumtafutia zuio hilo ili
aweze kulizungumzia zaidi.
WAANDISHI NA MAJADILIANO
Baada ya maelezo hayo, waandishi kwa pamoja walitoka nje ya
ofisi ya mfawidhi na kuanza mjadala kuhusu utata wa zuio hilo.
Mjadala huo ulikuwa ni juu ya namna ya kuipata amri hiyo
kuona kama ilikuwa halali ilitolewa na mahakama ama la.
Baada ya dakika kadhaa, Hakimu Mkeha alipita katika eneo
hilo na kuwataka waandishi hao kumfuata, ambapo wote waliambatana na hakimu
huyo hadi katika ofisi ya Hakimu Leman a kumuuliza kuhusu zuio hilo.
Swali: Mheshimiwa tunaomba kujua kama ulitoa amri ya kuzuia
Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliotakiwa kufanyika Februari 26,
mwaka huu.
Jibu: Hapana…Hapana.
Swali: Kuna amri ya zuio la Februari 5, mwaka huu lilitumika
kuzuia uchaguzi, lilionyesha limetolewa na wewe.
Jibu: Kulikuwa na maombi ya zuio yalifunguliwa Februari 5,
mwaka huu na Susan Masawe na Saad Khimji dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
Salaam wakiomba zuio la muda mrefu la uchaguzi uliotakiwa kufanyika Februari 8,
mwaka huu.
Hakimu Lema alisema maombi hayo yalikuwa ya upande mmoja,
ambapo mahakama ilitoa zuio dogo na kutoa muda mfupi hadi Februari 15 maombi
yasikilizwe kwa pande zote mbili kuwapo.
“Februari 15, mwaka huu ilipofika, waleta maombi hawakutokea
mahakamani, kesi ikaahirishwa hadi Februari 23, mwaka huu ambapo pia hakuna
aliyetokea.
“Kwa kuwa hakuna aliyefika, mahakama ililiondoa shauri hilo,
hivyo na zuio dogo pia liliondoka kwa sababu maombi yaliondolewa mahakamani,”
alisema.
Hakimu Lema alisisitiza kuwa hakuna zuio lililotolewa na
mahakama na kwamba aliyesema kuna zuio ni muongo.
Hata hivyo, nakala inayodaiwa kuzuia uchaguzi huo ni ya
Februari 5, mwaka huu ambayo kisheria haipo mahakamani tangu Februari 23 shauri
lilipoondolewa.
Hakimu Mfawidhi Mkeha alipotakiwa kuthibitisha kama alipokea
maombi Februari 25 ya kuzuia uchaguzi na kumpangia hakimu yoyote, alisema
hakuna maombi yoyote yaliyowasilishwa mahakamani hadi muda wa kazi unamalizika.
UCHAGUZI FEBRUARI 26
Vurugu kubwa zilitokea katika Uchaguzi wa Meya wa Jiji la
Dar es Salaam uliopangwa kufanyika Februari 26, mwaka huu mara baada ya
kuahirishwa tena kwa mara ya nne.
Katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti
wa uchaguzi huo, Theresia Mmbando ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es
Salaam, alitangaza kuuahirisha kwa madai ya kuwekewa pingamizi mahakamani na
wakazi wa jiji hilo, Susan Massawe na Saad Khimji.
Madiwani kutoka vyama vinavyounda Umoja wa katiba ya
Wananchi (Ukawa), walidai kuwa hawajapata barua ya pingamizi hilo, hivyo
wakataka waruhusiwe kufanya uchaguzi peke yao kwa kuwa akidi ya madiwani
kufanya uchaguzi ilikuwa imetimia.
Wakati Ukawa wakijiandaa kufanya uchaguzi huo wenyewe,
polisi zaidi ya 15 walivamia ukumbini na kuwataka waondoke jambo
lililowachukiza na kuibua patashika ndani ya ukumbi.
KAULI YA SIMBACHAWENE
MTANZANIA lilipomtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene kuhusu utata huo,
alisema kwamba hajapata taarifa zozote hadi kufikia jana.
“Nilitegemea leo (jana) nipate taarifa ya kilichotokea,
lakini kwa bahati mbaya huyo aliyepaswa kunipa taarifa hiyo niliambiwa alipigwa
yuko hospitali. Siwezi kusema chochote kwa sasa hadi nitakapopata taarifa rasmi
ndiyo nitaeleza msimamo wa Serikali,” alisema Simbachawene.
MDEE, KUBENEA MBARONI
Wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) pamoja na madiwani wawili wa chama hicho, wamehojiwa katika Ofisi ya
Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutokana na vurugu zilizotokea
kwenye uchaguzi huo mwishoni mwa wiki.
Wabunge hao ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Saed Kubenea
(Ubungo) ambaye aliunganishwa katika mkasa huo wakati alipokuwa akiwasilisha
malalamiko yake kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lukas Mkondya kuhusu
kusitishwa kwa uchaguzi huo.
Wakati akiwasilisha malalamiko hayo, alielezwa kwamba na
yeye ni miongoni mwa watuhumiwa waliokuwa wakitafutwa kwa ajili ya mahojiano,
hivyo alitakiwa kutoa maelezo yake.
Mdee akiwa ameambata na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther
Bulaya, alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Kati saa 7:20 mchana akiwa
kwenye gari aina ya Prado yenye namba T 781 ANU huku ikiongozana na gari ya
polisi Land Cruiser yenye namba T 424 BZN.
Baada ya kufika kituoni hapo, alipelekwa katika chumba cha
Mkuu wa Upelelezi Kanda Malaumu ya Dar es Salaam na kuhojiwa.
Mbunge mwingine ambaye anatakiwa kufika katika kituo hicho
kwa ajili ya kuhojiwa ni Mwita Waitara (Chadema) ambaye anatafutwa na polisi.
Hata hivyo, ilipofika saa 11:50 jioni waandishi wa habari
waliokuwapo katika eneo la Polisi Kituo Kikuu cha Kati, walielezwa kwamba
dhamana ya Mdee imezuiwa huku Kubenea akiachiwa.
Katika mahojiano hayo ya polisi, madiwani wa Hamphrey Sambo
wa Mbezi na Efraim Kinyafu wa Saranga wote wa Chadema pamoja na kada wa chama
hicho Kata ya Mabibo, Shafii Juma waliunganishwa katika kesi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo, Kubenea
alisema alifika kwa lengo la kutoa taarifa ya udanganyifu uliowasilishwa na
Wakili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elias Nawela kuhusu zuio la kupinga
kufanyika kwa uchaguzi huo.
POLISI WATINGA KWA MEYA
Awali maofisa wawili wa Jeshi la Polisi waliokuwa wamevaa
kiraia kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala, walifika katika Ofisi
ya Meya wa Ilala iliyopo eneo la Mnazi Mmoja na kumtaka meya hiyo, Charles
Kuyeko kuwapatia majina ya madiwani waliofanya vurugu katika uchaguzi huo.
Maofisa hao walikuwa na magazeti mawili ya kila siku ambayo
yalikuwa na picha zilizoonyesha madiwani hao wakilumbana na polisi ambapo meya
huyo alijibu kwamba hawatambui kwakuwa mkutano huo ulikuwa na madiwani wengi.
Alisema iwapo wanahitaji kuwakamata, aliwataka kusubiri
kikao cha madiwani kitakachofanyika Machi 3, mwaka huu na hivyo wanaweza
kuwapata ila akatoa angalizo kwamba wasubiri hadi kikao hicho kitakapomalizika.
PROFESA SAFARI
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makamu Mwenyekiti
wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema kosa alilokamatiwa Mdee ni
kumfanyia vurufu msimamizi wa uchaguzi huo, Mmbando.
“Halima hakuhusika kabisa na vurugu zile, lakini tunajua
hizi ni hila za CCM na kesho (leo) tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari katika
Ukumbi wa Karimjee,” alisema Profesa Safari ambaye ni mwanasheria.
WANASHERIA WAKOSOA
Wanasheria mbalimbali wamesema kuwa waliosababisha Uchaguzi
wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuahirishwa wachukuliwe hatua za kisheria kwa
kuwa ni kosa la kijinai.
Kauli hiyo ya wanasheria imekuja muda mchache baada ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa tamko juu ya amri iliyotolewa kuzuia
uchaguzi huo kuwa si halali.
Akizungumza na MTANZANIA kupitia simu yake ya kiganjani,
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema kitendo kilichofanywa na
chama tawala CCM ni cha kihuni na kwamba hakipaswi kufumbiwa macho.
“Huu ni uhuni waliofanya CCM…wachukuliwe hatua za kisheria,
na polisi ndio wafanye hivyo kwa sababu ni kosa la jinai. Wanaendaje kusema
uongo na kuzuia shughuli halali kwa uongo?” alihoji Lissu.
Kwa upande wake aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura, alieleza kushangazwa kwa kitendo hicho
akisema waliohusika kufanya hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.
“Nadhani nitoe maoni yangu binafsi, si ya TLS kwa sababu
mimi nimemaliza muda wangu hivi karibuni…hilo jambo kama ni la kweli
limenisikitisha sana na kunishangaza kwa chama tawala kughushi, kudanganya na
uchaguzi halali kuahirishwa, kwanza imetia hasara. Hivyo wahusika wachukuliwe
hatua kwa sababu ni kosa la jinai,” alisema Rwechungura.
0 comments:
Post a Comment