WAKATI Tanzania ikiendelea kunufaika na ugunduzi wa gesi
asilia, ambayo imeshaanza kutumika kufua asilimia 70 ya umeme unaotumika
nchini, ugunduzi mwingine mkubwa wa gesi kuwahi kutokea nchi kavu, umefanyika
na kuthibitishwa katika mkoa wa Pwani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika ziara ya Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, katika mitambo ya kuchakata na kusafirisha gesi ya Madimba,
mkoani Mtwara, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC), Dk James Mataragio, alisema wiki iliyopita kulifanyika ugunduzi wa gesi
nyingine, futi za ujazo trilioni 2.17.
Kwa mujibu wa Dk Mataragio, ugunduzi huo uliofanyika katika
Kitalu cha Ruvu, ni mbali na ugunduzi uliokuwa umeshafanyika wa futi za ujazo
trilioni 55.08 katika kina cha bahari na nchi kavu.
Kuhusu gesi ya Ruvu, alisema anazo taarifa zinazoonesha
kwamba kuna gesi nyingi katika Bonde la Ruvu, ambako ndio eneo pekee la nchi
kavu lenye gesi nyingi hapa nchini na kuongeza hiyo ndio tija anayoizungumzia.
Kuhusu mitambo hiyo ya Madimba, Dk Mataragio alisema mradi
huo ulianza kutekelezwa mwaka 2011, ukiwa na sehemu kuu tatu ambazo ni; ujenzi
wa bomba la inchi 36 kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, Dar es Salaam, ujenzi wa
mitambo hiyo ya kuchakata gesi asilia Madimba na mitambo mingine Songo Songo.
Kwa mujibu wa Dk Mataragio, gharama za mradi huo hadi sasa
ni takribani Dola za Marekani bilioni 1.2, ambazo kati ya hizo asilimia tano ni
mchango wa Serikali na nyingine ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Exim Bank ya
China.
Pamoja na gharama hizo, Dk Mataragio alisema matumizi ya
gesi asilia iliyotokana na mradi huo katika kufua umeme, yameokoa matumizi ya
fedha za kigeni takribani Dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka, ambazo
zilikuwa zitumike kununulia mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sasa tunazalisha wastani wa
futi za ujazo milioni 45-50 kwa siku (mmscfd) hapa Madimba. Hata hivyo uwezo
wetu ni kuzalisha futi za ujazo milioni 130 kwa siku (mmscfd) kutoka katika
visima vitano vya gesi asilia vilivyopo eneo la Mnazi Bay,” alisema.
Akizungumza baada ya kuelezwa kuhusu utendaji wa mitambo
hiyo na faida yake kwa Taifa, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema pamoja na mafanikio
ya sasa ya kuwasha umme kwa kutumia gesi asilia, ni lazima gesi ipelekwe kwa
wananchi kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
0 comments:
Post a Comment