HABARI kwamba Shirika la Umeme (Tanesco) limeanza mkakati wa
kushusha gharama za umeme ili kumpunguzia mzigo mwananchi ni ya kupongezwa ila
isije ikawa nguvu ya soda.
Kwa mujibu wa habari iliyoandikwa katika gazeti hili jana,
tayari shirika hilo limewasilisha katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(Ewura) maombi ya kushusha bei ya umeme kwa asilimia 1.1.
Katika maombi hayo, Tanesco pia imeamua kuondoa kabisa
gharama za maombi ya awali ya wateja wapya, zinazojulikana pia kama gharama za
fomu ambazo ni Sh 5,900.
Shirika hilo pia, kupitia maombi yake kwa Ewura linaondoa
gharama za huduma (service charges) zinazofikia Sh 5,520 ambazo wateja wa
majumbani wamekuwa wakikatwa kila mwezi.
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba, anasema kuwa
punguzo hilo la asilimia 1.1 ni kwa mwaka huu lakini matarajio ni kwamba mwaka
kesho watapunguza tena kwa asilimia 7.9. Anafafanua kuwa Tanesco imewasilisha
maombi yake Ewura pamoja na takwimu halisi zinazoshawishi mantiki ya
kubadilishwa kwa bei hizo.
Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba tayari Ewaura imeshapokea
maombi hayo yanayopaswa kujibiwa ndani ya siku 24 na keshokutwa (Ijumaa),
mamlaka hiyo itakutanisha wadau ili kuyajadili.
Matumaini yetu ni kwamba, Ewaura itayapitisha maombi hayo
ambayo kwa mujibu wa Mramba, shirika lake limejiridhisha baada ya kufanya
tathmini kwamba kwa kumpa mwananchi ahueni hiyo haitaathiri utendaji wa
shirika.
Mkurugenzi huyo amekanusha pia madai ya baadhi ya watu
wanaosema kwamba serikali imeilazimisha Tanesco kushusha bei ya umeme na
wakaonesha wasiwasi kwamba kwa kufanya hivyo shirika litafilisika.
Tumepokea kwa mikono miwili habari hiyo njema inayoakisi
kile ambacho kimekuwa kikisemwa kwamba nchi yetu itakapoanza kutumia umeme wa
gesi kwa kiwango kinachotakiwa, gharama za umeme zitapungua.
Kwa wale waliokuwa hawaamini kwamba kuna uwezekano wa
gharama za umeme siku moja kushuka ndio ambao wamekuwa na hofu kuwa Tanesco
itayumba na kudhani kwamba punguzo hili ni la kisiasa.
Kushuka kwa gharama za umeme kunatokana na ukweli kwamba
gharama za umeme wa gesi ambao umeongezeka katika gridi ya taifa ni nusu ya
gharama za umeme unaozalishwa kwa mafuta.
Ongezeko la umeme wa gesi, linakwenda sambamba na ongezeko
la ujazo wa maji katika mabwawa makubwa hasa Mtera, kwa kuwa umeme utokanao na
maji ni rahisi pia kulinganisha na wa mafuta.
Wakati tukiipongeza Tanesco kwa hatua hiyo huku tukiwa na
matumaini kwamba gharama za umeme zitazidi kupungua mwaka hata mwaka kadri
umeme wa gesi unavyoongezeka, shirika hilo litasimama imara katika kuhakikisha
haliyumbi.
Wananchi wanatarajia kuona Tanesco ikiwa haiishii kwenye
kupunguza gharama za umeme pekee, bali pia kuboresha huduma zao ikiwa ni pamoja
na kushughulikia maombi mapya ya kuwekewa umeme kwa muda mfupi. Kwamba Tanesco
pia itahakikisha umeme haukatikikatiki sambamba na kuitikia kwa haraka miito ya
wateja wao wanapokuwa na tatizo la umeme.
0 comments:
Post a Comment