NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla amewasimamisha kazi wauguzi sita wa wadi
ya wazazi Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam, kutokana na kudai rushwa ya
vifaa vya kujifungulia kwa mama mjamzito.
Wauguzi waliosimamishwa kazi ni Agnes Mapashe,
Beatrice Temba, Mariam Mohamed, Merion Said, Hadija, Salum na Elizabeth
Mwilawa. Wauguzi hao walidai vifaa hivyo kwa Roshan Seif aliyefika hospitalini
hapo kujifungua. Mtu huyo alitakiwa kupeleka baadhi ya vifaa vya kujifungulia,
ikiwa ni pamoja na glovu kwa madai kuwa havipatikaniki hospitalini hapo.
Mbali na hatua hiyo , uongozi wa hospitali hiyo
umepewa miezi mitatu kuhakikisha umeboresha wadi ya watoto wachanga kwa
kuongeza idadi ya vitanda kutoka tisa vilivyopo ili kila mtoto aweze kulala
kitanda chake peke yake.
Kadhalika, uongozi wa hospitali hiyo umepewa siku 30
kununua vifaa katika chumba cha upasuaji kwa wanawake, waweze kuwa na chumba
chao maalumu peke yao, ikiwa ni kupunguza idadi ya wanaopewa rufaa na kwenda
kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Dk Kigwangalla alifikia uamuzi huo hospitalini hapo
jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwa lengo la kutaka kujua changamoto
mbalimbali, wanazokumbana nazo wagonjwa katika kupata huduma za afya.
Kuhusu wauguzi waliosimamishwa kazi, aliutaka
uongozi wa hospitali hiyo kuwachunguza hadi kujulikana mmoja wapo aliyehusika
kudai rushwa hiyo ili hatua ziweze kuchukuliwa, kwa lengo la kukomesha vitendo
hivyo vyenye kusababisha hatari kwa usalama wa wazazi na wajawazito.
Aliutaka uongozi wa hospitali hiyo, kuchukua hatua
dhidi ya watumishi hao waliohusika kudai rushwa kwa wateja, ilhali wao wakiwa
na kazi nzuri wakilipwa vizuri kulingana na taaluma zao.
“Mchukue hatua dhidi ya watumishi waliodai rushwa
kwa wateja. Hawa wanatuangusha, tunataka kupunguza vifo vya wajawazito, lakini
wao wanaturudisha nyuma, wanadai glovu na vifaa, Mganga Mkuu wa Manispaa
wafuatilie wote na mchukue hatua za kinidhamu,” alisema Dk Kigwangalla.
Alisema vilevile wauguzi hao, wakabidhiwe kwa Baraza
la Wauguzi nchini ili kuchunguza mienendo yao ya maadili kwa kuwa hata katika
sera ya afya nchini, hairuhusiwi kudai vifaa kwa wajawazito.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Dk Kigwangala alielezwa
na mmoja wa ndugu wa mama aliyekwenda kujifungua, akitaka kujua kama wajawazito
wenye kadi ya bima ya afya iwapo hawaruhusiwi kutibiwa bila kuwa na vifaa vya
kujifungulia.
Ndugu huyo aliyetambulika kwa jina la Ismail Mkingi,
alidai kuwa alimfikisha mama huyo hospitalini hapo jana kwa ajili ya
kujifungua, lakini akiwa katika hatua za mwisho za kujifungua, ndipo muuguzi
aliyekuwa akimshughulikia alimtaka akanunue vifaa hivyo, huku akiambiwa kama
hawezi ampe Sh 5,000 (muuguzi) ili akamsaidie.
Alisema ndugu hao walihangaika na kuhakikisha vifaa
hivyo vimepatikana, ili huduma ziweze kutolewa kwa mama huyo ambaye alijifungua
jana.
Baada ya kusikiliza, Dk Kigwangalla aliyekuwa
akitoka chumba cha malalamiko hospitalini hapo na kuambiwa yapo malalamiko
mawili tu kutoka kwa wagonjwa yakihusu gharama kubwa za baadhi ya vipimo,
alikutana na Mkingi na kumweleza hayo, ambapo Naibu Waziri aliamua kwenda moja
kwa moja wadi ya wazazi na kumsaka muuguzi aliyehusika bila mafanikio.
Akiwa wadini hapo, Dk Kigwangalla alionana na mama
mjamzito aliyetakiwa vifaa hivyo, ambapo alieleza kuwa baada ya kupimwa
alitakiwa kutoa vifaa hivyo na kama hatavipata, atoe fedha ili aweze kuletewa
pale alipo.
Dk Kigwangalla aliagiza muuguzi huyo aliyehusika
atafutwe, lakini hakupatikana kutokana na wahusika hao kutoweza kutaja majina
moja kwa moja. Ndipo Naibu Waziri alipofikia uamuzi wa kuwasimamisha kazi wote
ili uchunguzi ufanyike ili apatikane aliyehusika.
Aidha alitembelea chumba cha upasuaji mkubwa wa
wazazi hospitalini hapo, upasuaji wa wagonjwa wengine, wadi za watoto na
maabara ya hospitali hiyo.
Aliitaka Manispaa ya Temeke inunue vifaa vya wadi
hiyo ya upasuaji ili wanawake wajawazito, waweze kuhudumiwa peke yao na kwamba
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo atajua atakakopata fedha. Alisema ndani ya muda huo
atakwenda kukagua na kuona kama wadi hiyo inafanya kazi.
“Mkurugenzi atajua atakapotoa hela, siku 30 nitakuja
kukagua nione wodi ya upasuaji inafanya kazi, kama haitakuwa tayari, nitaifunga
ili tuone utumishi wenu utakuwa wapi,” alisema Dk Kigwangalla.
Kuhusu wadi ya wazazi, alisema hali ya akinamama
wajawazito hairidhishi, kuna msongamano mkubwa na jengo halitoshi, hivyo kwa
haraka iongezwe ghorofa nyingine.
Pia chumba cha upasuaji wa wajawazito kikamilike
ndani ya siku 30, Manispaa ya Temeke inunue vifaa vya wadi ya upasuaji,
wapunguze idadi ya wanaoenda Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwani kuwapeleka
huko ni kuongeza msongamano.
Dk Kigwangalla alisema wadi mbili za upasuaji
zilizomo hospitalini hapo, zina hali mbaya. Alitoa miezi sita zikarabatiwe na
zikamilike katika viwango vinavyotakiwa.
Alionya kuwa endapo atakuta ziko hivyo hivyo miezi
sita ijayo, atazifunga. Alisema miongozo yote ipo, wahudumu katika hospitali
hiyo ni madaktari na wanajua vyema kinachoendelea, hivyo uongozi wa Hospitali
umwambie Mkurugenzi aweze kutoa fedha na kuweka kipaumbele katika afya.
0 comments:
Post a Comment