JUHUDI za Serikali ya Awamu ya Tano za kufufua na kujenga
viwanda vingi kadri inavyowezekana zimekuwa zikipata changamoto hasa kutokana
na umeme kuendelea kutokuwa wa uhakika.
Gazeti hili jana lilibeba habari inayohusu kiwanda cha chuma
cha Lodhia Group kinachomiliki kampuni nane hapa nchini kikiwamo kiwanda cha
kutengeneza nondo kilichopo mjini Arusha, kupunguza wafanyakazi 340 na kisha
kufunga uzalishaji kabisa kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa
mara.
Hiyo ni habari mbaya kwa kuwa Serikali hii inayoongozwa na
Rais John Magufuli imedhamiria kuinua viwanda na si kuvifunga, na wala kuona
wafanyakazi wake wakikosa ajira kwa kuwa lengo la kuweka mikakati ya kufufua
viwanda ni moja ya njia ya kuongeza ajira.
Katika habari hiyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Lodhia Group,
Sailesh Pandit amekaririwa akimwambia Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina kuwa umeme umekuwa ni kikwazo kikubwa
katika uzalishaji wa nondo kiwandani hapo.
Anasema, kwa saa moja, umeme unaweza kukatika hata mara 10,
hivyo kuzorotesha uzalishaji. Hali hiyo imesababisha kiwanda kulazimika
kupunguza wafanyakazi na hatimaye kusimamisha uzalishaji kwa kuwa hakuna umeme
wa uhakika.
Mkurugenzi huyo akaenda mbali zaidi kwamba, wafanyabiashara
wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakifurahia hali hiyo kwa kuwa wanatumia mwanya wa
uhaba wa nondo kuingiza nyingine kutoka nje ya nchi ambazo hazikidhi viwango
kwa kupitia njia za panya.
Kwa kuwa nia kubwa ya Serikali ni kuongeza viwanda,
tunaamini itaweka juhudi zaidi kama alivyosema Naibu Waziri baada ya kusikia
kilio cha mkurugenzi huyo katika kuhakikisha Shirika la Umeme nchini (Tanesco)
linafanya kila liwezalo kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la umeme katika
Jiji hilo la Arusha ambalo ni la kitalii na kibiashara.
Arusha ni Jiji ambalo limekuwa na shughuli nyingi za kitaifa
na kimataifa, hivyo kukatikakatika kwa umeme si tu ni adha kwa viwanda, lakini
pia ni kikwazo kwa ukuaji wa utalii nchini kwa kuwa jiji hilo ni kitovu cha
utalii.
Tunajua serikali inaendelea na mradi uliopewa jina la ‘uti
wa mgongo’ kwa kujenga njia ya umeme wenye msongo mkubwa zaidi utakaowezesha
kusafirisha umeme mwingi nchi nzima hadi mipakani, Arusha ikiwemo, lakini kabla
mradi huo haujakamilika, ni vyema Tanesco ikahakikisha mji kama Arusha inakuwa
na umeme wa uhakika ili kuimarisha viwanda, utalii na shughuli zingine za
uchumi na kijamii.
Lililotokea katika kiwanda hicho na hasa hatua ya kufunga
uzalishaji, linarudisha nyuma juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika
kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda. Ni katika muktadha huo, tunahimiza watendaji
kuwa makini katika kumsaidia Rais kutimiza lengo hili adhimu.
Tunasema hivyo, si kwa kulaumu uongozi mzima wa Mkoa wa
Arusha, kwa kuwa wao walikuwa na nafasi ya kutalifutia ufumbuzi suala hilo
kabla halijawa kubwa kwa kiasi fulani, nia ni kuwataka watendaji wa Serikali
kumsaidia Rais Magufuli katika jitihada zake za kufufua na kujenga viwanda
vingi kadri ya uwezo wa nchi.
0 comments:
Post a Comment