HATIMAYE kitendawili cha nani kuliongoza Jiji la Dar
es Salaam kimeteguliwa jana, baada ya wajumbe 158 kupiga kura ya kumchagua meya
wa jiji hilo na kumchagua Diwani wa Kata ya Vijibweni, Isaya Charles kushika
kiti hicho.
Charles ambaye ni Diwani wa Chadema Kata ya
Vijibweni Manispaa ya Temeke, alimshinda mpinzani wake kwa kupata kura 84 dhidi
ya kura 67 alizopata mgombea wa CCM, Yenga Omary.
Uchaguzi huo ulifanyika baada ya Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, kuamuru uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
kufanyika jana kama ilivyopangwa.
Uchaguzi huo ulifanyika katika Ukumbi wa Karimjee,
Dar es Salaam, na kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uanze
nchini mwaka 1992, Jiji la Dar es Salaam litakuwa chini ya Upinzani.
Uchaguzi huo ulianza saa 4:37 asubuhi baada ya akidi
ya wapiga kura kutimia ambapo wajumbe waliokwisha kufika hadi muda huo walikuwa
158 kati ya wajumbe 163 waliopaswa kushiriki kupiga kura.
Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Theresia Mmbando ndiye alifungua kwa kuwataka wajumbe kuwa
watulivu katika muda wote wa uchaguzi huo ili kufanikisha kazi hiyo ambayo
ilikwama kwa muda mrefu.
Baada ya ufunguzi huo aliwakaribisha wajumbe mmoja
mmoja kujinadi kwa wapiga kura, akianza mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Yenga Omary aliyeahidi kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.
Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) aliyeungwa mkono na Ukawa, Charles aliyetaja vipaumbele vyake viwili
vya kuanza navyo kazi endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo, akiahidi
kutafuta utatuzi wa tatizo la uhaba wa madawati katika shule nyingi za msingi
na kutatua kero ya foleni jijini Dar es Salaam.
Awali uliandaliwa utaratibu wa kupiga kura kwa
kutumia namba zilizogawiwa kwa wapiga kura wote, lakini Chadema ilipinga
matumizi ya namba na kutaka kutumia majina kwa kwenda kupiga kura, utaratibu
uliokubalika.
Ilipotimu saa 5:20 wajumbe walianza kupiga kura kwa
utaratibu wa kuita majina kwa kuanzia na Manispaa ya Ilala, ikafuatia Manispaa
ya Kinondoni kisha kumalizia na Manispaa ya Temeke.
Baada ya kumalizika kwa upigaji kura, kazi ya
kuhesabu kura lilianza na mgombea wa CCM alienda kusimamia kura zake mwenyewe
huku wa Chadema akisimamiwa na Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sarah
Yohana alisimama na kuanza kutangaza matokeo hayo kwa kueleza kuwa waliopiga
kura ni 158 na kura halali zilikuwa 151 na kura saba ziliharibika.
“Idadi ya waliopiga kura ni 158, kura zilizoharibika
ni kura saba, kura halali 151. Mgombea Yenga Omary amepata kura 67 na mgombea
Isaya Charles amepata kura 84,” alisema Yohana.
Meya huyo mpya wa Jiji la Dar es Salaam, Charles
aliwashukuru wajumbe wote kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo huku akiahidi
kufanya kazi na makundi yote.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi huo, Diwani wa Kata ya
Mwananyamala, Songoro Mnyonge alisema demokrasia imefuata mkondo wake na sasa
kilichobaki ni kufanya kazi.
Aliyekuwa mgombea wa Urais kupitia Chadema
aliyeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa alisema anashukuru kwa demokrasia
kuheshimiwa na kumtaka Meya huyo mpya wa jiji kufanya kazi kwa bidii. Uchaguzi
huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa na mawaziri ambao pia
walikuwa ni wapiga kura katika uchaguzi huo.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria na kupiga kura
ni Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
Upande wa wanasiasa wa upinzani ni Mwenyekiti wa
Chadema, na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji na wengineo.
0 comments:
Post a Comment