KWA mara ya kwanza Bajeti ya Serikali ya Rais John
Magufuli inatarajiwa kuwasilishwa Juni 9, mwaka huu, kwenye Mkutano wa Tatu wa
Bunge la 11, unaoanza mjini Dodoma kesho.
Bajeti hiyo itawasilishwa rasmi na Waziri wa Fedha
na Mipango, Dk Phillip Mpango saa 10 kamili jioni siku ya Alhamisi baada ya
kuwasilishwa kwa taarifa ya Hali ya Uchumi wa Nchi asubuhi siku hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha
Bunge jana, ilieleza kuwa baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, ambayo
mapendekezo yake ya awali kwa wabunge yalibainisha kuwa itakuwa ni ya Sh
trilioni 29, wabunge wataijadili kwa muda wa siku tisa kuanzia Juni 13 hadi
Juni 21, mwaka huu.
Pamoja na bajeti hiyo, pia Dk Mpango atawasilisha
Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2015/16 hadi 2020/21.
“Baada ya kuwasilishwa kwa mpango huo, Bunge pia
litapokea na kujadili utekelezaji wa bajeti kwa wizara zote kwa mwaka wa fedha
2015/16 na makadirio ya matumizi ya Serikali 2016/17, kazi itakayofanyika
kuanzia Aprili 22 hadi Juni 2, mwaka huu,” ilieleza taarifa ya Bunge.
Hivi karibuni, Dk Mpango aliwasilisha mapendekezo ya
ukomo wa bajeti hiyo ya mwaka 2016/17 mbele ya wabunge jijini Dar es Salaam, na
kubainisha kuwa inatarajiwa kuwa ya Sh trilioni 29.539 sawa na ongezeko la
asilimia 31.32 ya bajeti iliyopita ya mwaka 2015/2016.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya bajeti hiyo, Serikali
inalenga kutumia Sh trilioni 15.105 sawa na asilimia 82 ya mapato ya ndani,
mapato ya kodi na yasiyo na kodi na mapato kutoka halmashauri Sh trilioni 2.693
na Sh bilioni 665.4 na washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh
trilioni 3.600 ambayo ni sawa na asilimia 12 ya bajeti yote.
Akichanganua mapendekezo hayo, alisema kwa upande wa
matumizi katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inapanga kutumia Sh trilioni
17.719 kwa matumizi ya kawaida na Sh trilioni 11.820 kwa matumizi ya maendeleo
sawa na asilimia 40 ya bajeti yote.
Aidha, alitaja vipaumbele vingine kuwa ni viwanda
vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha
maendeleo ya uchumi na rasilimali watu na mazingira wezeshi kwa uendeshaji
biashara.
Pamoja na kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, pia katika
Mkutano huo Tatu wa Bunge unaoanza kesho, pamoja na kuwasilishwa hati za
mezani, Bunge pia litapokea Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15 ambayo hivi karibuni ilikabidhiwa kwa Rais
Magufuli.
“Pia Bunge litapokea majibu ya Serikali kuhusu hoja
zilizotolewa na CAG kwa hesabu za mwaka wa fedha 2014/15,” ilisema taarifa hiyo
ya Kitengo cha Mawasiliano cha Bunge.
Taarifa hiyo ilisema pia katika mkutano huo, Bunge
litajadili na kupitisha miswada miwili ambayo ni Muswada wa Sheria ya Matumizi
wa Mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2016.
“Vilevile inategemea kuwa Serikali itawasilisha
bungeni miswada ya Sheria kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa bungeni mara
baada ya shughuli ya kupitisha bajeti kukamilika,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, katika mkutano huo kutakuwa na shughuli ya
uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge kwa ajili ya kuziba nafasi iliyoachwa wazi
baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kufanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa
Kamati za Kudumu za Bunge. Nafasi hiyo imeachwa wazi na Mbunge wa Viti Maalumu,
Dk Mary Mwanjelwa.
Aidha, wabunge wapya wanne ambao ni Shamsi Vuai
Nahodha wa Jimbo la Kijitoupele, Ritha Kabati na Oliver Semguruka wote Viti
Maalumu CCM na Lucy Owenya wa Viti Maalumu Chadema, wanatarajiwa kuapishwa
rasmi.


0 comments:
Post a Comment