Kwa mujibu wa taarifa gazeti hili ilizopata kutoka
chanzo cha kuaminika, PAC haikuridhishwa na majibu ya hoja nyingi zilizotolewa
na watendaji wakuu akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
kuhusu mkataba wa Lugumi baada ya kukutana nao jana mjini hapa.
“PAC imelazimika kuunda kamati ndogo kesho (leo),
itakayokuwa na nguvu kuhoji mambo yote ukiwemo mkataba huo kwa sababu majibu
yaliyotolewa hayakuridhisha,” kilieleza chanzo hicho.
Kiliongeza kuwa baadhi ya mambo yanayokanganya PAC
ni kufahamu nani mkweli kati ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kupitia taarifa ya ukaguzi na maelezo ya Jeshi la Polisi kuhusu gharama
za mkataba.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, taarifa ya CAG inaonesha
kuwa mkataba huo ni wa Sh bilioni 37.742 wakati maelezo yaliyotolewa na
viongozi wa Jeshi hilo walipohojiwa na PAC hiyo jana, walisema ni Sh bilioni
37.163.
Hivyo kuwepo kwa tofauti ya zaidi ya Sh milioni
578.972. Aidha, utata mwingine ni jeshi hilo kukosa maelezo ya kwa nini katika
kutafuta mzabuni kwenye mradi huo, walitumia mfumo wa mzabuni mmoja badala ya
wengi.
Chanzo chetu kilisema katika mahojiano na viongozi
hao wa polisi, walishindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza kwa nini kitengo cha
manunuzi cha jeshi hilo walitumia mfumo huo. Hivyo kutokana na utata huo,
Kamati hiyo imeamua kukutana na Spika leo ili kumtaarifu hatua waliyofikia ya
kuunda Kamati Ndogo.
Juzi, taarifa ya Utekelezaji wa Mkataba tata wa
Kampuni ya Lugumi Enterprises ulioshinda zabuni mwaka 2011 ya kufunga mashine
za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi vya wilaya nchi nzima kwa
gharama ya Sh bilioni 37, ulitua ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC) na kuanza kujadiliwa.
Akizungumza na gazeti hili juzi bungeni, Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly alisema taarifa ya utekelezaji wa
mkataba huo ilifikishwa bungeni Jumatatu na juzi asubuhi wamepewa na wakaanza
kuujadili.
Awali, Aprili 5, mwaka huu mjini Dar es Salaam,
Kamati hiyo ilitoa siku saba kuanzia siku hiyo kwa Jeshi la Polisi nchini
kupeleka mkataba walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi iliyopewa zabuni ya
kufunga mashine 108 katika vituo tajwa nchini ila hadi sasa ni vituo 14 tu ndivyo
vilivyofungwa mashine hizo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kamati hiyo kukutana na
Jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu za jeshi hilo za mwaka 2013/14
zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
kubainika kuwa na ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo.
Ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo mwingine ni
pamoja na kampuni hiyo kulipwa asilimia 99 ya fedha zote za mkataba huo wenye
thamani ya Sh bilioni 37, huku kazi iliyofanywa ni chini ya robo.
0 comments:
Post a Comment