KOCHA wa zamani wa timu ya soka ya taifa,‘Taifa
Stars’, Dk Mshindo Msolla amesema maandalizi ya zimamoto ndiyo yaliyoiondosha
Azam kwenye michuano ya kimataifa juzi.
Azam iliyokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la
Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC), juzi ilitupwa nje ya michuano hiyo baada ya
kufungwa mabao 3-0 na Esperance ya Tunisia katika mechi ya marudiano ya raundi
ya pili iliyochezwa mjini Tunis.
Matokeo hayo yanaifanya Azam itolewe kwa jumla ya
mabao 4-2 baada ya kushinda mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Dar
es Salaam Aprili 10, mwaka huu. Akizungumza jana, Dk Msolla alisema Azam
haikuwa na maandalizi ya kutosha, ilicheza mechi chache za ligi ndipo ikaenda
kucheza na Esperance wakati wapinzani wao walijiandaa muda mrefu.
“Maandalizi ya zimamoto yaliiponza Azam, wenzetu
walijiandaa muda mrefu na walijua kwamba wanacheza na walijua kwamba wanacheza
na timu iliyowafunga mechi ya kwanza,” alisema. Dk Msolla alisema kingine
kilichoiponza Azam ni kukosekana umakini kwa wachezaji wa timu hiyo, jambo
ambalo lilifanya kufungwa mabao mepesi. “Timu haikuwa na mawasiliano, ikafungwa
mabao mepesi, wachezaji walimuacha Bocco (John) peke yake muda mrefu, hivyo
mabeki wa Esperance walipenya wanavyotaka,” alisema.
Naye Grace Mkojera anaripoti kuwa nahodha msaidizi
wa Azam FC, Himid Mao, amewataka mashabiki wao kutokata tamaa baada ya kutolewa
na Esperance ya Tunisia.
Kwa mujibu wa tovuti ya Azam FC, Mao aliyeingia
dakika ya 79 katika mchezo huo kuchukua nafasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’,
alisema kwa sasa nguvu zao zote wanahamishia katika Ligi Kuu soka Tanzania Bara
na Kombe la FA, akiwaahidi kuwa watapambana kuchukua makombe yote hayo.
“Matokeo yamewasikitisha watu wengi hasa sisi
wachezaji, lakini wanatakiwa wajue Azam FC ni timu changa sana na kwa sasa
tunapiga hatua kubwa, lakini hii haitufanyi tuvimbe vichwa kwani bado tuna
deni. “Hivyo nafikiri inabidi tufanye kitu kikubwa zaidi kuweza kusogea na wao
mashabiki waendelee kutupa sapoti, bado ligi ipo, FA ipo tutajitahidi kuweza
kuchukua makombe yote hayo. “Mchezo ulikuwa mgumu, ulikuwa mzuri dakika 45 za
kipindi cha kwanza, tuliweza kuikabili presha ya ugenini na hatukuweza kuruhusu
bao, kipindi cha pili naona wenzetu walirudi na nguvu zaidi, tulizuia wakapata
mabao kutokana na labda makosa yetu ya kiuchezaji wakaweza kushinda,” alisema.
Mao alisema ni hatua kubwa wamefikia mpaka sasa hadi
kutolewa hasa kutokana na ukubwa wa wapinzani wao waliokuwa wakipambana nao.
“Unajua mpira ni mchezo wa makosa na katika mpira
unajifunza kila siku iwe unacheza mechi au unafanya mazoezi, ukiiangalia
Esperance ipo kwenye nafasi za juu Afrika (nafasi ya tatu), ni timu nzuri ni
timu bora, sisi kufika hapa na namna tulivyocheza na hatua kubwa sana tumefika,
lakini ni changamoto kwetu inabidi tuchukue kitu ambacho kitatusaidia
kufanikiwa katika mashindano yanayokuja mbele,” alisema.
Azam FC iliyopanda Ligi Kuu miaka minane iliyopita,
msimu huu ilikuwa ikishiriki kwa mara ya nne michuano ya Afrika hadi inafika
raundi hiyo ilifanikiwa kuwatoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya
mabao 7-3.
0 comments:
Post a Comment