Beki wa pembeni wa Azam FC Shomary Salum kapombe
ameanza matibabu nchini Afrika kusini akiwa chini ya uongozi wa timu ya Bidvest
ya nchini humo.
Msemaji wa Azam FC Jaffery Iddy Maganga amesema,
Kapombe amepokelewa na uongozi wa Klabu ya Bidvest ambao walitengeneza ukaribu
baina na timu hiyo bila kujali wala kuangalia kuwa walicheza na timu hiyo na
kuitoa katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.
Maganga amesema, Kapombe amefikishwa hospitali ya
Morningside Mediclinic na ameanza kupatiwa matibabu baada ya kugundulika na
ugonjwa wa Pulmonary Embolism ambao ni donge la damu kuziba mishipa ya damu
katika mapafu.
Maganga amesema, Kapombe atakaa kwa takribani wiki
mbili kwa ajili ya matibabu na baada ya kurejea nchini atakaa kwa takribani
miezi miwili ili kujiangalia afya yake kabla ya kurudi mchezoni.
Maganga amesema, kukosekana kwa Kapombe kumekuwa ni
pigo kwa upande wao kwani ni mchezaji ambaye alikuwa sababu ya timu kutumia
mfumo ambao walikuwa wakiutumia na ndio maana katika mchezo dhidi ya Esperance
ya Tunisia mwishoni mwa wiki iliyopita waliamua kubadili mfumo wa uchezaji.
Kapombe aliyekosa mechi mbili zilizopita za Azam FC
dhidi ya Toto Africans na Ndanda, alianza kuumwa na kifua wakati kikosi hicho
kikijiandaa kuvaana na Toto jijini Mwanza kabla ya kukimbizwa hospitalini.
Kapombe ataukosa mchezo wa marudiano dhidi ya Esperance
utakaopigwa Aprili 19 nchini Tunisia pamoja na mechi zote za Ligi kuu ya soka
Tanzania bara zilizobakia za Azam FC msimu huu na huenda akarejea uwanjani
kwenye kipindi cha maandalizi ya msimu ujao.


0 comments:
Post a Comment