Waziri Mkuu Mheshimiwa KASSIM MAJALIWA ameongeza kuwa pamoja na hatua hizo, Mpango Maalum wa Ushiriki wa Watanzania katika miradi mikubwa ya uwekezaji ulioandaliwa nao utatekelezwa.
Mpango huo unalenga kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali za nchi yao kwa njia ya ubia kwenye miradi ya uwekezaji, ajira na kandarasi mbalimbali zitakazotolewa na kampuni kubwa kwa Wazawa.
Mheshimiwa MAJALIWA alikuwa akiwasilisha Bungeni Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na makairio ya maparo na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka 2016/2017.
Kuhusu ajira amesema jitihada za serikali za kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali na urasimishaji wa sekta isiyo rasmi zitaendelezwa ili kupunguza zaidi kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.
Kwa upande wa wakulima amesema katika kuongeza ya uzalishaji wa mazao amesema serikali itaendelea kutoa ruzuku za pembejeo zikiwemo mbolea na mbegu bora zenye ukinzani na ustahimilivu wa magonjwa na ukame; na zenye uwezo mkubwa wa kutoa mavuno.
HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHE. KASSIM M. MAJALIWA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA
SERIKALI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI
YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA 2016/2017
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa
Hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu
na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili
Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2015/2016 na
Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2016/2017. Vilevile, naliomba Bunge lako
Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya
Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2016/2017.
2.
Mheshimiwa Spika, huu ni Mkutano wa Bunge wa kujadili Bajeti ya Serikali
baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2015. Hivyo naomba nitumie
fursa hii kuwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuwa na imani na Chama Cha
Mapinduzi na hivyo kukiwezesha kushinda na kukipa tena ridhaa ya kuunda
Serikali na kuiongoza Nchi yetu. Aidha, kwa njia ya pekee napenda kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano. Pia, nampongeza
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile,
nampongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Balozi Seif
Ali Iddi kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Nawapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kuteuliwa kushika nyadhifa
hizo muhimu.
Nawahakikishia
wananchi wote kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itawatumikia kwa nguvu zake zote
bila kujali itikadi zao za kisiasa.
3.
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba
kutumia fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Waziri
Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uteuzi huo kuungwa mkono
na Waheshimiwa Wabunge kwa asilimia 73. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais
na Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kwamba sitawaangusha.
4.
Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia
Ackson Mwansasu (Mb.), kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Pia, nawapongeza
Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa Wawakilishi wa Wananchi katika
Bunge hili. Jukumu lililo mbele yetu sote ni kuwatumikia wananchi waliotuchagua
ili kuwaletea maendeleo.
5.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2015/2016, Nchi yetu imekumbwa na majanga
mbalimbali yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali. Nitumie fursa hii
kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie wale walioumia kupona haraka na kurejea katika
shughuli za ujenzi wa Taifa. Ninawapa pole wote waliofiwa na ndugu, jamaa na
marafiki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema
peponi. Amina!
6.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru
Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kupitia kwa kina Makadirio ya Matumizi
ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za
Serikali za Mitaa. Kipekee, nitumie nafasi hii, kuwashukuru Wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya
Bunge ya
Katiba na
Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji;
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Hasna
Sudi Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na
Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini. Kamati hizo
zimetoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, naomba niwapongeze Wenyeviti na Makamu
wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia makadirio ya
sekta zote. Maoni na ushauri wao umesaidia sana katika kuboresha Makadirio ya
bajeti ya Serikali.
7.
Mheshimiwa Spika, makadirio ya
bajeti ninayowasilisha leo ni mwendelezo
wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015. Ilani
hiyo, imeainisha ahadi ambazo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itazitekeleza
katika miaka mitano ijayo. Aidha,
makadirio ya Bajeti yamezingatia ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa wakati wa Kampeni na
katika uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja, tarehe 20 Novemba 2015. Serikali ya
Awamu ya Tano imedhamiria kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kujenga Taifa imara
kiuchumi na maendeleo ya watu katika Kanda ya Afrika Mashariki na Barani Afrika
kwa ujumla.
MWELEKEO WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
8.
Mheshimiwa Spika, kabla ya
kuwasilisha mapitio ya kazi za Serikali kwa mwaka 2015/2016 na mwelekeo kwa
mwaka 2016/2017, niruhusu kupitia Bunge lako Tukufu niwakumbushe Watanzania
wote kuhusu dhima ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye falsafa ya “Hapa Kazi Tu”.
Sote tunatambua kwamba ili Tanzania ifikie Nchi yenye Uchumi wa Kipato cha Kati
ifikapo mwaka 2025 ni sharti kila mmoja wetu afanye kazi kwa bidii, maarifa na
ubunifu wa hali ya juu.
9.
Mheshimiwa Spika, ili yawepo mapinduzi ya kweli ya kuelekea kwenye
uchumi wa kati tunaodhamiria ni lazima tuimarishe uwajibikaji na maadili kwa
Viongozi, Watendaji na kwa kila Mtanzania. Sote tumeshuhudia hatua
zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya Watumishi wasio waadilifu wanaotumia fedha
za umma au madaraka yao vibaya na kukwamisha utekelezaji wa mipango ya
maendeleo tunayojiwekea. Hatutaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa
viwanda kama tutaendelea kulea uzembe, ubadhirifu, uvivu na kukwepa wajibu
wetu. Ndiyo maana, tumeanza kwa nguvu kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na
matumizi sahihi ya fedha za umma ili zielekezwe kwenye shughuli zenye manufaa
kwa Watanzania walio wengi na siyo vinginevyo.
10.
Mheshimiwa Spika, pamoja na
kuimarisha ufanisi na tija ndani ya utumishi wa umma, tumebaini kuwa changamoto
ya utamaduni usioridhisha wa ufanyaji kazi upo katika sekta zote, za umma na
binafsi. Wizi, uzembe, udhuru wa kila siku na huduma mbaya kwa wateja ni baadhi
ya malalamiko ya wawekezaji hapa nchini. Tabia hizi ni lazima zikemewe kama
tunataka nguvu kazi yetu ipate ajira katika zama hizi tunazohamasisha mapinduzi
ya viwanda. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu katika jamii kusimamia maadili
na makuzi ya vijana ili nguvu kazi hii iweze kutumika ipasavyo kuchangia ukuaji
wa uchumi.
11.
Mheshimiwa Spika, imani yetu ni
kwamba tumeanza vizuri kwenye suala la kuongeza uwajibikaji na maadili ndani ya
Serikali. Serikali itaendelea kuwawajibisha wale wote ambao hawataendana na
Falsafa na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano. Jambo la msingi ni kwamba
tutachukua hatua kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Niwahakikishie Watanzania kwamba hakuna mtumishi au mwananchi atakayeonewa au
kunyanyaswa katika zoezi hili. Hivyo, wale wote ambao wako safi waendelee
kutimiza wajibu wao bila woga. Kazi zifanyike kwa weledi na kwa kasi bila urasimu.
12.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inachukua hatua za kuongeza mapato na kuziba mianya ya ukwepaji kodi ambazo zimeonesha
manufaa makubwa. Mathalan, hatua tulizochukua za kubana mianya ya ukwepaji kodi
zimeimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kutoka wastani wa Shilingi Bilioni
870 mwezi Novemba, 2015 na kufikia Shilingi trilioni 1.3 mwezi Machi, 2016.
Tunaendelea kuimarisha
ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki, kuziba mianya
ya ukwepaji kodi na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kila anayetakiwa kulipa
kodi alipe na fedha hizo zitumike kutekeleza mipango ya maendeleo. Vilevile,
Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima na kusimamia
matumizi sahihi ya rasilimali. Fedha zinazopatikana zitaelekezwa kwenye miradi ya kipaumbele yenye
kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.
13.
Mheshimiwa Spika, uchumi wa
viwanda utajengwa na Sekta Binafsi. Kazi ya Serikali ni kuhakikisha kunakuwa na
mazingira rafiki kwa sekta hiyo kuwekeza. Hivyo, Serikali itaendelea kubuni na
kutekeleza miradi itakayowezesha sekta binafsi kuwekeza bila vikwazo. Miradi
hiyo ni pamoja na miundombinu muhimu ya uchukuzi na usafirishaji, umeme,
mawasiliano na maji kwa ajili ya uzalishaji na biashara. Napenda kutumia fursa
hii kuwahakikishia wawekezaji wote nchini na wengine wanaokusudia kuwekeza
kwamba Serikali imedhamiria kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi. Hatua
zote zinazochukuliwa sasa ni za kuhakikisha kwamba sekta binafsi inawekewa
mazingira wezeshi na yenye ushindani wa haki ili iweze kuimarika.
SIASA
14.
Mheshimiwa
Spika, mtangamano
wa kisiasa ni nguzo muhimu katika kujenga Nchi yenye maendeleo makubwa na ya
uhakika. Mtangamano wa kisiasa unajumuisha siasa safi, za kiustaarabu na zinazoheshimu
mawazo ya kila mmoja wetu. Siasa za aina hii ndiyo chimbuko la mustakabali wa
amani na utulivu wa Taifa letu tangu tujipatie uhuru. Ni jambo la faraja na
kufurahisha kwamba, pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kujaa tashwishwi na
ushindani mkubwa, Taifa letu limeendelea kuwa na amani, utulivu na mshikamano
mkubwa Kitaifa kiasi cha kupigiwa mfano Barani Afrika na dunia kwa ujumla. Hali hii inaonesha kukua na kuimarika kwa demokrasia
ya vyama vingi vya siasa nchini ambapo hadi sasa vipo vyama 22 vyenye usajili
wa kudumu na vyama vitatu vyenye usajili wa muda na vingine sita vimewasilisha
maombi ya usajili wa muda.
15.
Mheshimiwa
Spika, Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015 umesaidia kupima namna demokrasia inavyozidi kukua na
kupanuka kwani kwa mara ya kwanza kulikuwa na mwitikio mkubwa wa kujitokeza kwa
wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na wananchi wengi kujiandikisha kupiga
kura. Vyama nane vilisimamisha wagombea wa nafasi ya Urais na vyama 22 Ubunge
na Udiwani. Idadi ya wapiga kura walioandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
ilikuwa 23,161,440, sawa na asilimia 96.9 ya makadirio. Idadi ya watu waliopiga
kura ilikuwa ni 15,596,110, sawa na asilimia 67.3 ya waliojiandikisha. Hii ni
idadi kubwa ya wapiga kura ikilinganishwa na chaguzi zote zilizopita. Hivyo,
naomba nichukue fursa hii kuipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kuanzia
katika uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura, ugawaji wa majimbo mapya ya
uchaguzi, kutoa elimu kwa umma, uandikishaji wa wapiga kura na kuusimamia kwa
umakini mkubwa uchaguzi wenyewe na kutangaza matokeo. Tume ilifanya kazi yake
kwa uhuru na kwa weledi mkubwa. Niwapongeze viongozi na wananchi wote
walioshiriki uchaguzi huo kwa amani na utulivu.
16.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na
kazi nzuri iliyofanywa na Tume na wananchi kuitikia wito wa kujiandikisha na
kupiga kura, bado kulikuwa na idadi kubwa ya waliojiandikisha lakini hawakupiga
kura. Naiagiza Tume ya Uchaguzi kufanya tathmini ya kina kubaini sababu
zilizofanya wapiga kura zaidi ya Milioni saba waliojiandikisha kupiga kura
kutoitumia haki yao ya Kikatiba. Hii
itasaidia kuboresha chaguzi zijazo kwani wananchi wana wajibu wa kutumia haki
yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka. Aidha, tathmini itasaidia kubaini
iwapo kuna vikwazo vinavyowazuia baadhi ya watu kupiga kura ili kwa pamoja
tuviondoe. Ndani ya Bunge hili tupo wabunge wa Vyama mbalimbali lakini kwa
lengo moja tu la kuwawakilisha wananchi wetu na kuishauri Serikali ili ipange
mipango mizuri itakayoharakisha maendeleo yao. Niseme tu kwamba sasa Uchaguzi
Mkuu umekwisha na Serikali zetu zipo madarakani kwa mujibu wa Katiba. Hivyo,
tuienzi falsafa ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya “Hapa Kazi Tu!” kwa kuchapa kazi na tusitoe nafasi
kwa tofauti zetu za kisiasa na kiitikadi kuwa kisingizio cha kukwamisha shughuli za maendeleo ya Nchi yetu.
17.
Mheshimiwa
Spika, dhamira ya
Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendelea kukuza Demokrasia ili kuwezesha ushiriki
mpana wa wananchi katika kufanya maamuzi ya maendeleo yao katika Taifa letu
chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hivyo, Serikali inaandaa mapendekezo
ya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama
za Uchaguzi ya Mwaka 2010 kwa lengo la kuondoa changamoto zilizojitokeza katika
utekelezaji wake na kuzifanya ziendane na hali halisi ya siasa nchini na kwa
mtazamo wa baadaye.
UCHUMI
Ukuaji wa Uchumi
18.
Mheshimiwa
Spika, malengo
yetu ya kufikia Nchi ya kipato cha kati na kufanyika mapinduzi makubwa ya
viwanda yanategemea sana utulivu wa uchumi. Kwa ujumla, ukuaji wa uchumi
umekuwa wa kuridhisha kwani mwaka 2015, uchumi ulikua kwa asilimia 7.1
ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2014. Sekta zilizochangia katika
ukuaji huo ni pamoja na Ujenzi, Mawasiliano, Fedha, Uchukuzi na Nishati. Pamoja
na ukuaji huu mzuri wa ujumla, Sekta ya Kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia
66.3 ya Watanzania wote wanaofanya kazi ilikua kwa asilimia 3.4 tu mwaka 2014.
Ukuaji huo mdogo unamaanisha kwamba juhudi za ziada na kubwa zinahitajika ili
sekta hii muhimu iweze kutoa mchango mkubwa zaidi wakati tunapotekeleza Mpango
wa Pili wa Maendeleo. Historia ya maendeleo ya uchumi inatuambia kwamba, Sekta
ya Kilimo ina mchango mkubwa na muhimu kwenye mapinduzi ya viwanda. Hivyo
hatuna uchaguzi mwingine bali kuelekeza nguvu zaidi kwenye sekta hii ya kilimo.
19.
Mheshimiwa
Spika, kwa ujumla tutahitajika kuongeza ufanisi na tija
katika sekta zote za uzalishaji na utoaji huduma ili malengo yetu ya ukuaji
uchumi yafikiwe katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Katika kufikia azma
hiyo, tutatekeleza sera madhubuti za fedha na kodi zitakazowezesha mfumuko wa
bei kuendelea kushuka na kubaki katika tarakimu moja kama ilivyo sasa.
Mathalan, mfumuko wa bei mwaka 2015 ulifikia wastani wa asilimia 5.6
ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.1 kwa mwaka 2014. Mwelekeo huu wa
utulivu wa uchumi utavutia mitaji mingi kutoka Sekta Binafsi kuwekeza kwenye
sekta za kipaumbele, kuwezesha ongezeko la ajira na kupanua wigo wa ulipaji
kodi.
Mazingira Wezeshi ya Uwekezaji
20.
Mheshimiwa
Spika, awali
nilidokeza kwamba, uwekezaji kwenye viwanda na sekta nyingine za kiuchumi
utafanywa na sekta binafsi na jukumu la msingi la Serikali ni kuweka mazingira
wezeshi. Kwa msingi huo, Serikali ya Awamu ya Tano itachukua hatua madhubuti na
za haraka kupunguza muda, gharama na idadi ya taratibu za kiutawala ambazo
Wafanyabiashara na Wawekezaji hulazimika kuzifuata ili kufanya biashara nchini.
Taratibu zinapokuwa ngumu na ndefu husababisha ongezeko la gharama za kufanya
biashara na hivyo kuwakatisha tamaa wawekezaji. Taarifa ya Wepesi wa Kufanya
Biashara duniani inayotolewa na Benki ya Dunia iliyochapishwa mwezi Novemba,
2015 inaonesha kwamba katika mwaka 2016, Tanzania imeshika nafasi ya 139 kati
ya Nchi 189 Duniani. Hali hii haikubaliki kabisa. Hivyo, eneo hilo litafanyiwa
kazi haraka ili kuharakisha mapinduzi ya viwanda.
21.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali itaimarisha utekelezaji wa Mpangokazi wa Kuboresha
Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini. Utekelezaji huo utazingatia
maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa mkutano na Wafanyabiashara
uliofanyika mwezi Desemba, 2015. Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine,
Mheshima Rais aliwataka watendaji kupunguza urasimu usio wa lazima kwa
wafanyabiashara na wawekezaji. Nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya kuyatumia mabaraza ya biashara ya Mikoa na Wilaya ili
kuhakikisha juhudi shirikishi za uboreshaji wa mazingira ya biashara
zinatekelezwa hadi ngazi ya chini. Pia, nawataka watumishi wa umma kuepuka
kuwachelewesha kwa uzembe au makusudi wawekezaji wenye nia njema ya kuwekeza
nchini ili kuleta maendeleo endelevu kwa wakati. Mtumishi yeyote wa umma
atakayeendeleza urasimu usio wa lazima hatavumiliwa.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
22.
Mheshimiwa
Spika, azma ya
kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda ni jambo
la msingi. Hivyo, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na
kuwadhamini wajasiriamali wenye miradi inayokidhi vigezo kwenye Taasisi za
Fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu. Pamoja na hatua hizo, Mpango
Maalum wa Ushiriki wa Watanzania katika miradi mikubwa ya uwekezaji
ulioandaliwa utatekelezwa. Mpango huo unalenga kuhakikisha kwamba Watanzania
wananufaika zaidi na rasilimali za Nchi yao kwa njia ya ubia kwenye miradi ya
uwekezaji, ajira na kandarasi mbalimbali zitakazotolewa na kampuni kubwa kwa
Wazawa. Wananchi pia wataendelea kuwezeshwa kupitia mikopo yenye masharti nafuu
kwa vikundi mbalimbali vya kiuchumi vya wakulima, wafugaji, wavuvi,
wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wa madini inayotolewa na Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii. Serikali imeruhusu Mifuko hiyo kutoa mikopo nafuu kwa wanachama wa
vikundi vinavyojiunga na Mifuko kunufaika na mafao ya afya na pensheni
yanayotolewa na mifuko husika.
23.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imehamasisha uanzishaji na usajili wa Vikundi vya Kiuchumi kama vile Vyama vya
Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOs) na Benki za Jamii Vijijini (VICOBA).
Serikali pia imesimamia uanzishwaji wa Taasisi Mwavuli ya kusimamia VICOBA
inayoitwa VICOBA FETA. Takwimu zilizotolewa mwezi Februari 2016 na Taasisi hiyo
zinaonesha kuwa kuna vikundi 100,000 vya VICOBA vyenye wanachama Milioni 2.2 na
mtaji wa Shilingi trilioni 1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya
wanachama wa VICOBA ni wanawake.
24.
Mheshimiwa
Spika, moja ya
ahadi muhimu iliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 ni kutenga
Shilingi Milioni 50 kwa kila kijiji nchini zitakazotumika kwa utaratibu wa
mzunguko (Revolving Fund). Lengo ni kuwawezesha wananchi kuanzisha na
kuendeleza shughuli za uzalishaji kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa na
vikundi vingine vya kiuchumi. Uhakiki wa Vyama vya Ushirika wa Kuweka na Kukopa
uliofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika unaonesha kwamba idadi ya SACCOs
zinazokidhi vigezo vya usajili nchini imepungua kutoka 5,559 mwaka 2013 hadi
3,856 mwaka 2015. Kati ya hizo, SACCOs 2,125 sawa na asilimia 55 zipo Vijijini
na 1,740 zipo Mijini. Ni dhahiri kwamba Mpango wa Shilingi Milioni 50 kwa kila
Kijiji unahitaji maandalizi mazuri, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uanzishaji
na usajili wa SACCOs na vikundi vya kiuchumi
vinavyokidhi vigezo, ili kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa
zinawafikia walengwa na zinatumika kwa shughuli zilizokusudiwa. Ninaziagiza
Halmashauri zote nchini ziweke orodha sahihi ya Vyama vya Ushirika wa Kuweka na
Kukopa vilivyosajiliwa kwa kila Kijiji na kuchukua hatua za kuwezesha
uanzishaji na usajili wa SACCOs zinazokidhi vigezo kulingana na shughuli za
uzalishaji katika Halmashauri husika.
25.
Mheshimiwa
Spika, napenda
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, maandalizi ya utekelezaji wa Mpango
huo yanaendelea vizuri katika kila Halmashauri. Tutatumia uzoefu uliopatikana
kwenye utekelezaji wa mifuko mingine, ukiwemo Mfuko wa Kuwawezesha Wananchi na
Kuongeza Fursa za Ajira maarufu kama “Mabilioni ya JK”, ili changamoto
zilizojitokeza zitusaidie kuboresha Mpango huu mpya.
26.
Mheshimiwa
Spika, Serikali itaendelea kuziwezesha Kaya maskini ili ziweze
kupata mahitaji yao ya msingi na kuongeza kipato kupitia Awamu ya Tatu ya Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III). Tangu utekelezaji wa Mpango huo uanze kaya
maskini 1,099,289 zimepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 164.8 kama ruzuku katika
Halmashauri 159 za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Aidha, kupitia Mpango wa Ajira za Muda kwa
Kaya Maskini, iliandaliwa miradi 1,880 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 42.6
kutoka Halmashauri 40 za Tanzania Bara na Zanzibar. Katika mwaka 2016/2017,
Serikali itaendelea kufanya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini katika
maeneo ambayo hayakufikiwa.
Ajira
27.
Mheshimiwa Spika, Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 imeweka umuhimu katika kupanua fursa za ajira kwa kutumia rasilimali
zilizopo nchini ili kila mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie kwenye uchumi na
kupata kipato halali. Msisitizo huo wa Ilani ya Uchaguzi unatokana na ukweli
kwamba Utafiti wa Hali ya Ajira Nchini wa mwaka 2014 umeonesha kuwa kiwango cha
ukosefu wa ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi asilimia 10.3
mwaka 2014. Aidha, ukosefu wa ajira kwa
vijana umepungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014.
Kiwango hicho bado ni kikubwa na tunaweza kufanya vizuri zaidi. Jitihada za
Serikali za kuvutia uwekezaji
kwenye sekta mbalimbali na urasimishaji wa sekta isiyo rasmi zitaendelezwa ili
kupunguza zaidi kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.
28.
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto
zinazosababisha ukosefu wa ajira ni vijana wetu kutojengewa maarifa na ujuzi wa
kuajiriwa na kuajirika. Hivyo, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi Nchini (2015/2016 – 2019/2020). Programu hiyo
inalenga kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi kutoka asilimia
3 ya sasa hadi asilimia 12 inayotakiwa kuendesha uchumi wa viwanda. Vilevile,
kupunguza idadi ya watu wenye kiwango cha ujuzi wa chini kutoka asilimia 75 ya
sasa hadi 54. Utekelezaji wa Programu hiyo utasaidia kupunguza pengo la
mahitaji ya rasilimali watu nchini ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya haraka ya
uchumi wa viwanda. Serikali itahakikisha
kuwa suala la ukuzaji ajira linazingatiwa katika mipango yote ya uwekezaji pamoja na mipango ya maendeleo ya kisekta
katika ngazi zote. Hivyo, nazielekeza Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za
Serikali, Taasisi za Umma, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha
ukuzaji wa ajira unakuwa ni agenda ya
msingi ya kudumu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Tayari
Mheshimiwa Rais amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kwamba vijana ambao ndiyo
nguvu kazi kuu ya Taifa wanatumia fursa itakayopatikana kutokana na Shilingi Milioni
50 zitakazotolewa kwa kila kijiji kuanzisha miradi ya maendeleo ya kujipatia
kipato.
VIJANA
29.
Mheshimiwa Spika, vijana ni hazina na rasimali watu muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonesha kuwa idadi ya vijana wenye umri kati ya
miaka 15 na 35 ni takribani Milioni 16.2, sawa na asilimia 35.1 ya Watanzania
wote. Aidha, Utafiti wa Nguvu Kazi wa mwaka 2014 unaonesha kuwa vijana ni
asilimia 59 ya nguvu kazi ya Taifa. Matokeo ya tafiti hizo yanathibitisha kuwa
kuna umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya vijana na ushirikishwaji wao katika
mipango ya maendeleo. Katika
mwaka 2014/2015 hadi 2015/2016, Serikali imewawezesha vijana kiuchumi kupitia
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Hadi kufikia mwezi Machi 2016, mikopo yenye
thamani ya Shilingi Bilioni 1.6 imetolewa na Mfuko huo kwa vikundi vya vijana
284 na mafunzo yametolewa kwa viongozi wa vikundi 2,552 kutoka Halmashauri 59.
Vilevile, Serikali imetenga maeneo maalum ya shughuli za kiuchumi na huduma kwa
vijana katika Halmashauri 30 nchini.
30.
Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha dhana ya ushiriki na
ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za maendeleo, Bunge la Kumi lilitunga
Sheria Na. 12 ya Baraza la Taifa la Vijana ya mwaka 2015. Napenda kuliarifu
Bunge lako Tukufu kwamba sasa Kanuni
za utekelezaji wa Sheria hiyo zimekamilika. Hivyo, katika
mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kuratibu uanzishwaji wa Baraza la Vijana
la Taifa na kuhimiza uanzishaji na uimarishaji wa SACCOs za vijana katika Halmashauri zote nchini na kuziwezesha
kupitia
Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana na Taasisi za fedha.
31.
Mheshimiwa
Spika, Maadili na Makuzi ya Vijana ni suala linalopewa
kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano. Hatuwezi kujenga uchumi imara wa
viwanda, kuongeza fursa za ajira na kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali za
umma kama jamii yetu, hasa vijana hawatajitambua kwa kuwa waadilifu, wazalendo
na wachapakazi. Serikali, itaendelea kuratibu utekelezaji wa Programu ya Stadi za Maisha na Programu ya
kujitolea kwa vijana ili kukuza maadili, uzalendo na kujenga utamaduni wa
kuchapa kazi kwa vijana.
WATU WENYE ULEMAVU
32.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
inathamini mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo na kwamba wana
haki sawa ya kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Katika
kuzingatia azma hiyo, Serikali inatekeleza Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9
ya mwaka 2010, ambayo, imewezesha kuundwa kwa Baraza la Kitaifa la Ushauri la
Watu wenye Ulemavu ili kuongeza ushiriki wa Watu wenye Ulemavu katika maamuzi.
Aidha, Kamati za kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu zimeundwa katika
ngazi za Mikoa, Halmashauri, Kata, Mitaa na Vijiji kwa ajili ya kuratibu
masuala muhimu kwa watu wenye ulemavu katika maeneo husika.
33.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na
juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuwalinda na kuwapatia fursa, kumekuwepo
na matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu hususan watu
wenye ualbino. Ukatili huo umesababisha watu wenye ualbino kupoteza maisha na
wengine kupata aina nyingine ya ulemavu wa kudumu. Hali hiyo haikubaliki na
haivumiliki katika jamii ya Watanzania. Serikali inafanya jitihada kubwa
kukomesha vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwakamata wote wanaojihusisha na
vitendo hivyo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Aidha, itaendelea kutoa
elimu kwa jamii ili kubadili mitazamo na imani potofu kuhusu watu wenye ualbino
na ulemavu kwa ujumla. Napenda kusisitiza kwamba watu wenye ulemavu wana haki
ya kuthaminiwa utu wao na kulindwa dhidi ya ukatili na aina yoyote ya ubaguzi.
34.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali itaviboresha Vyuo vya Ufundi na Marekebisho (Vocational and Rehabilitation Training
Centres) vya watu wenye ulemavu nchini ili kutoa ujuzi unaoendana na
mahitaji yao katika soko la ajira. Serikali pia, itaandaa walimu wa elimu
maalum na kutoa vifaa saidizi kwa walimu na wanafunzi wenye ulemavu mashuleni.
Kwa sasa Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwahabarisha watu wenye usikivu
hafifu kwa kuanzisha tafsiri za matangazo kwa njia za alama. Hivyo, wamiliki
wote wa Televisheni wametakiwa kuajiri wakalimani.
KAZI NA HIFADHI YA JAMII
Kazi
35.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kusimamia utekelezaji wa sheria na viwango vya kazi kwa kufanya kaguzi ili
kuhakikisha waajiri wanazingatia mikataba ya ajira, masaa ya kazi, likizo na
ujira kwa lengo la kupunguza migogoro na kuongeza tija. Hadi kufikia Machi
2016, jumla ya kaguzi za kazi 1,305
zilifanyika na migomo 23 katika sekta za usafirishaji, viwanda, ujenzi na
kwenye migodi ilisuluhishwa na kupatiwa ufumbuzi. Aidha, kaguzi za kawaida
4,670 na kaguzi maalum 17,005 zilizojumuisha kaguzi za umeme, mitambo na vipimo
vya mazingira ili kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa na afya njema na usalama
mahala pa kazi zilifanyika.
36.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya
Kuratibu Ajira ya Wageni Na. 1 ya Mwaka 2015 ilitungwa na kumpa Kamishna wa
Kazi mamlaka ya kutoa vibali vya kazi nchini ili kukuza fursa za ajira kwa
Watanzania. Tangu Sheria hiyo ianze kutumika rasmi tarehe 15 Septemba 2015 hadi
mwezi Machi 2016, mapato yaliyopatikana kutokana na vibali vya kazi
vilivyotolewa nchini ni Shilingi Bilioni 21.01, sawa na asilimia 356 ya lengo
la makadirio ya Shilingi Bilioni 7.5 kwa mwaka 2015/2016. Serikali pia imefanya
kaguzi katika Makampuni na Taasisi 400 zenye jumla ya wageni 3,939 na kubaini
wageni 779 hawana vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini. Kati ya hao, wageni
29 waliondolewa nchini, 317 walipewa hati maalum (special pass), 77
walifikishwa mahakamani na 356 walielekezwa kukamilisha taratibu za ukaazi wao
kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Sheria ya Uhamiaji. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itafanya kaguzi za kazi
56,200 katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini na itaanzisha Bodi mbili za
kupanga kima cha chini cha mishahara kwa sekta ya umma na binafsi.
Hifadhi ya Jamii
37.
Mheshimwa Spika, Sekta ya Hifadhi
ya Jamii ina mchango mkubwa katika uchumi wa Nchi yetu. Kwa kutambua hilo,
Serikali imeifanyia tathmini mifuko sita ambayo ni GEPF, LAPF, NHIF, NSSF, PPF
na PSPF kwa lengo la kupima uendelevu wake. Tathmini hiyo imebainisha kuwa
mifuko hiyo bado ni endelevu na rasilimali zake zimefikia Shilingi trilioni
8.8. Aidha, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
imetoa miongozo ya kupunguza gharama za uendeshaji wa Mifuko hiyo itakayoanza
kutumika Julai, 2016. Serikali imekamilisha uhakiki wa madeni ya PSPF
yaliyokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko huo mwaka 1999 yenye thamani ya
Shilingi trilioni 2.9. Hadi sasa,
Serikali imelipa sehemu ya deni la PSPF kiasi cha
Shilingi Bilioni 180 ili kuhakikisha kwamba mafao ya wastaafu wa Mfuko huo
yanalipwa kwa wakati. Serikali pia itaendelea kulipa deni la Shilingi Bilioni
840.4 linalotokana na miradi ya Serikali iliyogharamiwa na mifuko ya GEPF,
LAPF, NHIF, NSSF na PPF.
38.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa
asilimia 6.5 ya Watanzania wote ndiyo wanaofikiwa na huduma ya Hifadhi ya
Jamii. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya
Maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kuongeza wigo wa wanaofikiwa na
huduma hiyo. Hii ni pamoja na kujumuisha makundi mengine katika jamii kama vile
wazee na watu wenye ulemavu ambapo rasimu ya andiko la mpango wa pensheni kwa
makundi hayo imekamilika. Hatua inayoendelea hivi sasa ni ushirikishwaji wa
wadau na taasisi zitakazohusika katika kutekeleza mpango huo. Aidha, Serikali
itaendelea kuhamasisha uchangiaji wa hiari na kusimamia uendeshaji wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii ili kuhakikisha inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya utawala
bora na kuchangia zaidi katika ukuzaji
wa uchumi bila kuathiri mifuko.
SEKTA ZA UZALISHAJI MALI
Uzalishaji wa Mazao na Akiba ya Chakula
39.
Mheshimiwa Spika, sekta ya kilimo
inayojumuisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu
ndio tegemeo la maisha ya watanzania walio wengi. Hata hivyo, ukuaji wa sekta
hiyo umekuwa siyo wa kuridhisha kutokana na matumizi ya teknolojia isiyoendana
na wakati na pia kutegemea majaliwa ya Mwenyezi Mungu ya hali ya hewa. Pamoja
na changamoto hizo, hali
ya upatikanaji wa chakula imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi
hapa nchini. Katika msimu wa 2014/2015, wakulima walizalisha Tani Milioni 15.5 za mazao ya chakula. Kutokana
na uzalishaji huo, Nchi imejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120 kwani
mahitaji ya chakula kwa mwaka 2015/2016 ni Tani Milioni 12.95. Hali hii pia
imetuwezesha katika msimu huu kutoa chakula cha msaada na cha bei ya chini
katika maeneo yaliyopata upungufu wa chakula. Aidha, Wakala wa Taifa wa Hifadhi
ya Chakula - NFRA iliuza
jumla ya Tani 239,322 ya akiba yake kwa wafanyabiashara nchini ili kukabiliana
na mfumuko wa bei za vyakula hususan unga wa sembe katika masoko ya mijini. Hadi
kufikia mwezi Aprili 2016, NFRA ilikuwa na akiba ya Tani 67,895 za chakula.
Katika mwaka 2016/2017, Serikali itanunua Tani 100,000 kwa ajili ya hifadhi ya
chakula.
40.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imedhamiria kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kupanua na kuimarisha
kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha zaidi kwa ajili ya usalama wa chakula,
kuuza ziada nje na kupata malighafi za viwandani. Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2015, inalenga kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka Hekta 461,326 za sasa
hadi Hekta Milioni moja ifikapo mwaka 2020. Ili kufikia lengo hilo, Serikali
itashirikiana na sekta binafsi katika kujenga, kukarabati na kuboresha
miundombinu ya umwagiliaji nchini.
Ruzuku za Pembejeo
41.
Mheshimiwa
Spika, ongezeko la tija katika uzalishaji wa mazao unategemea
kwa kiasi kikubwa matumizi ya pembejeo zikiwemo mbolea na mbegu bora zenye ukinzani na ustahimilivu
wa magonjwa na ukame; na zenye uwezo mkubwa wa kutoa mavuno. Katika
msimu wa 2015/2016, Serikali imetoa vocha milioni tatu za pembejeo za kilimo
zikiwemo Tani 10,271 za mbegu bora za mahindi na mpunga na Tani 99,923 za
mbolea ambazo zimesambazwa katika mikoa 24 ya Tanzania Bara na kunufaisha kaya
999,926. Ninawaagiza Wakuu wa Mikoa hiyo kuhakikisha kuwa pembejeo hizo
zinawafikia walengwa kwa wakati na zinatumika kama ilivyotarajiwa na kuwachukulia
hatua wale wote watakaohujumu mpango huu.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
42.
Mheshimiwa Spika, mwezi Agosti 2015, Serikali ilizindua Benki ya Maendeleo
ya Kilimo ili kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu. Benki hiyo
inatoa mikopo ya muda mfupi na muda mrefu kwa riba kati ya asilimia saba na 12
imeanza na mtaji wa Shilingi Bilioni 60. Mikopo inayotolewa na Benki hiyo
inalenga kusaidia kugharamia uandaaji wa mashamba, ununuzi wa pembejeo za
kilimo, usindikaji wa mazao pamoja na hifadhi ya mazao. Serikali itaendelea
kuiongezea mtaji Benki hiyo ili ikopeshe wakulima wengi zaidi hasa kupitia
vikundi vya wanawake na vijana vinavyojihusisha na kilimo. Benki hiyo
itasimamia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 25 kwa ajili ya kudhamini mabenki
ya biashara ili yaongeze ukopeshaji kwenye miradi ya miundombinu ya masoko
na kuendeleza ubunifu kwenye miradi ya
maendeleo vijijini chini ya Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji wa
Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF). Vilevile, Benki hiyo itakuwa Wakala
wa Serikali wa kusimamia fedha za ruzuku ya pembejeo.
Miundombinu ya Masoko
43.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
itaimarisha utekelezaji wa Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani
na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) inayotekelezwa katika mikoa yote ya
Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Programu hiyo inasaidia kuboresha
miundombinu ya masoko, zikiwemo barabara na maghala ya kuhifadhia mazao;
kuwawezesha wananchi waishio vijijini kuongeza thamani ya mazao ya kilimo;
kuwajengea wananchi uwezo wa kuyafikia masoko na kupanua wigo wa huduma za
kifedha vijijini.
44.
Mheshimiwa
Spika, chini ya
Programu hiyo katika mwaka 2015/2016, Serikali imekarabati barabara za vijijini
zenye urefu wa kilomita 180 kwa kiwango cha changarawe zikiwemo kilomita 63.6
za Zanzibar. Aidha, imejenga maghala matano yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 1,000
za mazao kila moja na kuvijengea uwezo wa kufikia masoko vikundi 780, vikiwemo
vikundi 101 vya Tanzania Zanzibar. Vilevile, imezijengea uwezo Asasi ndogo za
Kifedha, zikiwemo SACCOs 291 na Benki tisa za Wananchi ili ziweze kutoa huduma
endelevu za kifedha. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea na uboreshaji
wa miundombinu ya masoko katika Halmashauri 38 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za
Zanzibar. Aidha, itaendelea kuwajengea wazalishaji wadogo uwezo wa kuhifadhi na
kusindika mazao, mbinu za kufikia masoko na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Mifugo
45.
Mheshimiwa Spika, tunayo fursa ya
kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya mifugo kama tutawekeza kwenye viwanda
vya kusindika nyama ili kuongeza thamani na kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali
kutokana na mifugo iliyopo nchini. Hali
ilivyo sasa siyo nzuri kwani tunauza mifugo mingi nje ya nchi ikilinganishwa na
nyama. Mathalan, katika mwaka 2015/2016 hadi kufikia mwezi Machi 2016, ng’ombe
milioni 1.5, mbuzi milioni 1.2 na kondoo 253,243 wenye thamani ya Shilingi Bilioni 976.5 waliuzwa nje ya nchi. Hii ina
maana kuwa mazao kama ngozi, kwato na damu za wanyama hao, ambazo zingeweza
kutumika kuzalisha bidhaa nyingine za viwandani, yamekwenda nje badala ya
kutumika hapa nchini. Tunaweza kabisa kugeuza hali hii haraka kwa kuhamasisha
ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani mifugo.
Nashauri wawekezaji binafsi kwenye sekta ya mifugo kuchangamkia fursa ya
kufufua viwanda vya nyama vilivyopo na
kujenga vingine vipya ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, ni lazima tuanze
kubadili fikra za wafugaji wetu ili ufugaji uwe na tija kwa kuwa na idadi ndogo
ya mifugo yenye ubora wa kisasa na inayoendana na uwezo wa eneo la malisho. Serikali
itaweka msisitizo wa kipekee katika kuboresha kosaafu za mifugo ili
kuzalisha mifugo yenye tija kwa kusambaza ng’ombe bora kwa ajili ya uzalishaji
wa maziwa na nyama kutoka katika mashamba ya kuzalisha mifugo na kuimarisha
uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo. Vilevile, juhudi za
kudhibiti magonjwa ya mifugo yasiyokuwa na mipaka na yenye athari kubwa katika
uchumi wa Taifa zitaongezwa. Serikali itaendelea kufanya tathmini ya uendeshaji
wa ranchi za Taifa zilizobinafsishwa ili kuhakikisha kwamba wale waliopewa
vitalu vya mifugo wanavitumia kwa mujibu wa mikataba ya mauzo au vinginevyo
kuwanyang’anya na kuwapa wengine wenye uwezo.
Viwanda
46.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuweka nguvu kubwa katika sekta ya
viwanda ili kufikia lengo la kuwa Nchi ya uchumi wa viwanda. Azma hiyo
imesisitizwa sana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015. Ili kufikia uchumi wa viwanda, kuanzia mwaka 2016/2017 jitihada kubwa
itawekwa katika kutenga na kuendeleza maeneo maalum ya viwanda; kuweka
miundombinu muhimu ya nishati, usafirishaji, maji na maghala. Aidha, tutaweka
utaratibu endelevu wa upatikanaji mitaji
na teknolojia ikiwemo kuanzisha dirisha maalum katika Benki ya Maendeleo TIB
na Benki ya Maendeleo ya Kilimo.
Serikali pia itapitia mifumo ya kodi, tozo na taratibu mbalimbali kwa lengo la
kuzipunguza na kuondoa urasimu ili kupunguza gharama za uzalishaji wa ndani na
kuwezesha bidhaa zetu kushindana katika soko la ndani na kimataifa. Aidha,
Serikali itaifanyia mapitio ya Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996 na Sheria yake
ya mwaka 1997 ili kuendana na wakati.
Masoko
47.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa
masoko ya uhakika unategemea mambo makuu manne. Ubora wa bidhaa au mazao;
uhakika wa kupatikana kwa mazao au bidhaa wakati wote; unafuu wa bei dhidi ya washindani wengine
katika soko; na ufungashaji na ujenzi wa jina la bidhaa (branding). Hivyo, ni
lazima mlolongo wote wa uzalishaji, uongezaji thamani na usafirishaji uwe mzuri
kuwezesha uwepo wa soko la uhakika. Mtiririko huo katika mnyororo wa thamani wa
bidhaa zenye uhakika wa soko ndio msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Tano na
msingi wa kuhamasisha mapinduzi ya viwanda kwa lengo la kuongeza thamani bidhaa
zetu kabla ya kuuzwa. Msukumo mkubwa
utawekwa katika uendelezaji na upatikanaji wa soko la ndani na nje kwa bidhaa
zinazozalishwa nchini, hususan katika masoko ya upendeleo ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na masoko mengine ya kimkakati ya Kikanda na Kimataifa. Vivyo hivyo,
uondoaji wa vikwazo vya kibiashara pamoja na kusimamia viwango na ubora wa
bidhaa za ndani na nje ya nchi utaendelezwa.
48.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi
cha mwaka 2015/2016, Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania zimekamilisha
mkataba mwingine wa kutumia Soko la Marekani
bila ushuru chini ya Mpango wa AGOA, kwa kipindi kingine cha miaka 10 kuanzia tarehe 30 Septemba, 2015
hadi 30 Septemba, 2025. Ni muhimu sana kutumia fursa hii mpya ya AGOA kufanya
biashara na Marekani katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Vyama vya
wafanyabiashara ni lazima viwaandae wanachama wao kupata taarifa kamili kuhusu
bidhaa zinazohitajika na ubora unaotakiwa.
Aidha, Serikali itasimamia uzalishaji wa bidhaa bora kulingana na ubora
unaotakiwa na masoko.
Madini
49.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
inatambua umuhimu wa uchimbaji madini mdogo kama kichocheo cha kuongeza ajira
na kukuza kipato cha wachimbaji wadogo wa madini na wananchi wanaozunguka
maeneo husika ya madini. Aidha, uchimbaji mdogo wa madini unachangia kukuza
uchumi na kuondoa umaskini. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imechukua
hatua mbalimbali za kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwatengea maeneo,
kuwapatia ruzuku na kutoa mafunzo ya kuwawezesha kutekeleza kazi zao kwa
ufanisi na tija. Katika mwaka 2015/2016, Serikali ilitenga Hekta 7,731 kwa
ajili ya uchimbaji madini mdogo katika maeneo ya Nyamongo (Tarime) na Muhintiri
(Singida). Aidha, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya TIB imetoa mikopo ya
masharti nafuu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.2 kwa ajili ya kukuza mitaji
ya wachimbaji wadogo. Pia mafunzo yametolewa kwa wachimbaji wadogo 1,520. Mikoo
hiyo pia inaweza kutolewa kupitia benki ya TIB Corporate.
50.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali itatenga zaidi maeneo tengefu kwa ajili ya uchimbaji
madini mdogo na kuongeza kiasi cha ruzuku inayotolewa kwa Wachimbaji Wadogo.
Serikali imetenga Shilingi Milioni 900 kwa ajili ya ruzuku na Benki ya Dunia
imeridhia kutoa Dola za Marekani Milioni Tatu kuchangia kwenye ruzuku hiyo. Aidha,
Serikali itaimarisha usimamizi katika biashara ya madini ya Tanzanite na kutoa
mwongozo mpya wa namna ya kuendesha uchimbaji madini mdogo kwa tija. Mafunzo kuhusu namna ya kufanya utafiti wa
awali wa madini na uchenjuaji bora wa madini yataendelezwa ili kazi za
wachimbaji madini wadogo zifanyike kwa ufanisi na tija.
Utalii
51.
Mheshimiwa
Spika, Sekta ya Utalii ni moja ya
sekta muhimu ambazo fursa zilizopo zikitumika vizuri zitasaidia sana kukuza
ajira na kupunguza umaskini. Juhudi
kubwa ambazo zimefanywa na Serikali katika kuboresha huduma na miundombinu ya
kitalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii zimeiwezesha Sekta ya Utalii
kuchangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 25 ya mapato yanayotokana na mauzo ya
nje mwaka 2015. Aidha, mwezi Julai 2015 Serikali ilizindua Kampeni Maalum
ya Kukuza Utalii wa Ndani ili kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vilivyopo
katika Hifadhi zetu. Kampeni hiyo imeongeza idadi ya watalii wa ndani kutoka
watalii 115,913 mwezi Septemba 2014 hadi 148,406 Septemba 2015. Mafanikio hayo
yanadhihirisha kwamba Sekta ya Utalii ikiboreshwa ina fursa nyingi za kuchangia Pato la
Taifa na kuongeza ajira na kipato cha wananchi. Hata hivyo, unahitajika uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya
utalii ikiwemo hoteli, usafirishaji na rasilimali watu imara na yenye weledi
katika kuwahudumia watalii wa ndani na nje.
52.
Mheshimiwa
Spika, tunahitaji kufanya vizuri zaidi
kwa kupanua vyanzo vya utalii na kuhakikisha fedha nyingi wanazotumia watalii
kuja Tanzania zinalipwa hapa nchini badala ya utaratibu wa sasa wa malipo hayo
kufanyika Nchi wanazotoka watalii. Tunahitaji pia kupanua na kuvutia utalii wa
kihistoria na malikale kama vile miji mikongwe ya Kilwa, Mikindani, Bagamoyo na
Mjimkongwe Zanzibar na vivutio vingine visivyo na mfano Barani Afrika; kuliko kuegemea tu utalii wa
wanyamapori na maliasili nyingine. Katika
mwaka 2016/2017, Serikali itaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Utalii
Nchini pamoja na kuendelea kutangaza vivutio maafufu kama Mlima Kilimanjaro,
Mbuga za Serengeti na Mapango ya Olduvai.
Kudhibiti Ujangili
53.
Mheshimiwa
Spika, Nchi yetu inakabiliwa na tatizo la ujangili hasa wa
tembo, faru na biashara haramu ya nyara za Serikali. Katika kukabiliana na
tatizo hilo, Serikali ilizindua Mkakati wa Kupambana na Ujangili na Biashara
haramu ya Nyara za Serikali ulioanza kutekelezwa mwaka 2015, kwa kuchukua hatua
mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja na kutumia vifaa na teknolojia ya kisasa kama
vile “Geographical Information System -
GIS” na “Global Positioning System - GPS”;
kuimarisha mfumo wa mawasiliano ya radio kutoka mfumo wa analogia kwenda
kidigitali; na kuanza kutekeleza Mpango wa Kikanda wa kukusanya taarifa za
kiintelijensia zinazoongoza doria katika kukamata watuhumiwa na wahalifu.
54.
Mheshimiwa
Spika, Serikali itaimarisha
utekelezaji wa Mkakati huo hususan kwa kuzingatia ukubwa wa changamoto ya
vitendo vya uwindaji haramu vinavyofanywa na majangili kwa kushirikiana na
baadhi ya watumishi wa Idara ya Wanyamapori wasio waaminifu na baadhi ya
wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka mapori. Serikali ya Awamu ya Tano
itahakikisha kwamba ujangili huu unakomeshwa haraka. Nichukue fursa hii
kuziomba jamii zinazozunguka hifadhi zetu kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
Serikali katika vita hii.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
55.
Mheshimiwa
Spika, ili azma yetu ya kufanya mapinduzi ya viwanda ifanikiwe,
inahitajika ardhi iliyopimwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Changamoto
tuliyonayo hivi sasa ni kwamba sehemu kubwa ya ardhi yetu haijapimwa na
kupatiwa hatimiliki. Hivyo, tumeanza kuchukua hatua za haraka zitakazowezesha
kupatikana kwa ardhi ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Wakuu wa Mikoa
na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa walishaagizwa kutenga maeneo ya
viwanda na biashara katika Mipango Miji. Napenda kutumia fursa hii kuitaka
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutopitisha maombi yoyote ya
Mipango Miji yasiyokuwa na maeneo ya Viwanda na Biashara. Nimefarijika kuona
kwamba chini ya Mpango wa Maeneo Huru ya Biashara, baadhi ya mikoa imeshatenga
ardhi ambayo itaweza kuanza kutumika mara moja kutekeleza Mpango huo kwa
kuwekewa miundombinu muhimu na kukamilisha upimaji. Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji zishirikiane
kufanya uhakiki wa haraka wa maeneo hayo ili wawekezaji watakaoonesha nia ya
kuwekeza kwenye viwanda wapatiwe maeneo yenye hatimiliki kwa haraka.
56.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
inatambua kwamba kuna migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo nchini. Migogoro hiyo, wakati mwingine imesababisha
uharibifu wa mali, majeruhi na mauaji ya binadamu na mifugo. Njia muafaka ya
kudhibiti migogoro hiyo ni kupima kila kipande cha ardhi, kukimilikisha kwa
mtumiaji kwa kumpatia hatimiliki na kusimamia matumizi yake. Kwa kutambua hilo,
mwezi Februari 2016, Serikali ilizindua Programu ya Kuwezesha Umilikishaji
Ardhi (Land Tenure Support Programme) ambayo imeanza kutekelezwa kwa majaribio
katika Wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi mkoani Morogoro. Programu hiyo
imelenga kuongeza kasi ya kupima ardhi na kutoa hakimiliki za kimila ambazo
zinaweza kutumika kama dhamana kwa wakulima na wafugaji kupata mikopo;
kupunguza au kuondoa migogoro ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi;
na kuhifadhi kumbukumbu za ardhi kwa matumizi sahihi ya rasilimali hiyo. Programu hiyo itatekelezwa kwa muda wa miaka
mitatu kwa gharama Dola za Marekani Milioni 15.2. Baada ya majaribio hayo, na
mafanikio kuonekana katika wilaya hizo, Programu itatekelezwa katika wilaya
zote nchini. Ninawaagiza viongozi wa Mkoa wa Morogoro na wilaya zinazohusika,
kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Programu hiyo kwani matokeo yake ni ya
muhimu sana kwenye mustakabali wa upimaji na matumizi endelevu ya ardhi yetu.
57.
Mheshimiwa
Spika, mwaka
2015, Serikali iliwaomba Waheshimiwa Wabunge kuainisha na kuwasilisha
Serikalini migogoro ya ardhi iliyopo kwenye majimbo yao. Napenda kutumia fursa
hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge walioitikia wito huo. Mchango wao
katika kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016, umewezesha jumla ya migogoro
1,130 ya ardhi kupokelewa Serikalini kutoka katika Halmashauri zote nchini.
Uchambuzi wa migogoro hiyo unaendelea ambapo taarifa za awali zinaonesha kwamba
migogoro mingi iliyopo ni kati ya wakulima na wafugaji, uvamizi wa mashamba na
viwanja, migogoro kati ya Mamlaka za Hifadhi za Taifa na wananchi na kati ya
wawekezaji na wananchi.
58.
Mheshimiwa
Spika, kutokana
na hali hiyo, tayari Serikali imechukua hatua kali dhidi ya maafisa ardhi
waliokiuka sheria na taratibu za usimamizi wa ardhi nchini. Hii ni pamoja na
kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Kwa mfano, hatua kali zimechukuliwa
katika Halmashauri za Majiji ya Mwanza na Arusha, Manispaa za Bukoba na Kahama
na kutengua madaraka kwa afisa ardhi mteule wa Manispaa ya Temeke. Ninaendelea kuwaomba Waheshimiwa Wabunge
kushirikiana na Halmashauri zao hususan Maafisa Ardhi na kutumia Dawati Maalum
la Kuratibu Migogoro ya Ardhi lililoanzishwa katika kila Halmashauri nchini ili
kuendelea kubaini migogoro iliyopo na kuitafutia ufumbuzi.
59.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali itaifanyia mapitio Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka
1995 ili kuweka vipengele muhimu vya kudhibiti migogoro baina ya watumiaji wa
ardhi na kuunda na kuzipa nguvu zaidi Ofisi za Ardhi za Kanda
zitakazosaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kupima na kupanga matumizi ya ardhi
na kutoa hati karibu zaidi na wananchi.
Aidha, Serikali itapitia upya Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi
ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 ili kuzifanyia marekebisho muhimu kuendana na
wakati.
Barabara
60.
Mheshimiwa Spika, miundombinu imara ni msingi muhimu wa maendeleo ya sekta
nyingine zote, ikiwemo Sekta ya Viwanda na Biashara. Katika miaka ya hivi
karibuni tumeshuhudia uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara nchini.
Mathalan katika mwaka 2015/2016, Serikali
ililenga kujenga kilometa
523 za barabara kuu kwa kiwango cha lami. Hadi kufikia mwezi Machi, 2016, jumla
ya kilometa 414.3 za barabara zilikuwa zimekamilishwa kwa kiwango cha lami,
sawa na asilimia 79 ya lengo lililowekwa. Aidha, jumla ya kilometa 82.4 za
barabara kuu zilikarabatiwa kwa kiwango cha lami, ikiwa ni sawa na asilimia 73
ya lengo la kilometa 113. Kwa upande wa barabara za
mikoa, jumla ya kilometa 52.19 zilijengwa kwa kiwango cha lami, sawa na
asilimia 68 ya lengo la kilometa 77 na jumla ya kilometa 676 za barabara za
mikoa zilifanyiwa ukarabati kwa kiwango cha changarawe, sawa na asilimia 54 ya
lengo la kilometa 1,252. Ujenzi wa madaraja makubwa 11 uliendelea ambapo Daraja
la Kigamboni limekamilika na kufunguliwa rasmi.
Reli
61.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatekeleza Mradi
wa Uboreshaji wa Miundombinu na Huduma za Reli ya Kati, lengo likiwa ni
kuboresha reli iliyopo kwa kutandika reli mpya na nzito zaidi; kuimarisha
matuta, mifereji na tabaka la kokoto. Aidha, tunaendelea na utekelezaji wa makubaliano baina ya Serikali
yetu na Serikali za Rwanda na Burundi kuhusu ujenzi wa reli ya Dar es Salaam –
Isaka – Keza - Kigali (Km. 1,464); na Keza – Musongati (Km. 197) kwa kiwango
cha Standard Gauge. Mkakati wa ndani ni pamoja na kujenga reli ya Standard Gauge
kuanzia Dar es Salaam –Kigoma yenye matawi mawili ya Kaliua-Mpanda-Karema na
…..(Haijamalizika NB Nasubiri HANSARD.
Bandari
62.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2015/2016, Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha
ufanisi wa bandari zetu kwa kuanzia na Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango
kuu la biashara katika Afrika Mashariki na Kati na kufuatiwa na Bandari za
Mtwara na Tanga. Tumeanza kwa kuondoa watumishi wote wasio waaminifu ambao
wanachangia kupoteza mapato ya Serikali yanayohitajika sana katika kutoa huduma
muhimu kwa wananchi wetu. Vilevile, tumefanya kazi kubwa ya kuimarisha mifumo
ya ukusanyaji mapato kwa kuhakikisha kwamba
malipo yote yanafanyika benki na kuoanisha mifumo ya Mamlaka ya Bandari
Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Niwahakikishie wananchi na wafanyabiashara kuwa Serikali itaendelea
kuboresha huduma katika bandari zetu na hususan Bandari ya Dar es Salaam kwa
kupunguza idadi ya siku za kutoa mizigo bandarini li tufikie siku mbili au
chini ya siku hizo. Aidha, tutaziondoa kero zote zilizoainishwa na Mawakala wa
Forodha nilipokutana nao tarehe 21 Machi, 2016 Jijini Dar es Salaam. Vilevile,
Serikali itaziba mianya yote ya upotevu wa mapato bandarini na wale wote
watakaobainika kushiriki kwenye wizi wa aina yoyote wataondolewa na kuchukuliwa
hatua za kisheria.
Mawasiliano
63.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inaendelea kukamilisha mradi wa ujenzi wa Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano
nchini ikiwemo ujenzi wa Kituo Mahiri cha Kutunzia Kumbukumbu katika Jiji la Dar es Salaam. Aidha, Serikali inaendelea na
ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini ambapo hadi sasa tumefanikisha
ujenzi wa kilometa 18,000 kati ya kilometa 20,000 za miundombinu ya mkongo
katika wilaya zote nchini. Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa
miundombinu ya mawasiliano katika vijiji 4,000 visivyokuwa na mawasiliano,
kuunganisha Ofisi zote za Wakuu wa Wilaya, Hospitali za Wilaya, Mahakama, Vituo
vya Polisi vya Wilaya, Ofisi za Posta na kuziwesha shule 431 kupata huduma ya
intaneti bila malipo.
Nishati
(a)Umeme
64.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwezesha
upatikanaji wa umeme wa uhakika, unaokidhi mahitaji na wenye gharama nafuu ili
kusukuma mapinduzi ya viwanda kwa kasi zaidi. Ili kutekeleza azma hiyo, katika
mwaka 2015/2016, Serikali imeongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme kutoka
Megawati (MW) 1,226.24 mwaka 2015 hadi kufikia MW 1,516.24 mwezi Januari 2016,
sawa na ongezeko la Asilimia 24.
Ongezeko hilo limetokana na uamuzi sahihi wa Serikali wa kutekeleza mradi
mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi pamoja
na mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi-I wenye uwezo wa kuzalisha MW 150. Mradi huo baadaye utapanuliwa na kuweza
kufikia MW 335 ifikapo mwaka 2017/2018. Sambamba na hatua hiyo, tarehe 16 Machi
2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo kingine cha Kinyerezi-II
cha kufua umeme kutokana na gesi asilia ambao utakapokamilika utazalisha MW
240. Lengo la Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kuongeza uwezo
wa uzalishaji umeme hadi kufikia MW 4,915 na hivyo, kuwezesha asilimia 60 ya
watanzania kupata umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2020 na kutekeleza ipasavyo
azma ya kuongeza uwekezaji mkubwa kwenye viwanda.
65.
Mheshimiwa
Spika, katika
kipindi cha mwaka 2015/2016, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea
kusambaza na kuunganisha umeme kwa wananchi waishio vijijini.
Katika
kipindi hicho, idadi ya wananchi waliopata umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya
Pili ni 71,724 katika vijiji 1,669. Aidha, hadi mwezi Januari, 2016 Serikali
imekamilisha ujenzi wa kilometa 12,193 za njia za msongo wa kati na kilometa
1,830 za msongo mdogo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya
Usambazaji wa Umeme Vijijini. Vilevile, umeme umefikishwa kwenye Makao Makuu ya
Wilaya mpya 12 za Buhigwe, Busega, Chemba, Itilima, Kakonko, Kalambo, Kyerwa,
Mkalama, Mlele, Nyasa, Nanyumbu na Uvinza. Utekelezaji wa miradi hiyo umeongeza
kiwango cha wananchi wanaopata huduma ya umeme kufikia asilimia 40.
66.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kutekeleza
Mradi wa Kinyerezi-II pamoja na
kuimarisha na kujenga njia za usafirishaji umeme katika Gridi ya Taifa
za Msongo mkubwa wa kiloVolts 400 kutoka Iringa kupitia Dodoma na Singida hadi
Shinyanga na kutoka Dar-es-Salaam kupitia Chalinze na Tanga hadi Arusha pamoja
na mradi wa kiloVolts 220 kutoka Makambako hadi Songea. Aidha, Serikali
itakamilisha Awamu ya Pili ya mradi wa usambazaji umeme vijijini na kuanza
utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya miradi ya REA.
(b) Gesi Asilia na Mafuta
67.
Mheshimiwa
Spika, baada ya ugunduzi mkubwa wa Gesi Asilia nchini, mikakati
ya Serikali inayoendelea ni kubuni miradi mbalimbali hasa ile itakayoendeshwa
na wafanyabiashara wazawa ili rasilimali hiyo iweze kuwanufaisha Watanzania na
kuwawezesha kumiliki uchumi wa Taifa lao. Serikali imetenga eneo la ardhi huko
Likongo Mkoani Lindi kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kuchakata Gesi Asilia
ikiwa ni sehemu ya kutekeleza azma hiyo ya kuwawezesha wazawa. Serikali itaanza
utekelezaji wa mradi huo katika mwaka 2016/2017.
68.
Mheshimiwa
Spika, katika
kuhakikisha kwamba Nchi inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta kwa
ushindani na gharama nafuu, Serikali imeanzisha Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa
Pamoja yaani Petroleum Bulk Procurement
Agency, ulioanza kazi rasmi mwezi Januari, 2016. Utaratibu huo utaiwezesha
Serikali kusimamia vizuri udhibiti wa uagizaji wa mafuta nchini na kuwawezesha
Wananchi kuwa na uhakika wa kupata mafuta bora yenye viwango vinavyokubalika
kimataifa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo na kijamii.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
69.
Mheshimiwa
Spika, kwa
kutambua umuhimu wa elimu kama nyenzo imara ya maendeleo ya kiuchumi na
kijamii, Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kuchukua hatua madhubuti za
kuboresha na kuimarisha elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu. Hatua zinazochukuliwa zinalenga
kuhakikisha kwamba elimu ya Tanzania ni
ya viwango vya ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha vijana wetu kukabiliana na
changamoto za maisha kwa kujiari wenyewe na kumudu ushindani katika soko la
ajira la ndani, kikanda na kimataifa. Aidha, hatua hizo zitatuwezesha kuwa na
rasilimali watu yenye weledi wa kutosha kujenga uchumi wa viwanda nchini. Moja
ya hatua kubwa iliyochukuliwa na Serikali ni utekelezaji wa ahadi ya utoaji wa
elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne kwa shule za umma
kuanzia mwezi Januari 2016. Ahadi hiyo ilitolewa na mgombea Urais kupitia CCM
wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2015 ambaye kwa
sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, ni matakwa ya
Kifungu cha 52(a) cha Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 ambacho
kinasisitiza kwamba Serikali itaandaa mfumo, muundo na taratibu nyumbufu za
kutoa elimu ya awali na elimumsingi bila malipo ili kila Mtanzania apate fursa
sawa ya kupata elimu.
70.
Mheshimiwa
Spika, naamini kabisa kuwa hatua hiyo nzuri iliyochukuliwa na
Serikali ya Awamu ya Tano, itawapunguzia wazazi na walezi hasa wananchi maskini
mzigo wa kugharamia elimu ya vijana wao. Kupitia Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka
2015, Serikali imefuta michango ya
maji, umeme, ulinzi, mitihani na ada iliyokuwa inachangishwa shuleni kwa idhini
ya Kamati na Bodi za Shule. Hata hivyo,
yapo majukumu yanayohusu mahitaji ya msingi ya mtoto ambayo yataendelea
kutekelezwa na wazazi na walezi kama ilivyokuwa inafanyika awali. Majukumu hayo
ni pamoja na kumnunulia mtoto sare za
shule na michezo, madaftari, kalamu na chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa kwa
utaratibu utakaowekwa na wazazi na walezi wenyewe. Maeneo mengine ni kulipia
nauli ya kwenda na kurudi shule mwanafunzi na mahitaji mengine kama vile
kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi binafsi. Vilevile, mzazi au mlezi ana
wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto wake.
71.
Mheshimiwa
Spika, baada ya kuanza utekelezaji wa mpango wa elimu bila
malipo, kumejitokeza changamoto kadhaa. Baadhi ya changamoto hizo ni uelewa wa
jamii juu ya umuhimu wa kuweka utaratibu muafaka wa kutoa chakula cha mchana
kwa wanafunzi wa kutwa na uendeshaji wa mabweni ambayo wazazi na walezi au
jamii walikuwa wanachangia fedha za chakula. Changamoto nyingine ni pamoja na
upungufu wa miundombinu kama madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu na
vyoo. Napenda kuwahakikishia wananchi kwamba Serikali inaendelea kuzifanyia
kazi changamoto hizo na jitihada kubwa zimewekwa katika kuielimisha jamii na
wadau mbalimbali kuhusu mpango mzima wa utoaji elimu bila malipo.
72.
Mheshimiwa
Spika, tunayo
changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati baada ya kuanza kuandikisha watoto shule
bila malipo. Hili ni jambo kubwa na tulishatoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu
wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha kuwa kila Halmashauri inatumia rasilimali
zake kutengeneza madawati kwa kila shule. Nitumie nafasi hii kuwashukuru wadau
walioanza kuchangia madawati katika maeneo mbalimbali na ninawasihi wengine
waendelee kuunga mkono jitihada hizi za Serikali. Kuanzia leo hii, nawaagiza
Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi waliokamata mbao ndani ya Halmashauri zao
kuzitumia kutengenezea madawati na siyo kuzipiga mnada. Natumia nafasi hii
kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Watendaji wa Bunge kwa Mkakati wa kubana
matumizi uliowezesha kupata Shilingi Bilioni sita zitakazotumika kutengeneza
madawati. SUMA JKT na Magereza wameanza kazi ya kutengeneza madawati hayo.
Tunatarajia kupata madawati 80,000 ambayo tutawagawia Wabunge wa Majimbo yote
na kwa wastani kila Jimbo litaweza kupata madawati 300.
73.
Mheshimiwa
Spika, napenda
nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika juhudi
za kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu elimu bila malipo. Aidha, nawaomba wote kwa ujumla wetu
kushirikiana katika kuwaelimisha wananchi kuhusu mpango huu na wajibu wa kila
mmoja wetu katika kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapata fursa za kupata elimu
bora. Tukifanya hivyo, tutaweza kufikia lengo letu la kuwa Nchi yenye uchumi wa
kipato cha kati kwa haraka zaidi.
74.
Mheshimiwa
Spika, elimu ya
ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ni nguzo muhimu ya kuwapatia ujuzi na
kuwajengea uwezo na uzoefu wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari.
Uzoefu wa Nchi za Asia zilizowekeza katika elimu ya ufundi na ufundi stadi
unaonesha kwamba maendeleo ya haraka waliyoyapata na hususan kufikia uchumi wa
kati na wa viwanda umechangiwa sana na elimu ya ufundi. Kwa kutambua umuhimu huo,
Serikali itaelekeza nguvu zake katika kujenga na kuimarisha miundombinu ya
elimu ya ufundi na kuboresha mitaala ili iendane na mahitaji ya sasa ya uchumi
wa viwanda. Kwa kuanzia, Serikali imeridhia vyuo vya maendeleo ya wananchi
kuhamishiwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na kufanyiwa
ukarabati kwa ushirikiano na Sekta Binafsi ili viweze kutoa mafunzo ya ufundi.
Hatua hiyo itaharakisha kufikiwa kwa lengo la Serikali la kuwa na chuo cha
ufundi kwa kila Wilaya.
75.
Mheshimiwa
Spika, udahili katika
vyuo vya elimu ya juu umeongezeka kutoka wanafunzi 214,722 mwaka 2014 hadi
kufikia wanafunzi 220,531 mwaka 2015.
Aidha, hadi kufikia Februari 2016, idadi ya wanafunzi waliopewa mikopo
ya elimu ya juu ilifikia 122,886. Kiasi
cha fedha za mikopo kilichotolewa kwa wanafunzi hao ni Shilingi Bilioni 207.
Hata hivyo, hali ya urejeshaji wa mikopo iliyotolewa hairidhishi. Hivyo,
naiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kufuatilia urejeshaji wa mikopo hiyo
ili fedha hizo zitumike kuwakopesha wanafunzi wengine.
Afya
76.
Mheshimiwa
Spika,
uimarishaji wa huduma za afya nchini, kwa maana ya kinga na tiba ni muhimu
sana. Nguvukazi yenye afya njema hutoa mchango mkubwa kwenye uchumi
ikilinganishwa na nguvukazi dhaifu kiafya. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali
imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za kinga, uchunguzi na upatikanaji wa
dawa na vifaa-tiba katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maalum, Hospitali za
Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati. Aidha,
Serikali imetoa maelekezo kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kufungua na kuendesha
maduka ya dawa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufaa za
Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Wilaya ili kuhakikisha
kwamba dawa za kutosha zinapatikana wakati wote na kwa bei nafuu.
77.
Mheshimiwa
Spika, napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Bohari Kuu ya Dawa imefungua na inaendesha
maduka ya dawa yanayouza bidhaa zake kwa bei nafuu ndani ya maeneo ya Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, Sekou Toure (Mwanza), Mawenzi (Kilimanjaro) na Mount
Meru (Arusha). Pamoja na juhudi hizo za Serikali za kuimarisha huduma za afya
nchini, milango ipo wazi kwa sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi kuwekeza
katika sekta ya afya.
78.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma za Bima ya Afya ili kuongeza
na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya afya kwa watu wote. Idadi ya wanufaika
wa Bima ya Afya tangu kuanzishwa kwake ni 11,729,281, sawa na asilimia 27 ya
watanzania wote kulingana na Sensa ya mwaka 2012. Kati ya hao, wanufaika
8,390,550 wako katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na 3,338,755 ni
wanachama wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Hata hivyo, idadi ya wanufaika wa Bima bado ni ndogo,
hivyo naagiza viongozi wa Mifuko hiyo kushirikiana pamoja kutoa elimu na
kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na Mifuko hiyo. Serikali inaendelea
kuangalia uwezekano wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili Katibu Tawala wa Mkoa
aratibu maendeleo ya Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati.
Maji
79.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inaendelea kutekeleza
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma
ya maji safi, salama na ya kutosha. Hadi kufikia Desemba 2015, Serikali
imefikisha huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 72 katika maeneo ya
vijijini, asilimia 86 miji mikuu ya mikoa na asilimia 60 katika miji mikuu ya
wilaya na miji midogo. Mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa miradi ya
maji 1,143 kati ya miradi 1,855 ya maji mijini na vijijini ambayo imetekelezwa
chini ya Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Aidha,
huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na miji ya Bagamoyo na Kibaha
imeongezeka na kufikia asilimia 68, lengo likiwa kufikia asilimia 95 ifikapo
mwaka 2025. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itatekeleza Awamu ya Pili ya
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji pamoja na kukamilisha miradi 712 ambayo
haikutekelezwa katika Awamu ya Kwanza. Natoa wito kwa wananchi wote kutunza
vyanzo vya maji pamoja na miundombinu yake ili kuhakikisha upatikanaji endelevu
wa maji vijijini na mijini.
80.
Mheshimiwa
Spika, sote tunafahamu kwamba maji ni moja ya vigezo muhimu
katika kuanzisha na kuendeleza viwanda. Hivyo hatua zinazochukuliwa na Serikali
katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji nchini, pamoja na kuongeza
huduma ya maji safi na taka, ina lengo la kuongeza mchango wa Sekta ya Maji
katika Sekta ya Viwanda. Mathalan, ongezeko la maji kutokana na utekelezaji wa
miradi ya kuboresha miundombinu ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini umesaidia kupunguza
tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam. Serikali itahakikisha kuwa maeneo
yenye viwanda na yanayotegemewa kuwa na viwanda yanaunganishwa na miradi mikubwa
ya maji ili kuongeza kasi ya uzalishaji.
SHERIA, ULINZI NA USALAMA
Sheria
81.
Mheshimiwa
Spika, ni dhamira
ya Serikali kuona kwamba kero ya mlundikano wa mashauri Mahakamani inakuwa
historia na kwamba wananchi wanapata haki kwa wakati. Katika kufanikisha
dhamira hiyo, Serikali imeimarisha utendaji wa Mhimili wa Mahakama kwa kuongeza
rasilimali watu na fedha. Aidha, Serikali imeboresha na kuongeza ufanisi katika
upelelezi na uendeshaji wa mashauri kwa kutenganisha jukumu la upelelezi na
uendeshaji wa mashauri. Vilevile, uongozi wa Mahakama umejiwekea utaratibu wa
Majaji na Mahakimu kuwa na malengo ya idadi ya mashauri ambayo wanapaswa
kuyasikiliza kila mwaka.
82.
Mheshimiwa
Spika, katika
juhudi za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa majengo ya Mahakama na vitendea
kazi katika ngazi zote, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, ametekeleza ahadi yake aliyoitoa tarehe 4 Februari
2016 ya kutoa fedha zote za maendeleo za Mahakama kiasi cha Shilingi Bilioni
12.3 kwa mwaka 2015/2016. Hatua hiyo
imeiwezesha Mahakama kuendelea na ukarabati na ujenzi wa Mahakama katika ngazi
mbalimbali na pia ununuzi wa vitendea kazi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais
kwa uamuzi huo.
83.
Mheshimiwa
Spika, wakati
akihutubia Bunge lako Tukufu mwezi Novemba, 2015 Mheshimiwa Rais aliahidi kuwa
katika mwaka 2016/2017, Serikali itaanzisha Mahakama Maalum ya Ufisadi. Napenda
kuliarifu Bunge lako kwamba, Serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya
Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi mwezi Julai
2016. Aidha, Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki.
Ulinzi na Usalama
84.
Mheshimiwa
Spika, vyombo vya
ulinzi na usalama vimeendelea na jukumu la kulinda mipaka, raia na mali zao.
Kwa jumla, hali ya ulinzi na usalama wa Nchi yetu ipo shwari. Napenda kutumia
fursa hii kuvipongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kazi yao nzuri,
weledi na uzalendo wa hali ya juu katika kuhakikisha Taifa letu lina usalama wa
kutosha pia kuchangia usalama wa mataifa mengine duniani yenye migogoro ya
kisiasa. Mambo yote haya yanatokana na ukweli kwamba Serikali imekuwa
ikiviwezesha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuwa na uwezo wa kulinda mipaka
ya Nchi, raia na mali zao. Katika kujenga utayari wa Majeshi wakati wote,
askari wetu wameshiriki kwa ufanisi katika majukumu ya kimataifa ya kulinda
amani katika Nchi zenye migogoro duniani, hususan Darfur, Sudan, Lebanon na
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
85.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2015/2016, jumla ya vijana 27,463 walipatiwa mafunzo ya kujenga uzalendo,
ukakamavu, maadili mema, utaifa pamoja na stadi za kazi na za kimaisha. Kati
yao, vijana 7,517 ni wa kujitolea na 19,946 ni wa mujibu wa sheria. Ni jambo la
kutia moyo kwamba vijana 5,453 waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
wamenufaika na utaratibu wa kuajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama. Kati ya
hao, Vijana 3,521 wameajiriwa na JWTZ; Polisi 1,185; Usalama wa Taifa 106, Takukuru
vijana 24 na Jeshi la Zimamoto vijana 617.
Aidha,
Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kuishi kwa watumishi wa vyombo vya
ulinzi na usalama ambapo ujenzi wa nyumba 4,744 za makazi zimekamilishwa kati
ya nyumba 6,064 za awamu ya kwanza kwenye mradi wa nyumba 10,000 zinazotarajiwa
kujengwa Nchi nzima.
86.
Mheshimiwa
Spika, Serikali italiimarisha Jeshi letu kwa kulipatia mafunzo,
zana bora na za kisasa zaidi; kuboresha mazingira ya kufanyia kazi; na maslahi.
Aidha, itaimarisha uwezo wa Jeshi katika utafiti na kuendeleza teknolojia kwa
madhumuni ya kuongeza ubunifu katika kuzalisha bidhaa bora zaidi na huduma kwa
ajili ya matumizi ya jeshi na raia nchini na nje ya nchi.
Udhibiti wa Uhalifu Nchini
87.
Mheshimiwa
Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kulinda usalama wa raia na
mali zao na kudumisha amani na utulivu nchini. Katika kipindi cha Januari hadi
Desemba 2015, jumla ya makosa makubwa ya jinai 68,814 yaliripotiwa katika Vituo
vya Polisi kote nchini ikilinganishwa na makosa 70,153 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2014, sawa na
upungufu wa asilimia 1.9. Upungufu huo wa makosa umetokana na kuongezeka kwa
ushirikishwaji wa wananchi katika vita dhidi ya uhalifu na kuongezeka kwa
taarifa za kiintelijensia. Aidha, Jeshi limeimarisha doria za Nchi kavu na
majini pamoja na kufanya misako na operesheni maalum kwa ngazi ya Taifa, Mkoa,
Wilaya, Tarafa, Kata na Shehia. Katika mwaka 2016/2017, Jeshi la Polisi
litaendelea kutoa elimu ya Ulinzi Shirikishi kwa wananchi ili waweze kuongeza
ushirikiano na Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa jukumu la kupambana na
uhalifu.
MICHEZO
88.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya, kuongeza ajira, kujenga udugu na
mshikamano miongoni mwa jamii na mataifa mbalimbali duniani, Serikali itaendelea kuimarisha michezo
nchini ili wanamichezo wetu waweze kufanya vizuri katika medani za michezo
ndani na kimataifa.
Katika kufikia azma hiyo, mwaka 2016/2017, Serikali itakamilisha mapitio ya Sera ya Maendeleo ya
Michezo ya mwaka 1995 na kuendelea kutoa mafunzo ya michezo kwa walimu wa shule
za msingi na sekondari ili kuibua vipaji. Serikali pia itaendelea kusimamia
maendeleo ya michezo katika shule, vyuo, taasisi na vilabu. Lengo ni
kuhakikisha kuwa michezo inatoa fursa kwa vijana kupata ajira na kuendeleza
vipaji vyao.
HABARI
89.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatambua kwamba Sekta ya Habari ni nguzo muhimu
katika kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha umma. Kutokana na umuhimu huo,
Serikali imeendelea kusimamia Sekta ya Habari kikamilifu na kuhakikisha
vyombo vya habari vinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni,
Maadili na Weledi. Uhuru
wa vyombo vya habari ni mkubwa na wigo wa
ushiriki wa Sekta Binafsi umeongezeka sana. Hadi kufikia mwezi Machi,
2016 Serikali ilikuwa imesajili Vituo vya Televisheni 26, Vituo vya Redio 126
na Magazeti 833. Muhimu hapa ni matumizi mazuri ya kalamu na kuweka uzalendo wa
Nchi mbele.
90.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za
Habari kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa vyombo vya Habari. Aidha,
itaboresha Idara ya Habari- Maelezo ili itimize jukumu lake kama Msemaji Mkuu
na Mratibu wa Mawasiliano Serikalini. Vilevile, itaendelea kufuatilia kwa karibu maudhui ya vituo
vyote vya utangazaji kupitia mtambo maalum wa ufuatiliaji wa maudhui na
kuhakikisha vituo vya utangazaji vinakuwa na wakalimani wa lugha ya alama.
Napenda nitumie fursa hii kuvitaka vyombo ya habari nchini, kufanya kazi zake
kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizopo, mambo ambayo ni muhimu
sana katika tasnia ya habari kama wafanyavyo wenzao katika Nchi zote duniani
yaani uzingatiaji wa maadili katika tasnia ya habari. Aidha, niwaombe wamiliki
wa vyombo vya habari na wanahabari kutanguliza uzalendo wa Nchi yao mbele.
MASUALA MTAMBUKA
Lishe
91.
Mheshimiwa
Spika, lishe bora
ni nguzo muhimu katika kujenga Taifa lenye rasilimali watu wenye afya bora na
uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya kazi. Ukosefu wa lishe bora husababisha
utapiamlo ambao una madhara makubwa kiuchumi na kijamii kwa kaya, jamii na
Taifa kwa ujumla. Hali hiyo ikitokea ndani ya kipindi cha siku 1,000 kuanzia
ujauzito hadi miaka miwili ya ukuaji wa mtoto husababisha udumavu ambao madhara
yake hayawezi kurekebishwa katika maisha yake yote. Udumavu unaathiri mwili na
akili ya mtoto na hivyo hawezi kujifunza vizuri darasani na pia hupunguza uwezo
wake katika kuchangia maendeleo ya Taifa lake hapo baadaye.
92.
Mheshimiwa
Spika, athari
nyingine za utapiamlo ni pamoja na watoto kuugua mara kwa mara, hali
inayochangia ongezeko la gharama za matibabu kwa familia, jamii na Taifa; na
wazazi kutumia muda mwingi kuuguza watoto badala ya kufanya shughuli za kukuza
uchumi. Hali hiyo inatutaka sote tuwe mabalozi wa kuelimisha umma kuhusu
umuhimu wa lishe bora. Vilevile, ni muhimu kwa wajawazito kuhudhuria kliniki
ili kuchunguzwa afya zao na pia kupata ushauri wa kitaalam utakaowawezesha kupata watoto wenye afya njema. Wakina mama
waelimishwe kunyonyesha watoto wao kwa kipindi kisichopungua miezi sita
mfululizo na kuwapatia vyakula vyenye viini lishe vya kutosha baada ya hapo.
Masuala haya yanahitaji elimu zaidi kwa sababu vyakula hivyo vinapatikana
kwenye jamii na kaya zetu na siyo ghali kuvipata.
Vita Dhidi ya Rushwa
93.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kupambana na rushwa kwa kuchunguza
tuhuma za rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya vyombo vya sheria. Katika
mwaka 2015/2016, Serikali imeshughulikia tuhuma 3,911 ambapo uchunguzi wa
tuhuma 324 ulikamilika. Kati ya tuhuma hizo, majalada 252 yaliombewa kibali cha
Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo majalada 156 yalipata kibali cha kuwafikisha
watuhumiwa Mahakamani. Aidha, Majalada 329 yaliyotokana na taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yalichunguzwa. Majalada 19 yalikamilika
na kuombewa kibali kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo majalada 12 yalipata
kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani. Vilevile, majalada nane
yaliyohusu tuhuma za rushwa kubwa yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Kati
ya hayo, majalada mawili yamepata kibali na watuhumiwa wamefikishwa Mahakamani.
94.
Mheshimiwa
Spika, Miradi ya Maendeleo 284 yenye thamani ya Shilingi Bilioni
41.63 ilikaguliwa kupitia ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo katika Serikali za
Mitaa. Miradi 69 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 8.32 ilibainika kuwa na
kasoro ambapo miradi 10 wahusika walishauriwa namna ya kurekebisha kasoro
zilizojitokeza wakati miradi 59 uchunguzi wa kina umeanzishwa ili wahusika
wachukuliwe hatua. Aidha, ufuatiliaji maalum wa miradi ya afya inayofadhiliwa
na Benki ya Dunia unaendelea kufanyika ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa
kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na kasoro, ikiwemo kuanzisha uchunguzi wa
awali ambapo majalada 85 yamefunguliwa.
95.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
itaendelea kuchunguza tuhuma 3,444 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kukamilisha
uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa. Aidha, itawajengea uelewa wa masuala ya
rushwa makundi mbalimbali katika jamii na hususan Asasi za Kiraia, madhehebu ya
dini na wanahabari ili washiriki kikamilifu kuwaelimisha wananchi kuhusu
kudhibiti rushwa na kuendelea kufungua na kuimarisha klabu za wapinga rushwa
katika shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuendelea kujenga jamii
inayochukia rushwa.
Kudhibiti UKIMWI
96.
Mheshimiwa Spika, maambukizo mapya ya Virusi vya UKIMWI
yanaendelea kupungua kutoka
asilimia 5.7 mwaka 2008 hadi 5.1 kwa takwimu za 2011/2012. Vifo vitokanavyo na
UKIMWI navyo vimeendelea kupungua kutoka wastani wa vifo 79,338 mwaka 2012/2013
hadi vifo 50,219 mwaka 2014/2015. Maambukizi mapya ya UKIMWI nayo yamepungua
kutoka wastani wa 78,843 mwaka 2012/2013 hadi 69,000 mwaka 2014/2015. Idadi ya
watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI inakadiriwa kuwa milioni 1.4 kwa mwaka
2012/2013 na watu milioni 1.5 mwaka 2014/2015.
97.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kupungua kwa kasi ya
maambukizi, UKIMWI bado ni tishio linaloathiri maendeleo na maisha ya wananchi. Hatuna budi kuendelea kuchukua hatua
za dhati na madhubuti za kudhibiti maambukizi mapya, kutoa huduma za afya na
matibabu kwa wale walioambukizwa na kuwahudumia wale wenye mahitaji kutokana na
vifo vya wazazi hususan watoto yatima. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza
Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018
unaolenga kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 50, kupunguza vifo
vitokanavyo na UKIMWI na kuondoa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi
na virusi vya UKIMWI ifikapo 2018.
98.
Mheshimiwa Spika,
huduma za upimaji wa virusi vya UKIMWI
na uingizwaji kwenye mpango wa
matunzo na matibabu kwa wale wanaogundulika na
maambukizi ya VVU zinaendelea kutolewa. Jumla ya watu wanaoishi na
virusi vya UKIMWI wanaopata dawa za ARV ni 640,084, sawa na asilimia 43 ya watu
wote wenye maambukizi. Kati yao, asilimia 69 ni wanawake na watoto. Serikali
imeanza utaratibu mpya wa kutoa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa yeyote
atakayepimwa na kukutwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI tofauti na utaratibu
wa awali ambao mwathirika alianzishiwa dawa kutegemea idadi ya CD4. Utaratibu
huo umeanza katika Halmashauri 48 zenye kiwango kikubwa cha maambukizi na
hatimaye kueneza huduma hii Nchi nzima. Katika juhudi za kupunguza maambukizi
ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Serikali imeendelea kutoa huduma katika vituo 5,361 kati ya 5,863 vinavyotoa
huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini. Vilevile, Serikali
imeendelea kutoa elimu kwa umma katika masuala ya VVU, UKIMWI, Afya ya Uzazi na
Ujinsia. Kuanzia mwezi Julai 2016, Serikali itaanza zoezi la kupima kiwango cha
maambukizi kwa Nchi nzima, kila Mkoa, ikiwa ni mara ya nne zoezi hili kufanyika
nchini.
Hifadhi ya Mazingira
99.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kuweka na kutekeleza mipango na mikakati thabiti ya kutunza
mazingira kwa lengo la kutunza vyanzo
vya maji, Bioanuai, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na uharibifu wa misitu.
Aidha, Serikali imeandaa Kanuni mpya ya Mifuko ya Plastiki ya mwaka 2015
inayokataza kuzalishwa na kuingizwa nchini matumizi ya mifuko ya plastiki yenye
unene chini ya mikroni 50. Vilevile, Serikali imeendelea kufanya kaguzi katika
maeneo mbalimbali ili kubaini iwapo sheria za mazingira zinazingatiwa na
kuchukua hatua za kuvifungia viwanda tisa na kutoa onyo kwa viwanda 63. Taasisi
zinazohusika na usimamizi wa Sheria ya Mazingira hazina budi kuvisaidia kiufundi viwanda
husika ili visifungwe kwa muda mrefu kwani ni hasara kwa Taifa.
100. Mheshimiwa Spika, wakati
wa maadhimisho ya 54 ya Uhuru, tarehe 9 Desemba, 2015 Mheshimiwa Rais Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli alifanya uamuzi wa busara wa kuwataka wananchi wote
kuyatumia maadhimisho hayo kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao yanayowazunguka
na maeneo ya Taasisi za Umma. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza kwa
dhati wananchi wote, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi na Asasi za kiraia kwa
mwitikio mkubwa waliouonesha katika kushiriki na kufanikisha zoezi hilo la usafi.
101.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
umuhimu wa usafi wa mazingira, Serikali imeamua kwamba zoezi la usafi wa
mazingira litakuwa endelevu. Hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na
Ofisi ya Rais – TAMISEMI, tayari zimetoa Waraka maalum wa kuifanya kila
Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku maalum ya wananchi wote kufanya usafi wa
mazingira nchini kote. Napenda kuwahimiza Viongozi na Watendaji wote wa Wizara,
Mashirika na Taasisi za Umma na Sekta Binafsi,
Mikoa, Wilaya na Halmashauri zote nchini pamoja na Watendaji wa Mitaa,
Kata na Vijiji na Vitongoji na Wakuu wa Kaya kusimamia usafi wa mazingira
katika maeneo yao. Aidha, nawasihi Wananchi wote kudumisha utamaduni na tabia
nzuri ya kuhakikisha kuwa maeneo yao yanakuwa safi wakati wote ili kuboresha
afya zao na kuleta maendeleo endelevu nchini.
Menejimenti ya Maafa
102.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imeendelea kutekeleza jukumu la kuwalinda na kuwasaidia wananchi dhidi ya maafa
yaletwayo na matukio mbalimbali ya kiasili. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa
ni pamoja na Serikali kutoa Tani 31,184 za chakula kwa halmashuri 69
zilizokumbwa na tatizo la upungufu wa chakula katika mwaka 2015/2016. Kati ya
hizo, Tani 7,727 zilitolewa bure kwa kaya zisizo na uwezo na Tani 23,457
zilitolewa kwa bei nafuu ya Shilingi 50 kwa Kilo.
103.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia imetoa misaada mbalimbali ya
kibinadamu yenye thamani ya Shilingi Milioni 42.5 na kiasi cha Shilingi Milioni 143.5 kwa ajili
ya ununuzi wa mbegu za mihogo na mtama kwa waathirika wa maafa ya mafuriko,
mvua ya mawe na upepo mkali. Mikoa iliyopata misaada hiyo ni Mtwara, Mara,
Dodoma, Shinyanga, Iringa, Tanga, Pwani, Lindi na Tabora. Pia Shilingi Milioni
516 zilitolewa kama fidia kwa watu waliotakiwa kupisha ujenzi wa upanuzi wa
mtaro katika eneo la Buguruni - Mnyamani.
Serikali imeimarisha Mfumo wa Upatikanaji wa Taarifa za Tahadhari za
majanga kwa haraka kwa kujenga vituo 16 vya upimaji wa hali ya hewa na kuweka
vifaa vya kupima wingi na kasi ya maji katika vituo 10 vilivyopo katika mabonde
ya mto Pangani na mto Ruvuma. Aidha, Serikali imetoa mafunzo kwa Kamati za
Maafa katika wilaya 14 za mikoa mitano nchini. Katika mwaka 2016/2017, Serikali
itaendelea kuimarisha uratibu na menejimenti ya maafa nchini kwa kuanzisha
Wakala wa Usimamizi wa Maafa, kuzijengea uwezo Kamati za Maafa za Mikoa na
Wilaya na kuendelea kuimarisha Mfumo wa Taarifa za Tahadhari ya Awali.
Kudhibiti Dawa za Kulevya
104.
Mheshimiwa
Spika, dawa za
kulevya ni changamoto kubwa kwani huwaathiri watu wengi hasa vijana ambao ni
nguvu kazi ya Taifa. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia
Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ilifanya marekebisho ya Sera ya
Kupambana na Dawa za Kulevya na kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria Mpya ya
Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya na kupitishwa na Bunge lako Tukufu na kuanza
kutumika tarehe 15 Septemba 2015. Sheria hiyo inaipa Tume nguvu zaidi ya
kudhibiti na kupambana na tatizo hilo.
105.
Mheshimiwa
Spika, Tume
imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za biashara na matumizi ya dawa
za kulevya na kutoa huduma za matibabu kwa waathirika. Hadi kufika mwezi
Februari 2016, zaidi ya watumiaji 2,223 wamepata
huduma katika Hospitali za Muhimbili, Temeke na Mwananyamala. Tume kwa
kushirikia na Jeshi la Polisi wameendesha misako, doria na operesheni nchini
kwa lengo la kudhibiti uuzaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya,
ambapo wamefanikiwa kuteketeza mashamba ya bangi na mirungi katika mikoa ya
Kilimanjaro, Arusha na Mara. Katika mwaka 2015/2016, jumla ya watuhumiwa 43
walikamatwa na kiasi cha kilo 37.2 na kete 156 za dawa aina ya heroin na bangi.
Pamoja na ukamataji huo, Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa hukumu kwa kesi kubwa
nne za dawa za kulevya. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itakamilisha utaratibu
wa kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza
ufanisi. Mamlaka itashirikiana na Jeshi la Polisi kubaini mtandao wa wahalifu
wa ndani na nje ya nchi unaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa dawa za
kulevya nchini na kuwafikisha wahusika Mahakamani.
USTAWISHAJI MAKAO MAKUU DODOMA
106.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2015/2016, Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu imepima viwanja 957 katika maeneo ya Mkalama,
Nkuhungu Kusini na Mahungu. Vilevile, jumla ya viwanja 6,599 vilisanifiwa
katika eneo la ukubwa wa Hekta 493 na kutoa vibali 275 vya ujenzi. Katika mwaka
2016/2017, Mamlaka inatarajia kuandaa ramani za jumla na ramani za kina katika
maeneo ya Ihumwa na Hombolo pamoja na kupima viwanja vipya 4,000 katika maeneo
mbalimbali ya Mji wa Dodoma na kujenga kwa kiwango cha lami barabara zenye urefu
wa kilometa 23.
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
107.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kushiriki kwenye utengamano wa
kikanda na kimataifa na kuendeleza Diplomasia ya Uchumi na Siasa kwa kuzingatia maslahi
muhimu ya Nchi yetu. Mathalani, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Miaka Mitatu (2016-2018)
wa Ushirikiano kati ya Tanzania na China. Mpango huo umeainisha miradi ya
kipaumbele ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali nchini. Ushirikiano huo umelenga
kutumia fursa ya Dola za Marekani Bilioni 10 zitakazotolewa na Serikali ya
China chini ya Mpango wa kuzisaidia Nchi nne za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika Mkutano wa Sita wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa
la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Johannesburg, Afrika
Kusini tarehe 5 Desemba 2015. Nchi nyingine zitakazofaidika na Mpango huo ni
Afrika Kusini, Ethiopia na Kenya.
Serikali pia imesaini Mkataba wa ushirikiano na Serikali ya Japan kwa
ajili ya ujenzi wa Gridi ya umeme na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kusaidia
mpango wa maboresho ya Terminal Two ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere.
108.
Mheshimiwa
Spika, ili kuwezesha Nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025,
Serikali itaendelea kusimamia na kutekeleza diplomasia thabiti ambayo
itachangia katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu ya Tanzania.
Aidha, itakuza ubia wa kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Barani
Afrika na wadau wengine wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapata
manufaa ya fursa za utandawazi.
URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI
109.
Mheshimiwa
Spika, ili kazi
zote zilizopangwa kutekelezwa zifanyike kwa ufanisi, tunahitaji uratibu mzuri
wa sekta zote ili kila mmoja atekeleze wajibu wake kikamilifu. Hivyo, kuanzia
mwezi Julai, 2016 Serikali itaanza kutumia mfumo wa wazi wa kielektroniki wa
kufuatilia uwajibikaji na utendaji kazi kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni na
Miongozo mbalimbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mfumo huo ni muhimu ili
kuhakikisha kuwa utendaji kazi unaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano
katika kufikia malengo yaliyopangwa. Mfumo huo utarahisisha ufuatiliaji wa
utekelezaji wa shughuli za Serikali kulingana na Ilani ya Chama Mapinduzi ya
mwaka 2015, Mipango ya Maendeleo ya Kitaifa, Ahadi na Maagizo ya Viongozi
Wakuu. Aidha, Mfumo huo utapunguza ucheleweshaji wa utekelezaji, mwingiliano wa
majukumu na gharama zisizo za lazima katika utendaji kazi.
HITIMISHO
110.
Mheshimiwa
Spika, nimetumia
muda mrefu kuelezea baadhi ya shughuli ambazo Serikali ya Awamu ya Tano
itazipatia kipaumbele. Kabla ya
kuhitimisha Hotuba yangu, napenda kusisitiza masuala machache yafuatayo:-
(i)
Tunayo
changamoto kubwa ya kutumia rasilimali fedha kidogo tuliyonayo kukidhi mahitaji
makubwa ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mathalani, upo upotevu wa mapato kwa kushindwa kudhibiti na kusimamia
mapato na matumizi ya fedha za umma.
Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji
mapato na kuhakikisha kwamba fedha za umma zinatumika kulingana na sheria na
kanuni za matumizi ya fedha za Serikali;
(ii)
Tumedhamiria
kufanya mapinduzi ya viwanda ili kujenga uchumi imara kwa faida ya
wananchi. Hata hivyo, tunalo jukumu kwa
kila mmoja wetu kuunga mkono dhamira ya kweli ya Serikali ili kufikia lengo
hili. Tuungane na Mheshimiwa Rais kuondoa kasoro zilizopo kwa kupunguza urasimu
katika kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje; kuimarisha huduma na miundombinu
ya kiuchumi kama vile umeme, barabara, reli, maji na rasilimali watu yenye
ujuzi kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa na ambavyo havifanyi kazi vianze
kufanya kazi. Ni muhimu kuhimiza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vyenye
kutumia malighafi iliyopo nchini kwa faida na maendeleo ya wananchi wetu.
Watanzania na wawekezaji kutoka nje mnakaribishwa kuwekeza;
(iii)
Tunahitaji
kuboresha Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na bidhaa za masoko kama njia ya
kujenga muunganisho wa sekta hizi na viwanda ili kuongeza thamani kwa lengo
la kuondoa umaskini kwa wananchi wetu
ambao wengi wao ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Tutumie akili, maarifa na
nguvu zetu kuhakikisha kwamba wananchi wanapata nyenzo na pembejeo za
kuwaongezea uwezo wa uzalishaji wenye tija kwa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi
na misitu. Tumedhamiria kuupitia mfumo wa masoko ya mazao yetu ili wakulima
wauze kwa faida mazao yao;
(iv)
Tunalo
jukumu kubwa la kuboresha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa
maji safi na salama na miundombinu ya umeme hasa vijijini. Tumeanza utaratibu wa kutoa elimu bila malipo
kwa wanafunzi, kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne;
(v)
Bado
tunalo tatizo kubwa la biashara na matumizi ya Dawa za Kulevya. Tuunge mkono juhudi za Serikali katika vita
hii kubwa ya kupambana na tatizo la Dawa za Kulevya ambazo zinaleta athari
kubwa kwa wananchi hususan vijana;
(vi)
Umuhimu
wa kurejesha maadili katika utumishi wa umma ni suala la kipaumbele. Ni vyema
kila mtumishi wa umma kuzingatia sera, sheria na kanuni kuhusu Maadili ya
Viongozi na Watumishi wa Umma. Aidha, ni vyema viongozi na watumishi wa umma
kila mmoja kwa nafasi yake, awajibike kwa cheo na dhamana aliyopewa katika kuwatumikia
wananchi. Dhana ya “Kutumbua Majipu”
iwe kichocheo cha kuwabaini na kuwarekebisha wale wote wenye dhamira ya kukiuka
maadili kwenye nyadhifa zao na katika kuwatumikia wananchi;
(vii)
Tunayo
changamoto ya ukuaji wa uchumi ambao hauendi sambamba na kasi ya upatikanaji wa
ajira. Aidha, zipo dalili kwamba vijana
wetu wamekuwa wakitumia muda mwingi kufanya shughuli ambazo hazichangii sana
katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Tuendelee kuwahimiza vijana na kujenga
utamaduni kwa kila mwananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi kwa
maendeleo yetu. Tuunge mkono falsafa ya
“Hapa Kazi Tu” na kwamba Asiyefanya kazi na Asile; na
(viii)
Mwisho,
niwaombe Watanzania wote kuendelea kuishi kwa amani na utulivu. Tunayo Nchi
nzuri na Watanzania wote ni watu wenye upendo. Tudumishe amani, umoja na mshikamano
kwa kuwaunga mkono viongozi wetu ili tuongeze kasi ya kuleta maendeleo katika Nchi
yetu kwa maana Umoja ni Nguvu. Sekta
Binafsi, ambayo ndiyo Injini ya Ukuzaji Uchumi wa Taifa letu, isiwe na
tashwishwi hata kidogo. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuienzi na
kuisaidia Sekta Binafsi katika kuchangia maendeleo ya Taifa letu.
SHUKRANI
111. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu
Mawaziri kwa ushirikiano walionipa tangu wateuliwe. Aidha, nawashukuru
Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu
Kiongozi, kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017. Nawashukuru
Watanzania wote kwa kushiriki katika ujenzi wa Taifa.
112. Mheshimiwa
Spika, vilevile, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge
wa Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na wenye Ulemavu); Mheshimiwa Dkt. Abdallah Saleh Possi, Mbunge, Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Anthony Peter
Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,
Ajira na Vijana) kwa msaada na
ushirikiano wao mkubwa katika
utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru vilevile
Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu,
Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua; Bwana Uledi A. Mussa na Bwana Eric F. Shitindi kwa
ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi
katika kipindi hiki. Nawashukuru kwa kukamilisha kwa wakati maandalizi yote ya
Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2016/2017.
113. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2015/2016, Nchi yetu imepata misaada na
mikopo kutoka kwa Wahisani wetu mbalimbali. Misaada na mikopo hiyo imetoka kwa
Nchi rafiki, Nchi fadhili, Taasisi za Fedha duniani, Mashirika ya Umoja wa
Mataifa, Mifuko mbalimbali ya Fedha duniani, madhehebu ya dini na Mashirika
yasiyo ya Kiserikali. Misaada na mikopo hiyo imechangia sana katika kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Napenda kuwashukuru wote kwa dhati na kuwahakikishia kuwa Watanzania
tunathamini misaada na mikopo waliyotupatia na tutaendelea kushirikiana nao
katika harakati za kuleta maendeleo ya Taifa letu.
114.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia
fursa hii kuwashukuru kwa dhati wapiga kura wangu wa Jimbo la Ruangwa kwa imani
na heshima kubwa waliyonipa ya kunikubali na kunichagua kuwa Mbunge wao.
Napenda kuwaahidi kuwa sitawaangusha. Ninawashukuru viongozi wenzangu wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote kwa
ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka kwao ambao umeniwezesha kutekeleza jukumu
hili kubwa la kusimamia utendaji wa Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi
wa Shughuli za Serikali Bungeni. Asanteni
sana.
115.
Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kuishukuru familia yangu hususan mke wangu
Mary Majaliwa na watoto wangu wote kwa kuniombea na kunipa moyo mara baada ya
kuteuliwa kushika wadhifa huu. Maombi yao yamenipa nguvu ya kutekeleza majukumu
yangu.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA 2016/2017
116.Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
2016/2017, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako Tukufu
liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Mbili Thelathini na Sita,
Milioni Mia Saba Hamsini na Tisa, Mia
Nane Sabini na Nne Elfu, Mia Saba na Sita (236,759,874,706). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na Moja, Milioni Mia Tano Sitini na Nne, Mia Mbili
Tisini na Tatu Elfu, Mia Saba Sabini na Tatu (71,564,293,773) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na
Shilingi Bilioni Mia Moja Sitini na Tano, Milioni Mia Moja Tisini na Tano, Mia
Tano Themanini Elfu, Mia Tisa Thelathini na Tatu (165,195,580,933) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
117.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa
hoja.
0 comments:
Post a Comment