Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Canada hapa nchini
Alexandre Leveque mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es
Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ameikaribisha nchi ya Canada kushirikiana na serikali yake ya awamu ya
tano katika kuleta mageuzi ya kiuchumi, hususani katika uwekezaji kwenye
sekta ya Kilimo, Madini, Uvuvi na Huduma za kijamii.
Rais Magufuli
ametoa ujumbe huo alipokuwa akizungumza na Balozi wa Canada hapa nchini
Mheshimiwa Alexandre Le've'que aliyekutana nae Ikulu Jijini Dar es
salaam na kupokea barua yenye ujumbe wa Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa
Justin Trudeau.
Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amesema
serikali yake hairidhishwi na jinsi kilimo cha Tanzania
kisivyowanufaisha wakulima ipasavyo, na hivyo ameikaribisha nchi ya
Canada hususani sekta binafsi ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania
kujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na uvuvi ili kuzalisha
ajira na kuongeza thamani ya mazao kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote
mbili.
Dkt. Magufuli pia ametaka Canada yenye uwezo mkubwa
kiteknolojia na mtaji ishirikiane na Tanzania katika uwekezaji kwenye
sekta ya madini na gesi kwa kujenga viwanda vya kuchakata madini ndani
ya nchi ya Tanzania na pia rasilimali ya gesi ambayo mpaka sasa Tanzania
imethibitika kuwa na hifadhi ya futi za ujazo zaidi ya Trilioni 57.
"Mheshimiwa
Balozi Alexandre Le've'que naomba ukamweleze Waziri Mkuu wa Canada
Mheshimiwa Justin Trudeau kuwa Tanzania na Canada sio tu ni nchi
marafiki bali pia ni ndugu wenye uhusiano wa kihistoria. Ningependa
kuona Canada inashirikiana na serikali yangu, katika juhudi zake za
kuachana na usafirishaji wa mchanga wa madini badala ya madini
yaliyochakatwa na pia kuachana na usafirishaji wa mazao yakiwa ghafi"
Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Balozi wa Canada hapa nchini
Mheshimiwa Alexandre Le've'que amemhakikishia Rais Magufuli kuwa
atafikisha ujumbe huo kwa Waziri Mkuu Canada Mheshimiwa Justin Trudeau,
na amebainisha kuwa nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika
juhudi zake za kuimarisha uchumi, hasa baada ya kujionea juhudi za Rais
Magufuli katika kukabiliana na rushwa, kuongeza ukusanyaji wa mapato na
kusimamia nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma.
Wakati huo huo,
Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Aljeria Mheshimiwa
Abdelaziz Bouteflika ambaye pamoja na kumpongeza kwa hatua anazochukua
katika uendeshaji wa serikali, amemhakikishia kuwa Aljeria ipo tayari
kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania huku
akitaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni nishati na kilimo.
Ujumbe wa
Rais Bouteflika umewasilishwa kwa Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es
salaam na Balozi wa Aljeria hapa nchini Mheshimiwa Belabed Saada.
Rais
Magufuli amemhakikishia Rais Bouteflika kuwa Serikali yake itaendeleza
na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Aljeria, na kwamba hivi
karibuni imepanga kuanzisha ofisi za Ubalozi katika nchi hiyo.
Kuhusu
sekta za nishati na kilimo, Rais Magufuli amesema serikali yake
inakaribisha uwekezaji kutoka Aljeria hasa wakati huu ambapo Tanzania
imethibitika kuwa na kiasi kikubwa cha gesi, na kwa upande wa kilimo
ametoa wito kwa Aljeria kushirikiana na Tanzania katika mpango wake wa
kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, ikiwemo usindikaji wa
zabibu, viwanda vya nguo, viwanda vya ngozi na nyama na viwanda vya
kusindika minofu ya samaki.
"Naomba ukamweleze Mheshimiwa Rais
Bouteflika kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano
wake na Aljeria na kwamba imefurahishwa sana kuona Aljeria ipo tayari
kusaidia juhudi za kuendeleza sekta ya kilimo nchini Tanzania" Rais
Magufuli amemweleza Balozi Belabed Saada.
Katika hatua nyingine, Rais
Dkt. John Pombe Magufuli ameagana na Balozi wa Vatican hapa nchini
Mheshimiwa Francisco Montecillo ambaye anamaliza muda wake baada ya
kuiwakilisha Vatican kwa muda wa miaka minne na nusu.
Home
News
Slider
Tanzania na Canada kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuleta mageuzi ya Kiuchumi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment